MSANII WA WIKI: Arejea nyumbani kuvisuka vipaji
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
SI siri kwamba Kenya kuna vipaji kali katika ulingo wa burudani iwe ni wanamuziki au maprodusa na Awadh Salim maarufu Shirko ni miongoni mwao.
Shirko amewahi kuwa kiongozi na mtayarishaji wa muziki wa kituo cha Mkubwa na Wanawe Youth Organisation (MNW) cha jijini Dar es Salaam nchini Tanzania ambacho kilikuwa kinakuza vipaji vya sanaa za muziki, uigizaji na unenguaji (densi) kwa wasanii chipukizi.
Aidha alikuwa produsa na mkono wake umewaelekeza baadhi wasanii ambao sasa ni maarufu nchini humo.
Hebu tujulishe ni wasanii gani wa Bongo ulioachangia kuinua vipaji vyao?
Shirko: Nilikuwa mwasisi wa kundi la Yamoto Band ambalo lilikuwa na waimbaji chipukizi kina Aslay, Mbosso, Enock Bela na Beka Fleva. Pia kuna msanii mwingine wa kizazi kipya, Kayumba Juma ambaye naye anatoka kituo cha MNW aliyewahi kushinda Epic Bongo Star Search (EBSS) mwaka 2015.
Je, kuna wale ulioandaa kazi zao na zikaishia kuvuma?
Shirko: Nina furaha kuwa mnamo mwaka 2008 nilimtayarishia albamu Berry Black kutoka kwenye kundi la 2Berry na kuimba naye wimbo wa Najua ambao ulipata umaarufu na albamu hiyo kuuza zaidi Afrika Mashariki wakati huo.
Nini hasa kilichokufanya uondoke hapa nyumbani na kuelekea Bongo?
Shirko: Niliondoka hapa kuelekea Tanzania kutafuta nafasi ya kuinua kipaji changu cha uimbaji pamoja na uprodusa. Nilikosa fursa hiyo hapa nyumbani lakini Watanzania walinikumbatia.
Imekuaje hivi sasa umeamua kurudi nyumbani?
Shirko: Kutokana na jina langu kuwa kubwa Tanzania, baadhi ya washika dau wa muziki hapa Mombasa, walinifuata na kuniomba nirudi nyumbani kuwainua wanamuziki chipukizi.
Ni miezi saba sasa tangu urudi nyumbani, unasemaje kuhusu muziki na wanamuziki wa hapa nchini?
Shirko: Nimeona kuwa muziki wetu unaendelea kupiga hatua na nina hakika kama tutashirikiana, haitachukua muda mrefu kwa chipukizi wetu wengi kuwa na majina makubwa katika fani hii kama walivyo wenzetu kule Bongo.
Hebu tufahamishe wewe mwenyewe hivi sasa bali na uprodusa, unaimba?
Shirko: Naam! Naimba Kasida za dini yetu ya Kiislamu ili kuwapa motisha waimbaji wengine Waislamu wajitose kwenye tasnia hii. Nawaomba wenye uwezo wasaidiane nami kuhakikisha tunakuwa na waimbaji wengi wa Qasida na kuchangia gharama za kukuza tasnia hiyo.
Tangu urudi, una mpango wowote wa kuwainua waimbaji chipukizi?
Shirko: Nimeanza na kijana Ali Mahaba na tayari kibao chake cha Sina Ujanja kinafanya vizuri. Ninaamini kijana huyu atawika na kufikia kiwango cha juu zaidi kama walivyo wasanii wengine.
Unawaambia nini mashabiki wako?
Shirko: Nawaomba wapenzi na wadau wa muziki tushirikiane katika kuwaunga mkono waimbaji wetu ili tukuze vya kwetu kwani yataka tufahamu kuwa cha mwenzio si chako. Pia ninaomba vyombo vya habari viwe vikikuza nyimbo za wasanii wetu.