MR BEE: Mmliki wa studio ya kunoa vipaji vya chipukizi
Na JOHN KIMWERE
PENYE nia pana njia. Msemo huu unathibitishwa na vijana wengi tu ambao wamezamia kutekeleza shughuli mbali mbali katika harakati za kusaka riziki maishani.
Kati yao akiwa kijana mcheshi, Sebastian Kilanya Bijiwe mtunzi wa muziki wa burudani aliyegeukia shughuli za uratibu wa sherehe (MC) maarufu MCEE. Kando na hayo, chipukizi huyo anamiliki studio kwa jina Akili Mbili Production aliyoanzisha mwaka mmoja uliyopita.
Amezaliwa hapa Kenya mara nyingi amekuwa akifanya shughuli za wafawidhi nchini Tanzania katika kile anachodai kukutana na panda shuka nyingi.
“Kiukweli nimezoea pia nimeshakuwa mwenyeji katika taifa lile kwani nimeishi kule kwa muda mrefu sasa,” amesema na kuongeza kuwa duniani hamna sheria inayomzuia yoyote kuishi katika taifa lingine.
MR Bee kama anavyokwenda kwa jina la msimbo, anajivunia kutua jukwaa moja na wacheshi wa nguvu pia wenye majina makubwa.
Baadhi yao wakiwa: marehemu Mzee Majuto, Kingwendu, Churchill, Eric Omondi, Mdomo Bagy, Sleey David, Smart Joker pia msanii na rais wa WCB, Diamond Platnum kati ya wegnine.
Anasema amepania kuzamia shughuli kutwa pia kujijenga zaidi kutinga viwango vya wenzake wakiwamo Eric Omondi, Kingwendu na Churchill kati ya wengine.
Kuwa mratibu wa sherehe mwanzo inahitaji nidhamu, kipaji cha kuzungumza mbele na watu wengi kwa ufasaha pia ubunifu.
Mr Bee amewahi teuliwa mara nne kuwania tuzo ya MCEE Bora katika hafla tofauti ikiwamo Kilimanjaro Awards, Pwani Awards, Mtaani Awards na Mashujaa Awards. “Mwaka 2015 na 2016 ndio niliibuka Mcee bora kwenye tuzo za Mtaani Awards na Mashujaa Awards zilizoandaliwa jijini Nairobi,” alisema.
Katika muziki muimbaji huyu amefanya kolabo na wasanii tofauti hapa Kenya na Tanzania. Chipukizi huyu anajivunia kutoa fataki iliyofaulu kuvuma kweli kweli kama moto nyikani iitwayo ‘Jipe Shughuli,’ kisha alifanya kolabo ya kibao cha Maccarina,’ akimshirikisha mwenzake, Babu Dee Mapete mzawa wa Bongo.
“Mwaka 2013 nilishirikiana na mwimbaji mwenzangu mzawa wa Uganda, Ivy kutoa teke iliyokwenda kwa jina ‘Nipe Nafasi’ iliyotengezwa na prodyuza Shaky ndani ya lebo ya Mandugu Digital ya kule Tanzania,” anadokeza.
Mr Bee anasema alianzisha studio ili kukuza wasanii wanaoibukia.
”Nimepania kusaidia wenzangu kwa kuwatosa ada ya chini kiasi ili kuwapa nafasi kutambua talanta zao katika muziki,” asema.
Msanii huyo anasema wanarekodi muziki wa audio, video pia wanafunza wasanii chipukizi masuala ya muziki. Wanafundisha chipukizi jinsi ya kutoa nyimbo nzuri, kucheza piano na gita.
Kadhalika amesema wameanzisha wakfu wa Mr Bee ambapo wanatembelea vituo vya kurekebisha watoto tabia, familia za watoto wa kurandaranda mitaani pia watoto katika mitaa ya mabanda.
Wakfu huchukua nafasi hiyo kuwafunza watoto hao kuhusu madhara ya kutumia mihadarati.
Anasema jina Akili Mbili alifikia uamuzi huo baada ya kuwazia maisha aliyopitia mitaani na maisha ya shuleni ambapo alifunzwa mengi hali iliyomjenga kufikia alipo kwa sasa.
CHANGAMOTO
Kama kawaida mwimbaji huyu anasema hakuna sekta isiona na pandashuka. “Katika suala la nzima la uratibu wa sherehe, wateja wengine hulalama kuwa tunawatosa fedha nyingi ilhali si kibarua rahisi kwani wenyewe hawawezi kukitekeleza. Baadhi yao hupenda kuchelewesha malipo kinyume cha makumbaliano.”
”Aidha wanawake wengine hupenda kubadilisha biashara na kutaka kujenga uhusiano wa kimapenzi kusudi kuepuka kulipa huduma zetu.
Mratibu wa sherehe anahitaji kudumisha nidhamu kulingana na kanuni za kikazi,” akasema.
Chipukizi huyu alitambua kipaji chake akiwa mwanafunzi wa darasa la sita kwenye shule ya Msingi ya Kathanga.
Alikuwa kati ya wanafunzi waliopata nafasi kuwalikisha shule hiyo kwenye mashindano ya muziki lakini alianza kujituma rasmi mwaka 2009 baada ya kukamilisha elimu ya sekondari.
Anatoa mwito kwa vijana wenzake wenye vipaji mbali mbali kutovunjika moyo baada ya kukutana na mabonde na milima.
Anawahimiza kuendelea kutia bidii kukuza talanta zao na kila wanalotenda kumuweka Mungu mbele kuwaongoza. Mr Bee alizamiwa miaka 29 iliyopita katika kijiji cha Mutuati, eneo bunge la Igembe Kaskazini Kaunti ya Meru na kusomea shuleya Msingi ya Kathanga.