Msomi akejeli Trump kwa kuunda sanamu yake chooni
HUKU ulimwengu ukivuta pumzi kuelekea kuapishwa kwa Donald Trump kesho, Januari 20, msomi mmoja Mkenya, David Maillu, amejenga choo chenye sanamu ya kuvutia ya Rais Mteule wa Amerika.
Msomi huyo anasema sanamu hiyo ya chuma na simiti ni kielelezo cha malalamishi ambayo anatumai yataibua mjadala kuhusu ubaguzi wa rangi na utu wa Mwafrika.
Sanamu hiyo ya ajabu iliyopewa jina la ‘Rais Donald Trump S***hole’, imechochewa na tamko la kudhalilisha – linalochukuliwa na wengine kama ubaguzi wa rangi – ambalo Rais Trump alitoa mnamo 2018 dhidi ya nchi za Kiafrika.
‘Tumetumia kejeli dhidi ya (rais mteule) Donald Trump baada ya kuwatusi Waafrika kwa kuwaita watu kutoka nchi za shimo la kinyesi . Sanamu hiyo ni sehemu ya ubunifu wetu ambao unakusudiwa kuzua gumzo kuhusu ubaguzi wa rangi,” Bw Maillu aliambia Taifa Jumapili alipokuwa akiwasimamia wafanyikazi wawili waliokuwa wakikamilisha sanamu hiyo akiwa ameketi kwenye kona ya nyumba yake ya mashambani katika Kaunti ya Makueni.
Kazi ya kuunda sanamu ya Trump ‘inayonuka’ ilianza mnamo 2018 kwa kuchimba shimo refu. Ujenzi ulikwama wakati Bw Trump aliposhindwa uchaguzi wa 2020 na Rais Joe Biden. Bw Maillu alianzisha tena mradi huo wakati mgombea huyo wa Republican Trump aliponyakua kiti hicho baada ya kumshinda Kamala Harris kwenye uchaguzi wa Novemba mwaka jana.
Kundi la nyasi kavu hutengeneza nywele huku mchanganyiko maridadi wa rangi nyekundu na simenti nyeupe ukitumiwa kuonyesha rangi ya ngozi ya Bw Trump.
‘Tumeweka sanamu kubwa kwa sababu Rais Trump ni mtu mashuhuri,’ Bw Maillu alisema.
Uzinduzi wa sanamu hiyo umepangwa Jumatatu, Januari 20, siku ambayo Rais Trump anatazamiwa kuapishwa kwa wadhifa huo. Huku ulimwengu ukitazama baada ya Bw Trump kuapa kuwatimua maelfu ya wahamiaji kutoka Amerika wakati wa kampeni zake, Bw Maillu anatumai kuwa sanamu hiyo angalau itazingatia maoni ya Bw Trump yaliyotolewa hapo awali kuhusu Afrika na, tunatumai, itasaidia kubadili mitazamo kama hiyo.
Muhimu zaidi, anatumai kuwa sanamu hiyo itazua gumzo kuhusu ubaguzi wa rangi na kurejesha utambulisho wa Mwafrika ambao anaamini umetoweka kwa miaka mingi, hasa wakati wa ukoloni.
“Kama rais wa nchi yenye nguvu zaidi duniani, Rais Trump anapaswa kujiepusha na ubaguzi wa rangi. Anapaswa kujua kwamba sisi sote ni binadamu. Ikiwa kuna chochote imefanya, jamii ya Weusi ina jukumu kubwa katika uchumi wa Amerika,’ Bw Maillu alisema.
Maillu ambaye alijifundisha usanii, kwa miaka mingi amekuwa mchongaji stadi, mchoraji, mwandishi wa riwaya, mshairi na mwanamuziki. Akiw na umri wa miaka 85 anatumia kazi zake za sanaa kukosoa walio mamlakani.
Sanamu hiyo ya ukumbusho wa Trump ndio nguzo ya hivi punde zaidi katika vita vyake dhidi ya ukoloni mamboleo, mada ambayo imetawala kazi zake za sanaa. Kulingana na riwaya yake ya hivi punde zaidi, Push Gen Z Push Harder: Storm of Political Revolution, kwa mfano, anahoji kuwa ubepari na ukoloni mamboleo ni vichocheo muhimu vya mawimbi ya machafuko ambayo yamefafanua hali ya kisiasa ya Kenya kwa miaka mingi.
Bw Maillu anahisi kungekuwa na jibu kali zaidi kwa tusi la Bw Trump mwaka wa 2018 dhidi ya Afrika na wahamiaji wengine.
“Kama Waafrika, bado tunauguza makovu ya ukoloni. Tumewekewa masharti kwamba ni makosa kuwakosoa walio madarakani. Miaka mingi ya ukoloni imetufanya tupoteze nguvu zetu mbele ya mataifa yenye nguvu. Ilitunyima hisia zetu za utambulisho. Tumeharibiwa kisaikolojia. Watu wengi wamefanywa kujihisi duni na ubunifu wetu umeharibiwa. Ndio maana kama msanii nimekuwa nikijaribu kushughulikia shida hii. Nimejipanga kuelimisha jamii kurejesha utambulisho wetu uliopotea,” alisema.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA