• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 1:20 PM
Wafugaji Nakuru walalamikia nyani kunyonya maziwa ng’ombe wakiwa malishoni     

Wafugaji Nakuru walalamikia nyani kunyonya maziwa ng’ombe wakiwa malishoni    

NA RICHARD MAOSI.

WAFUGAJI ng’ombe kutoka mtaa wa Pipeline viungani mwa Jiji la Nakuru wamelalamikia kuhangaishwa na nyani ambao hunyonya maziwa yote mifugo wanapokuwa malishoni.

Sio nyani tu, bali pia wezi wamekuwa wakiruka uzio au kuta na kuingia kwenye maboma yao kwa lengo la kukama maziwa usiku wenyeji wanapokuwa wamelala.

Wanateta hilo linawasababishia hasara wakulima wadogo, na kuwafanya waagizie maziwa kutoka maeneo jirani ya Dundori, Lanet, Gwa Kiongo na Ol-Kalou.

Mchana kutwa wakulima hushinda wakiwafukuza nyani kutoka kwenye mashamba yao hasa msimu huu ambao mahindi yamekomaa, ila mara nyingine wanashindwa kuwadhibiti idadi yao ikizidi.

Changamoto kubwa inayowakumba wakulima wadogo hapa ni; hawana uwezo kuajiri vibarua kuwalindia mifugo nyakati za mchana, hivyo basi huwaacha mifugo wao wakizurura.

Irene Wambere mfugaji wa ng’ombe na kondoo kutoka eneo la Mzee Wanyama, anasema nyani ni wanyama werevu sana kiasi kwamba wamejifunza kuishi vizuri na mifugo hasa ng’ombe na mbuzi.

“Ndio sababu wengi wetu tuliacha kukama maziwa kitambo kwa sababu siku ikiwa nzuri mfugaji anaweza kupokea labda vikombe viwili tu vya maziwa kwa siku,” akasema.

Nyani kutoka Mbuga ya Wanyama ya Ziwa Nakuru wakiruka ukuta na kuingia kwenye boma la watu katika mtaa wa Lakeview Nakuru. PICHA|RICHARD MAOSI.

Bi Wambere anasema ni jambo la kawaida nyani kutangamana na ng’ombe, ikizingatiwa kuwa Mbuga ya Wanyama ya Ziwa Nakuru inapakana na sehemu ya Mzee Wanyama.

Kwa miaka mingi anasema wakazi wa mitaa ya Pipeline, Mwariki, Lake View, Free Area na Manyani wamekuwa wakiomba serikali ya Kitaifa na Shirika la Uhifadhi la Wanyama Pori (KWS), kutafuta suluhu la kudumu, ili kukabiliana na kero ya nyani wasumbufu.

Edwin Warui, ni mfugaji mwingine Pipeline ambaye ng’ombe wake wa maziwa hawampi faida kamwe kufuatia kero ya nyani.

“Inaonekana ninafugia ng’ombe wangu nyani. Kazi yao imekuwa kuwanyonya wakiwa malishoni,” Bw Warui akaambia Taifa Leo Dijitali.

Hata hivyo, malalamishi yao yamekuwa yakigonga mwamba jambo linalowalazimu kutafuta njia mbadala ya kujilinda dhidi ya hasara za mara kwa mara.

Aidha, wanasema kuwa bei ya kununua vyakula vya kulisha mifugo huwa imepanda sana kiasi kwamba siku hizi wakulima wengi wanajitengenezea malisho nyumbani ifikapo msimu wa kiangazi.

Hili linajiri siku chache baada ya wafanyibiashara katika barabara ya Nakuru Nairobi kulalamikia ongezeko la idadi ya nyani ambao wamekuwa wakiwaibia bidhaa zao.

Wengine, wamekuwa wakitwanga walevi.

Ni jambo ambalo limepokelewa kwa hisis mseto huku baadhi ya wakazi wakidai kuwa mtaa wa Pilepine hushuhudia visa vingi vya uhalifu kila siku.

  • Tags

You can share this post!

OCS mpenda hongo Ruai Nairobi akamatwa  

Naisula Lesuuda kati ya wabunge 10 bora wa kike wanaochapa...

T L