Makala

Msanii atumia muziki kutuliza wagonjwa hospitalini

September 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

Anatumia muziki kuwatuliza wagonjwa waliolazwa hospitalini. Ni kazi ambayo Bw Willis Ochieng amekuwa akifanya kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Kwa muda huu, Fololo, kama anavyojulikana kwenye ulingo wa muziki, amekuwa mmoja wa kikundi cha wanamuziki watano ambao wamekuwa wakitumbuiza wagonjwa katika hospitali ya Mater, jijini Nairobi, kila siku kati ya saa nne asubuhi na saa nane adhuhuri.

“Kwa kawaida shughuli hii huchukua kati ya saa tatu na nne kila siku, ambapo sisi huwatumbuiza wagonjwa katika vyumba tofauti vya wagonjwa, vile vile wafanyakazi wa hospitalini,” aongeza.

Tiba hii sio tu ya wagonjwa, bali pia kwa wafanyakazi na wateja ambao wameleta wagonjwa hospitalini. “Hii inasaidia kutuliza mazingira ya hospitalini, na hivyo kuwapa wahusika kumbukumbu nzuri,” asema.

Kwa kawaida wao hucheza mchanganyiko wa muziki wa injili, pop na rhumba miongoni mwa aina zingine za muziki.

Kulingana naye kwa kawaida wao huhudumia wagonjwa 50, huku wakati mwingine idadi hiyo ikiongezeka na kufikia 70 na kujumuisha pia wale ambao bado hawajalazwa.

Na anasema kwamba kuna mara nyingi ambapo huduma hii imesaidia wagonjwa kupata nafuu. “Kwa mfano, mwaka jana nakumbuka kulikuwa na mwanajeshi mmoja kutoka nchini Sierra Leone ambaye baada ya kumuimbia kwa siku kadhaa, alianza kuonyesha ishara ya kuimarika kiafya, na baadaye akapona,” asema.

Bwana huyu alitambulishwa katika shughuli hii ya tiba kutumia muziki mwaka wa 2017 kupitia rafiki yake. “Niliona kama mbinu mwafaka ya kutumia kipaji changu kusaidia watu walio na matatizo mbalimbali ya kiafya,” asema.

Mwaka mmoja baadaye alihitimu kama mhudumu wa kutumia tiba ya muziki na kupewa hati na kikundi cha madaktari kutoka nchini Amerika, waliokuwa wakifanya mradi sawa na huu nchini humo.

Mafunzo hayo ya wiki mbili yalihusisha ujuzi maalum uliohitajika kufanya kazi na wagonjwa tofauti, kama vile watoto walio na mahitaji maalum na watu waliolazwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi.

Ni mradi ambao ni wa kujitolea kumaanisha kwamba hauna malipo, ila tu kwa marupurupu kidogo. Lakini licha ya haya, anasema kwamba inaridhisha kwamba anatumia kipaji chake kuwasaidia wagonjwa.