• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 2:21 PM
Mpango wa kuimarisha maisha ya vijana wanaorandaranda Nakuru

Mpango wa kuimarisha maisha ya vijana wanaorandaranda Nakuru

Na GEOFFREY ONDIEKI

IDADI ya vijana wa kurandaranda mitaani wasio na makao inazidi kuongezeka kila kukicha Nakuru licha ya serikali ya kaunti hiyo kuweka mikakati ya kumaliza tatizo hilo.

Serikali hiyo haijapata suluhisho la kudumu la kudhibiti zaidi ya chokoraa 440.

Awali Gavana wa Kaunti ya Nakuru Lee Kinyanjui alitangaza kuwa serikali ina mipango ya kurejesha makwao familia hizo za mitaani, mpango ambao ungali kutekelezwa hadi sasa.

Kwenye mahojiano na mkurugenzi wa masula yanayohusu jamii Bw Joseph Kimemia, alisema kuwa serikali ya kaunti inaandaa basari kwa wanafunzi 53 ambao walionyesha ari ya kurejea shuleni kuendelea na masomo yao.

“Kwa sasa tunandaa basari ya kuwafadhili zaidi ya wanafunzi 53 ambao wangependa kurudi shuleni,” alisema Bw Kimemia.

Kulingana naye, kaunti ya Nakuru itatumia kitita cha Sh2 milioni kufadhili mafunzo ya watoto hao kuanzia mwaka 2020.

Vijana wanaorandaranda katika mitaa ya Kaunti ya Nakuru wapata ushauri nasaha katika hospitali ya Nakuru Level Five. Picha/ Richard Maosi

Alikiri kuwa watoto wengi wameathiriwa vibaya na uraibu wa dawa za kulevya na hivyo wanahitaji ushauri nasaha ili kurejelea katika hali yao ya kawaida.

Jumla ya taasisi nane za mafunzo kwenye kaunti ndogo saba Nakuru zitatwaa wanafunzi hao 53.

Taasisi ya mafunzo ya Dundori katika kaunti ndogo ya Bahati itapokea wanafunzi 14, ambao ni kiasi kikubwa cha wanafunzi kuliko taasisi yoyote.

Taasisi zingine ambazo zitapokea wanafunzi ni pamoja na taasisi ya mafunzo ya Mutethie katika kaunti ndogo ya Naivasha na wanafunzi 13, taasisi ya mafunzo ya Subukia katika kaunti ndogo ya Subukia na wanafunzi 12, taasisi ya mafunzo ya Nakuru katika kaunti ndogo ya Nakuru Mashariki na nyinginezo.

Ushauri

Watoto wengine, alisema hawapo katika hali nzuri ya kurejea shuleni moja kwa moja na kuwa wanahitaji ushauri nasaha kurejelea hali ya kawaida.

Bw Kimemia alisema serikali ya kaunti ina mipango ya kuwashirikisha washikadau kutoka sekta mbalimbali ili kusaidia kumaliza tatizo hilo.

“Watoto wa kuranda randa mitaani ni tatizo linalokumba sio tu kaunti ya Nakuru, bali kaunti nyingi nchini na tupo katika mstari wa mbele kumaliza tatizo hilo. Tumepanga kuleta washikadau wengine kwenye sekta hii kutusaidia,” alisema Bw Kimemia.

Washikadau ambao aliwataja ni pamoja na idara ya watoto na idara ya elimu.

Familia za kurandaranda mitaani zinapitia hali ngumu katika mitaa ya mji wa Nakuru na miji mingine nchini Kenya, na suluhisho la kudumu lingali kitendawili.

Wahisani wengi wamejaribu kuingilia kati kusaidia hali ufanisi wa hadi asilimia 100 bado.

Mwanzoni mwa mwaka 2019 watoto wa mitaani 42 kutoka Nakuru walitelekezwa eneo la Torongo katika Kaunti ya Baringo.

Ni hatua ambayo ilikosolewa vikali na viongozi kadhaa wa humu nchini na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu.

You can share this post!

Njama ya Uhuru, Raila kusukuma BBI

Kura yalalama kuhusu wizi, uharibifu wa vifaa vya barabarani

adminleo