Mshukiwa wa utapeli alivyohamisha Sh322 milioni kutoka Benki ya Equity hadi Abu Dhabi
MNAMO Aprili 2023 wapelelezi wanasema mtu fulani aliingilia mfumo wa malipo ya Benki ya Equity na ule wa kuzuia ulaghai wa kimtandaoni.
Wanadai alibadilisha kinga za kiusalama za wafanyabiashara ambao walikuwa wamejisajili kupewa kadi za malipo za benki ya Equity.
Katika mfumo wa kubaini uhalifu wa kimtandao, kinga za usalama za wafanyabiashara hao zinashukiwa kubadilishwa ili kuruhusu pesa kutolewa kwa urahisi.
Kwa kipindi cha miezi mitatu, kadi bandia za kufanyia malipo (credit cards) zilidaiwa kutumiwa kufanya malipo kwa wafanyabiashara hao watatu.
Wapelelezi wanasema hamna bidhaa au huduma zilitolewa licha ya kwamba mamilioni ya fedha ziliwaendea wafanyabiashara hao watatu, kutoka kisanduku ambako Benki ya Equity huweka fedha za kugharamia malipo yanayofanywa kupitia kadi za malipo (credit card).
Hii ina maana kuwa pesa ziliibwa polepole kutoka benki hiyo.
Kufikia wakati Benki ya Equity iligundua hilo na kupiga ripoti kwa polisi, ilikuwa imepoteza jumla ya Sh322.1 milioni.
Mawasiliano kati ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) yaliyoonwa na Taifa Leo Dijitali yamefichua jinsi pesa hizo zilihamishwa kupitia akaunti mbalimbali za benki huku kiasi fulani cha pesa hizo kikifikishwa nchini Milki ya Muungano wa Kiarabu (UAE).
Wapelelezi wamependekeza kuwa washukiwa wanne wafunguliwe mashtaka. Majina ya washukiwa hao yamebanwa kutoka na sababu za kisheria.
“Kwa hivyo, malalamishi ni kwamba kati ya Aprili 2023 na Julai 2023 wafanyabiashara watatu (majina yao yamebanwa) kila mmoja alilaghai Benki ya Equity kwa kubadilisha kinga dhidi ya wizi wa mtandao (CyberSource) kutoka 3D hadi 2D. Hii iliwaruhusu wafanyabiashara hao kutumia kadi bandia za malipo kupata Sh322, 154, 851 moja kwa moja kutoka akaunti ya benki hiyo ya kugharamia malipo kupitia kadi,” inasema barua ya ODPP.
Baadaye wafanyabiashara hao wanadaiwa kuhamisha pesa walizopokea kupitia ulaghai huo, wa kutumia kadi za malipo, hadi akaunti moja katika Middle East Bank inayoendeshwa na kampuni moja.
Jamaa mmoja, mshirika wa wafanyabiashara hao, mwenye uraia wa Kenya na Uingereza alihamisha pesa hadi kampuni moja ya kibinafsi jijini Abu Dhabi, nchini UAE.
Mnamo Aprili mwaka huu, DCI ilipendekeza kwa ODPP kwamba wafanyabiashara hao watatu na mshirika wao mwenye uraia wa Kenya na Uingereza wafunguliwe mashtaka matatu ya; wizi, utakasaji wa pesa na ulaghai kupitia mitandao.
Imetafsiriwa na Charles Wasonga