MakalaSiasa

Mlima Kenya: 'Bibi Harusi' mpya kisiasa anayeng'ang'aniwa

September 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

ENEO la Mlima Kenya limegeuka kuwa ‘Bi Harusi’ wa kisiasa ielekeapo 2022, huku wanasiasa wakuu wanaopania kuwania urais mwaka huo wakikita mikakati na mikataba ya kisiasa kwa njia za kulivutia.

Mbali na hayo, wengi wamekuwa wakifanya ziara mbalimbali katika eneo hilo, katika kile kinafasiriwa kuwa mikakati ya mapema ya kurusha ndoano kuwarai wakazi kuwaunga mkono.

Eneo hilo linang’ang’aniwa kisiasa na Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga, kiongozi wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi.

Dkt Ruto amekuwa akifanya ziara nyingi katika kaunti mbalimbali za eneo hilo, akishiriki hafla za kuchangisha fedha kwenye makanisa, shule na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo, akijinadi kama “mtumwa” wa Rais Uhuru Kenyatta.

Eneo hili linajumuisha kaunti kumi zikiwemo Nyeri, Kiambu, Nyandarua, Kirinyaga, Tharaka Nithi, Meru, Embu, Kiambu, Murang’a na Laikipia.

Kwenye takwimu za idadi ya kura zilizotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) mnamo 2017, eneo hilo lina wapigakura 4.6 milioni waliosajiliwa, hali ambayo wachanganuzi wanataja kama sababu kuu ya kung’ang’aniwa na vigogo hao.

“Idadi kubwa ya wapigakura ni mojawapo ya sababu kuu ya eneo kuwa kivutio kikubwa cha wanasiasa. Wanaliona kuwa litakalojaza kapu ya kura watakazohitajika kujaza ili kuibuka washindi kwenye uchaguzi huo,” asema Prof Peter Kagwanja, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa.

Mdadisi huyo pia anasema kuwa kutokuwepo kwa mrithi rasmi wa kisiasa wa Rais Kenyatta atakapong’atuka uongozini, ndiyo sababu nyingine inayowavutia wanasiasa wengi.

Kulingana na wachanganuzi, sababu kuu ya Dkt Ruto kuwekeza kisiasa katika eneo hilo ni imani kwamba bado atakuwa na uungwaji mkono, kutokana na mkataba wa kisiasa waliobuni na Rais Kenyatta mnano 2012 kwa kubuni Muungano wa Jubilee.

Wanasema kuwa imani hiyo inadhihirishwa na hatua yake kubuni kundi la ‘Tanga Tanga’ ambalo linajumuisha wabunge ambao wamekuwa wakiandamana naye katika hafla mbalimbali, wakimhakikishia kwamba eneo hilo “litarudisha mkono” kwa kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Hatua ya Dkt Ruto kubuni kundi la ‘Tanga Tanga’ ni kuhakikisha kuwa anadumisha uungwaji mkono wake wa kisiasa dhidi ya ‘uvamizi’ wowote wanasiasa kama Odinga na Kalonzo, anaowaona kama tishio kuu kwa azma yake,” asema Mark Bichachi, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kwa Bw Odinga, wachanganuzi wanasema kuwa hatua yake kubuni handisheki na Rais Kenyatta ni kuhakikisha kuwa amepata uungwaji mkono wa ukanda huo.

Tangu mwafaka huo wa kisiasa, Bw Odinga amekuwa akizuru eneo hilo bila hofu, hali ambayo ilikuwa kinyume kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2017.

Vilevile, amekuwa akizindua miradi mbalimbali ya maendeleo, huku akipokewa na viongozi kama magavana, maseneta na hata wabunge.

Mwezi uliopita, Bw Odinga alibuni kundi maalum la wanasiasa, ambapo duru zinaeleza litakuwa likinadi ajenda na mikakati yake katika eneo hilo.

Kundi hilo linajumuisha Gavana Anne Waiguru (Kirinyaga), mbunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), aliyekuwa Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Nyeri Priscilla Nyokabi, mbunge maalum Maina Kamanda kati ya wengine.

Mabwana Kamanda na Wambugu wamekuwa wakiongoza kundi la ‘Kieleweke’ ambalo limekuwa likipinga azma ya Dkt Ruto kuwania urais, likimtaja kuwa mfisadi.

Wiki iliyopita, Bw Kamanda alisema kuwa kundi hilo linalenga kubuni muungano wa kisiasa na chama cha ODM, ili kuuza sera za Bw Odinga katika eneo hilo.

“Tunadhamiria kupanua muungano wetu wa kisiasa kwa kuwajumuisha viongozi kama Odinga, Kalonzo na Mudavadi, ili kumzima Dkt Ruto. Muungano huo unalenga kuhakikisha kuwa eneo hili halionekani kama choyo kisiasa,” akasema Bw Kamanda.

Bi Waiguru naye alisema kuwa ukanda huo utamuunga mkono Bw Odinga, akigeuza msimamo wake mkali aliokuwa nao dhidi ya Bw kinara huyo wa ODM.

Bw Odinga pia amekuwa akipokea wajumbe mbalimbali kutoka ukanda huo katika afisi yake ya Capitol Hill jijini Nairobi, wakijumuisha wazee na viongozi wa zamani wa kisiasa.

Bw Musyoka naye amekuwa akifanya ziara mbalimbali katika eneo hilo, hasa katika Kaunti ya Murang’a, ambako ameshiriki katika michango kadhaa ya kuchangisha pesa.

Ingawa hajaeleza rasmi azma yake kisiasa, wachanganuzi wanasema kuwa huenda ziara zake zinalenga kupanua ajenda zake za kisiasa.

“Ikumbukwe kuwa Bw Musyoka alikuwa Makamu wa Rais chini ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki, hivyo bado anaonekana kuwa mtu wa karibu wa jamii za GEMA, hasa Wakikuyu,” asema Prof Ngugi Njoroge.

Sawa na Bw Odinga, Bw Mudavadi pia amekuwa akipokea wajumbe kutoka eneo hilo, hali ambayo wachanganuzi wanataja kuwa mikakati ya kujipanga kupata uungwaji mkono.

Wachanganuzi wanasema kuwa Bw Kibaki pia alipendelea Bw Mudavadi kuwa mirthi wake mnamo 2012 kupitia chama cha UDF, ishara kuwa vilevile yumo mbioni kujaza pengo la kisiasa linaloonekana kuwepo.