• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 9:50 AM
MSANII WA WIKI: ‘Nilijisuta sana baada ya rafiki yangu kuaga dunia’

MSANII WA WIKI: ‘Nilijisuta sana baada ya rafiki yangu kuaga dunia’

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

TAJRIBA ya msanii na mazingira anamoishi huathiri pakubwa anavyousawiri ulimwengu na uamuzi na hatua anazochukua maishani.

Catherine Mbithe ‘Princess Cathy’ anasema mkondo wa maisha yake ulibadilika ghafla baada ya kifo cha rafiki yake wa chanda na pete.

“Nilipata mshtuko mkubwa rafiki yangu wa chanda na pete alipopata ajali na kufariki. Nilihisi kana kwamba maisha yananitesa na ndipo niliamua kumpa Mola moyo wangu. Na katika kuokoka kwangu, niliona ni muhimu kujitosa katika fani ya muziki ili kuhimiza waja kurejea njia ya sawa na Muumba wetu wasije wakajipata kati hali iliyonikuta,” asema Princess Cathy.

Msanii huyu anasema kuwa alisikia wito wa kwenda kulitangaza neno la Mungu na ndipo alipoanza kutunga na kurekodi nyimbo zilizojumuisha albamu yake ya kwanza Hapo Nimefika alioachia 2014.

Umesema kifo cha rafikiyo kilishtua sana kiasi cha wewe kuokoka na kuanza kuimba nyimbo za sifa. Mbona hasa nyimbo za Injili ilhali ungewasilishha maudhui yako katika za kilimwengu pia?

Princess Cathy: Kabla kuokoka, niliishi maisha ya raha na anasa tupu ila alipoaga rafiki yangu nilijipata nikiwazia mkondo wa maisha yangu na sikuridhika. Niligundua kuwa maisha ni mafupi sana na nisipojirekebisha, basi huenda yakakatizwa ghafla kama ya mwandani wangu huyo. Hivyo nilipokata kauli kuokoka, niliamua kumtukuza Bwana sababu ndiye muamuzi wa maisha yangu.

Katika siku za hivi karibuni, wasanii wa Injili wanazidi kuongezeka Pwani na huenda ule msemo ‘Mombasa Raha’ ukakosa mashiko kabisa. Mbona?

Princess Cathy: Yaonyesha muda umefika kwa binadamu kurudi kwa njia za haki na sio kwetu sisi Wakristo pekee bali hata wa dini zingine. Kwa mfano, waimbaji wa kasida zenye mawaidha ya kuwataka watu wote wafuate njia njema wameongezeka pia.

Mbali na albamu yako ya kwanza, una nyingine na unaandaa chochote kipya?

Princess Cathy: Niiko katika harakati za kutoa albamu yangu a pili Utanu itakayokuwa na ngoma Utanu na Nimusinde ambazo zinatamba kwa sasa kwenye audio.

Waimbaji gani wa hapa nchini na ng’ambo wanaokukosha?

Princess Cathy: Waimbaji wanaonipunga kwa nyimbo zao za Injili hapa nchini ni Ali Mkhwana, Mercy Masika na Evelyne Wanjiru hali kimataifa napendelea nyimbo za Don Moen.

Umepata vikwazo vyovyote kutoka kwa familia yako sababu ya kujitosa katika fani hii ya muziki?

Princess Cathy: Mwanzo ni mashabiki wangu nambari moja na wamekuwa wakinipa sapoti kuhakikisha nafanikiwa katika lengo langu la kuwa msanii mwenye kutajika sio hapa nchini pekee bali kote barani Afrika na kwingineko duniani.

Mipango yako ya usoni?

Princess Cathy: Napania kuwa msanii mtajika sio hapa nchini tu bali kimataifa.

Unawaambia nini wapenzi wa muziki wako?

Princess Cathy: Ninawaambia mashabiki wa nyimbo zangu kuwa nawapenda sana na wazidi kuniombea. Pia nawashukuru watumishi wa Mungu ambao wamekuwa wa karibu nami wakati wote. Nawaambia wapenzi wa muziki wangu kuwa kabla ya kumalizika mwaka huu, watarajie vibao visivyopungua saba ambavyo nina hakika vitawapendeza.

You can share this post!

Droo ya mechi za kufuzu Afcon 2021 kufanyika Julai 18

KRA yanasa Range Rover iliyofichwa kwenye kontena...

adminleo