MUTANU: Wakenya wasikubali uchochezi dhidi ya raia wa kigeni
Na BERNARDINE MUTANU
Matamshi ya Mbunge wa Starehe Charles Njagua dhidi ya raia wa kigeni, hasa kutoka mataifa jirani sio tu ya kuhofisha, yana uwezo wa kuhujumu uhusiano wa kidiplomasia kati ya Kenya na mataifa mengine.
Ingawa kwa mwanasiasa huyo chipukizi ilikuwa ni siasa kama kawaida, ni matamshi kama hayo ambayo huchochea watu dhidi ya wengine na kuzua mauaji ya kiholela.
Kenya ina uhusiano mzuri na Tanzania na Uganda, mataifa mawili chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kibiashara na kijamii.
Matamshi kama hayo yanaweza kuzua uhusiano baridi kati ya mataifa hayo, ingawa raia wake wamekuwa wakiishi kama ndugu.
Visa vya ubaguzi wa raia wa kigeni sio vipya Afrika. Nchini Afrika Kusini, visa vya mara kwa mara vya aina hiyo vimesababisha maafa makubwa.
Raia wa Afrika Kusini hudai nafasi zao za kazi zimetwaliwa na raia wa kigeni huku wao wakitaabika. Kutokana na hilo, baadhi ya Wakenya na raia wengine wa kigeni nchini humo wamepoteza maisha na mali yao.
Hali hiyo ndiyo Njagua analenga kupalilia nchini. Kwa hakika, tuna raia wengi wa kigeni Kenya wanaofanya kazi au hata biashara. Lakini vile vile maelfu ya Wakenya wamo katika mataifa mengine wakiendesha biashara na kuchapa kazi.
Ingawa kumekuwa na uhasama wa hapa na pale kati ya Tanzania na Kenya, ukweli ni kwamba matamshi hayo hayakufaa.
Mbunge hawezi kuwachochea Wakenya dhidi ya raia wa kigeni kwa kuwa huo ni wito kwa Wakenya walioko nje ya nchi kutimuliwa wanakoishi. Wafanyibiashara na Wakenya kwa jumla hawapaswi kukubali kuchochewa kwani watakapokuwa wakipigana na kudhulumiana na raia wa kigeni, wachochezi wao hawatakuwa karibu.
Wakati Gikomba, Nyamakima na maeneo mengine ya kibiashara yatakuwa motoni, wachochezi hao watakuwa majumbani mwao katika mitaa mikubwa, au pengine watakuwa wametoroka nchini.
Uhusiano mzuri kati ya Kenya na mataifa mengine ni muhimu kwa uchumi na maendeleo kwa jumla. Hivyo basi, matamshi ya Njagua ni ishara kwamba huenda haelewi uhusiano huo.
Ukweli ni kwamba, Kenya huagiza na kuuza bidhaa katika mataifa jirani ya Mashariki mwa Afrika na kwingineko. Hivyo, kutatizika kwa uhusiano huo kunaweza kuleta hasara kubwa zaidi ya anayodai Njagua.
Kenya ni taifa linaloaminika na kutambulika ulimwenguni kwa sera yake wazi ya kukaribisha watu wote kutoka kote ulimwenguni. Litakuwa jambo la kuhusunisha kwa matamshi machafu ya mwanasiasa limbukeni kushusha hadhi hiyo ya nchi yetu kimataifa.