MOHAMMED: Muafaka wa Uhuru na Raila hakika ni laana ya aina yake
Na MAINA MOHAMMED
LABDA ni mojawapo ya masuala yatakayoandika upya historia ya siasa za upinzani Kenya. Ama karata aliyocheza Rais Kenyatta na kuyumbisha upinzani ni laana inayotafuna mustakabali wa taifa. Ni karata zilizomyeyusha gwiji wa upinzani Raila Odinga na sasa zimemlaza?Kalonzo Musyoka.
Matokeo yake ni kuwa wananchi tumepigwa chenga na kuachwa hoi. Hatuna tena viongozi wa upinzani wenye sifa na uwezo wa kuiwajibisha serikali.
Awali, kivuli cha Bw Odinga kilitisha serikali na mafisadi wake wote, hali iliyopelekea wao kupunguza kasi ya kuhujumu uchumi pamoja na miiko ya utawala bora.
Alipomezwa Bw Odinga, matumaini yetu yakageuka kwa vigogo wenza ndani ya NASA, Bw Musyoka na Bw Mudavadi.
Lakini kule Tseikuru, Kaunti ya Kitui, Bw Musyoka naye akabwaga manyanga na kutangaza peupe?kuwa yuko radhi kuwa ‘mtu wa mkono’ wa Rais Kenyatta.
Kama zawadi kwa uamuzi wao wa ‘busara’ wa kuacha tabia ya ‘kikorofi ‘ ya kuibana serikali ya Jubilee. Bw Odinga na Bw Musyoka wakavuna unono nalo taifa linaelekea jehanamu.
Bw Odinga akapewa wadhifa wa mjumbe mshirikishi wa Miundombinu Afrika ndani ya Umoja wa?Afrika (AU) naye Bw Musyoka sasa akatunukiwa ujumbe maalumu wa amani nchini Sudan Kusini.
Hali hii sasa inaibua suala zito la ni ipi hatima ya upinzani Kenya. Mfumo wetu wa utawala umejengwa juu ya msingi wa uwepo wa mgawanyo wa madaraka ili kudhibiti serikali.
Wabunge wa upinzani na viongozi wa kambi ya upinzani ndio vidhibiti mwendo vya serikali. Ama serikali zote duniani zina tabia ya kukiuka mipaka kuhusiana na matumizi ya pesa za umma na haki za kimsingi za raia.
Hapa Kenya kukosekana kwa upinzani imara na makini, ni leseni ya mafisadi kujihodhia utajiri haramu. Tangu Jubilee kuchukua hatamu za kuongoza nchi madudu ya ufisadi yametafuna nchi nusura ibaki mifupa.
Katika kila idara na wizara ya serikali, pameripotiwa kufisadiwa kwa mamilioni ya pesa.
Na ingawa kwenye awamu yake hii ya mwisho Rais Kenyatta amewavutia pumzi mafisadi serikalini, mambo bado sio shwari hata kidogo.?Mafisadi wamebadili mbinu kwenda na nyakati.
Fauka ya hayo, maelekezo mengi aliyotoa Rais Kenyatta kupambana na rushwa na wizi yamebaki tu maneno bila vitendo.
Kwa mfano, kuchunguzwa kwa chanzo cha mali ya watumishi wakuu serikalini bado ni suala la mahubiri. Hata watuhumiwa wa ufisadi wa mamilioni waliobururwa mahakamani bado wana wigo mpana na kujinasua.
Kwa namna hii, tunahitaji sana upinzani makini na wenye nguvu. Upinzani wa sasa ni sawa na ng’ombe asiyekuwa na pembe vitani.
Musa wetu amegeuka kuwa sehemu ya watesi wetu.