Afya na JamiiMakala

Mradi wa mbuzi wa maziwa unavyowafaa kina mama eneo kame

Na PAULINE ONGAJI August 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NI mchana, jua limeangaza miale yake na kwenye ziara ya Akilimali katika eneo la Umande, Kaunti ya Laikipia tunakutana na Julia Muthoni akilisha mbuzi wake wa maziwa.

Anasema zoezi la kuwakama humchukua takriban dakika 15 kila siku kabla ya kuzamia shughuli za siku.

Muthoni ni mmoja wa akina mama ambao wamekumbatia ufugaji wa mbuzi wa maziwa, ikizingatiwa kwamba sehemu kubwa ya eneo la Laikipia hushuhudia mvua kidogo kila mwaka.

Anasema huu ni mradi ambao alianzisha kutokana na mtaji wa Sh5, 000 kutoka kwa akiba yake.

Hii ni baada ya kubaini kwamba angetengeneza hela za ziada badala ya kutegemea kilimo cha mahindi na maharagwe.

Muthoni ambaye alianza na mbuzi mmoja anajivunia juhudi zake kwani hivi sasa anamiliki jumla ya mbuzi 11, spishi ya Kenyan Alpine.

“Mwanzoni nilikuwa nikikama kikombe kimoja cha maziwa mpaka nilipopokea mafunzo kutoka kwa shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ambalo limekuwa likielimisha wakulima hapa namna ya kuendesha kilimo chenye tija na namna ya kutengeneza malisho ya kisasa,” aeleza.

Muthoni ni kati ya akina mama ambao wamefaidi kutokana na Mradi wa Women Empowerment Through Climate Smart Agriculture ambao unafadhiliwa na Serikali ya Korea chini ya mwavuli wa Korean International Cooperation Agency (KOICA).

Aidha, anasema amejitosa kwenye biashara ya kuuza mbuzi katika soko jirani ambapo humpatia kati ya Sh8, 000-12, 000 kwa kutegemea kimo cha mifugo wake.

Elizabeth Obanda meneja wa Mradi huo kutoka Shirika la UN Women anasema miradi kama hii inaendeshwa katika Kaunti za Laikipia, Kitui na Pokot Magharibi.

“Lengo kuu ni kusaidia akina mama kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi,” asema.

Isitoshe, walianzisha mradi huu ili kina mama wawasaidie waume zao kulisha familia, kulipa karo na kulea watoto.

Lucy Nyokabi ambaye ni mwenyekiti wa kikundi cha Dwiga Kwinyitia kutoka eneo la Umande, Kaunti ya Laikipia akilisha mbuzi wa maziwa. PICHA|RICHARD MAOSI

Lucy Nyokabi ambaye ni mwenyekiti wa kikundi cha Dwiga Kwinyitia ambapo Julia ni mmoja wa wanachanma anasema hivi sasa kuna mwanamume mmoja na akina mama 17 katika kikundi chao.

Anasema hili ni jukwaa maalum ambapo wao hubadilishana mawazo na pia wamejifunza kwamba kilimo cha mbuzi wa maziwa kinaweza kuwapatia hela nzuri wakiyakusanya na kuyauza kwa wingi.

Anasema akina mama wengi hapa hukama mara mbili kwa siku, ambapo wanaweza kupata lita mbili ya maziwa kutoka kwa mbuzi mmoja kila siku.

Maziwa ya mbuzi huwapatia hela nzuri ya Sh60 kwa lita.

Na faida wanazozitengeneza zimewasaidia kuanzisha chama cha table banking, baadhi yao wakilenga kuwekeza kwenye miradi mingine kama vile ufugaji wa kuku.

Hata hivyo, anasema changamoto ambayo kina mama wengi wamekuwa wakikumbana nayo ni ukosefu wa malisho ya kutosha na yenye virutubisho vya hali ya juu.

Miezi kadhaa iliyopita akina mama 18 walipewa mbuzi kila mmoja, kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Laikipia.

Azma yao ni kukusanya maziwa mengi iwezekanavyo ili wayauze kwa madalali wanaochukua kwa Sh150 kwa lita.