Mpeketoni yapona makovu ya mashambulio ya Al-Shabaab
NA KALUME KAZUNGU
DOA jeusi lililosababishwa na shambulio la Al-Shabaab mnamo Juni 2014 linazidi kusafishwa na kuacha mji wa Mpeketoni ukiwa mweupe.
Hii ni kutokana na hatua kubwa za kimaendeleo ambazo zimepigwa karibu miaka 11 sasa tangu Al-Shabaab washambulie mji huo wa Kaunti ya Lamu na kusababisha vifo vya wanaume karibu 90 kwa usiku mmoja.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini wazi jinsi mji wa Mpeketoni ulivyopona makovu ya mashambulio hayo ya Al-Shabaab kwani maendeleo yanazidi kunoga karibu sekta zote kila kuchao eneo hilo.
Utapata biashara ya nyumba za kukodisha ikitia fora kwani wapangaji,hasa wale waliokuwa wakikimbilia kuishi kisiwa cha Lamu wamekuwa wakihama kuja kuonja mandhari mapya ya mji wa Mpeketoni.
Wamiliki wa nyumba za kukodi waliozungumza na Taifa Leo mjini Mpeketoni na viunga vyake walisema kwa sasa hakuna tofauti kubwa kati ya Biashara ya nyumba kisiwani Lamu na Mpeketoni.
Bw Samuel Karanja anasema nyumba yake ya vyumba kumi vyote vimekodishwa na wapangaji.
Nyumba ya vyumba viwili,jiko na choo kwa mfano,huenda kati ya Sh10,000 na Sh15,000 kwa mwezi kulingana na pahali nyumba ipo,iwe ni katikati au nje ya mji wa Mpeketoni.
“Mpeketoni imepanuka. Kinyume na miaka ya awali baada ya shambulio na mauaji ya halaiki yaliyotekelezwa na Al-Shabaab ambapo yalisukuma wengi kutoroka mji huu,Leo twajivunia kwamba usalama umedumishwa na hadhi ya Mpeketoni imerejea hadi kupanuka hata zaidi. Kila mtu Sasa ataka kujinyakulia ardhi Na kujiendeleza Mpeketoni. Mpeketoni ni mji mwafaka wa biashara ya aina yoyote ile,” akasema Bw Karanja.
Mbali na biashara ya nyumba za kukodi kuongezeka,wakazi pia wamejitosa kwenye kilimo ambacho kinafanya vyema zaidi.
Soma Pia: Wanawake wasiojua kuendesha baiskeli hatarini kukosa waume
Utapata mashamba yaliyojaa mahindi,hasa kupitia kilimo cha unyunyizaji maji wakati au msimu wowote ule,uwe ni wa mvua au kiangazi.
Bi Susan Mwangi,mkulima eneo la Bakanja, vitongojini mwa mji wa Mpeketoni, anasema kinyume na kisiwa cha Lamu ambapo wakazi hulazimika kujinunulia vyakula Na mboga, Mpeketoni mambo ni tofauti kwani wengi hutumia bidhaa kutoka mashambani mwao,hivyo kupunguza gharama ya maisha.
“Wewe ukiwa na bidii zako hapa Mpeketoni hutalia njaa kama wengine. Waweza jikodishia shamba lako’ ukalima nyanya,mahindi,pojo,maharagwe na kadhalika. Ukijipanga vyema hapa maisha yatakwendea nywe,” akasema Bi Mwangi.
Barabara za mji Wa Mkepetoni pia zimeboreshwa baada ya serikali ya kaunti ya Lamu kuweka mawe maalumu (cabro), hivyo kuufanya mji wa Mpeketoni kung’ara vilivyo.
Isitoshe,Biashara ya uchukuzi pia imenoga kwani kampuni nyingi za magari ya usafiri wa umma (PSV) zimefungua matawi au ofisi zake za kukatia tiketi mjini Mpeketoni.
Bw Francis Waweru,mkazi wa Mpeketoni, aliiomba serikali kuzidisha ulinzi eneo la Mpeketoni na viunga vyake ili yaliyorekodiwa eneo hilo 2014 yasijirudie tena.
Mji Wa Mpeketoni Ni wa pili kwa ukubwa baada ya ule wa kisiwa cha Lamu.
Miji mingine mikubwa ya Lamu ni Mokowe, Witu, Faza, Kizingitini na Kiunga ulioko mpakani mwa Kenya na Somalia.