Msichana 13, aongoza kampeni ya kupanda miti nchini
AKIWA na umri wa miaka 13 pekee, Karen Wanjiru tayari amepanda zaidi ya miti 20,000 katika misitu mbalimbali nchini Kenya iliyoharibiwa na shughuli za binadamu.
Mwezi huu wa Novemba, mwanafunzi huyo wa shule ya msingi jijini Nairobi ataingia katika awamu mpya ya mradi wake wa mazingira kupanda maelfu zaidi ya miti katika ekari 50 za Msitu wa Kirinyaga.
Hatua hiyo, inayoungwa mkono na Huduma ya Misitu Kenya (KFS), inaashiria kutambuliwa rasmi kwa juhudi za vijana katika vita vya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Karen, ambaye ni mwanafunzi wa Gredi 8 katika Shule za Rophine Group, amekuwa msukumo kwa watoto na watu wazima nchini kote. Kufikia Novemba 22, ataweka historia mpya katika safari yake ya kulinda mazingira.
Kwa miongo kadhaa, Kenya imepoteza sehemu kubwa ya misitu yake kutokana na ukataji miti kiholela, ukataji haramu na matumizi duni ya ardhi. Juhudi kama za Karen zimekuwa muhimu katika kurejesha misitu kulinda mito na kuzuia mmomonyoko wa udongo, hasa katika maeneo ya milimani yanayokumbwa na maporomoko ya ardhi.
Karen anasema mafanikio yake yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na wazazi wake, hususan mama yake, Bi Ann Kimani, ambaye amekuwa nguzo kubwa kumpa moyo tangu akiwa mdogo.
“Nawashukuru sana wazazi wangu, hasa mama yangu, kwa kuniamini na kuniunga mkono katika kila hatua. Kutoka kupanga hafla hadi kunitia moyo nyakati ngumu, wamekuwa mabingwa wangu wa kweli,” alisema Karen.
Kwa upande wake, mama yake alisema:
“Kuona binti yangu akijitolea kulinda misitu yetu na kuhamasisha wengi ni fahari kubwa. Kumsaidia ni heshima, na ninatumai wazazi wengine pia watakuza vipaji vya watoto wao bila kujali ukubwa wa ndoto zao.”
Karen alijulikana kwa mara ya kwanza kupitia jarida la Young Nation, la Sunday Nation, alipokuwa amepanda miti 16,000 katika Msitu wa Kinale. Kwenye Siku ya Mazingira mwaka huu, alirejea huko na marafiki wakapanda miti 4,000 zaidi, na kufikisha jumla ya miti 20,000.
Kadri mradi wake ulivyopanuka, Huduma ya Misitu Kenya (KFS) ilimkabidhi ekari 50 katika Msitu wa Kirinyaga, ishara ya imani na matumaini katika uongozi wa kijana huyo mdogo.
“Kupata ekari hizi 50 ni habari njema,” alisema Karen.
“Zitanipa nafasi ya kupanda maelfu zaidi ya miti na kuonyesha kuwa hata mtoto mmoja anaweza kuleta mabadiliko makubwa. Nia yangu ni kugeuza kila kipande cha ardhi kuwa kijani.”
Mwanafunzi mwenzake, Aisha Mwangi, ambaye pia ni mwanachama wa Klabu ya Mazingira ya Utawala, alisema:
“Kupanda miti na Karen kumetufundisha kuwa vitendo vidogo vinaweza kuleta mabadiliko makubwa. Ekari hizi ni fursa ya kipekee ya kuhamasisha wengi zaidi.”
Karen alizungumza na Taifa Leo kutoka California, Amerika, ambako anawakilisha Kenya katika mashindano ya Little Miss World. Akiwa Little Miss Kenya, anatumia jukwaa hilo kuelimisha dunia kuhusu suluhu za tabianchi zinazoongozwa na vijana.
“Miti ikikatwa, mito na mashamba navyo hupotea. Maporomoko ya ardhi huharibu nyumba, familia hupoteza riziki. Lakini kama kila Mkenya angepanda mti mmoja tu kwa mwaka, tungepona haraka,” alisema Karen.
Nation Media Group, ambayo ni washirika wa miradi yake, itaunga mkono shughuli yake kuu ya kupanda miti Kirinyaga, kusaidia kufikisha ujumbe wake kwa hadhira ya kitaifa.