• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
MUTUA: Kalonzo atumie tajriba kuwapatanisha Riek Machar na Salva Kiir

MUTUA: Kalonzo atumie tajriba kuwapatanisha Riek Machar na Salva Kiir

Na DOUGLAS MUTUA

MMOJA wa watu mashuhuri waliofanikisha kupatikana kwa uhuru wa Sudan Kusini kutoka Sudan ni aliyekuwa makamu wa rais wa Kenya, Bw Kalonzo Musyoka.

Wakazi wa eneo la kusini mwa Sudan walipopiga kura ya maamuzi kujitenga na taifa la Sudan, Bw Musyoka alieleza furaha na fahari yake kwamba, juhudi zake zilifanikiwa.

Nakumbuka vyema alipohojiwa wakati huo akieleza jinsi mara nyingine, ujumbe wake wa wapatanishi ulivyolazimika kutumia vitisho dhidi ya wadau ili wakubaliane.

Wadau wakati huo walikuwa ni Rais Omar ‘al-Bashir wa Sudan, aliyepinduliwa na majeshi mapema mwaka huu, na kiongozi wa waasi, Dkt John Garang, aliyefariki 2005.

Wawili hao walitishiwa kwamba, serikali ya Sudan ingepinduliwa au wangekamatwa kuwashtaki kwenye mahakama za kimataifa kwa kusababisha umwagikaji damu.

Bw Musyoka alieleza jinsi vitisho hivyo vilivyowaogofya mahasimu hao mpaka wakaridhia kutia saini mkataba wa amani ulioishia kwenye uhuru wa Sudan Kusini.

Sasa, kwa sababu Bw Musyoka ameteuliwa mjumbe maalumu wa Kenya nchini Sudan Kusini, tunatarajia kuona tajiriba yake ya mashauriano ikiwanufaisha raia wa nchi hiyo.

Ingawa kwa mtizamo wa Mkenya wa kawaida uteuzi huo ni njia ya Rais Uhuru Kenyatta kumzawadia Bw Musyoka kwa kuacha kumponda kisiasa, unafaa.

Mtizamo huo uwe wa kweli au la – mradi raia wa Sudan Kusini wapate amani na kufaidi uhuru waliopigania kwa miaka mingi – kwangu haidhuru. Uteuzi wenyewe una umuhimu mkubwa kuzidi siasa za ndani kwa ndani ambazo Wakenya wamezoea kushiriki kila mara.

Utakuwa usaliti mkubwa kwa Kenya na Sudan Kusini ikiwa Bw Musyoka atalaza damu au kutumia muda wake mwingi kufanya siasa badala ya kazi aliyoteuliwa kufanya.

Amani ya Sudan Kusini ni suala la dharura ambalo kamwe halipaswi kufanyiwa mzaha na yeyote aliye na akili timamu.

Nimesema uzembe na mzaha ukiingia, utakuwa usaliti kwa Wakenya kwani pesa zao zinazotumika kumlipa Bw Musyoka na wasaidizi wake.

Vilevile, anga ikinuka baruti nchini Sudan Kusini, utakaokipata ni uchumi na usalama wetu; wakimbizi watamiminika Kenya na kuongeza masaibu juu ya tuliyonayo.

Unapoisoma makala hii, wapo raia wa Sudan Kusini wanaovuka mpaka kuingia Kenya ili kukimbia dhiki nchini kwao.

Bw Musyoka asipojitolea kikamilifu, utovu wa amani na usalama utatamalaki. Tafakari ukiishi ndani ya nchi ambapo kufa au kuishi dakika moja ijayo hakutabiriki.

Maradhi ya kuaibisha kama kipindupindu na vifo vya njaa kwenye nchi iliyo na utajiri wa mafuta kama Sudan Kusini ni udhalilishaji mkubwa wa binadamu.

Hakuna mtu anayepaswa kuishi kwa dhiki kiasi hicho huku nchi nyingine duniani zikiendelea kufurahia amani na ustawi.

Afrika inapaswa kuungana kuhakikisha Sudan Kusini imeuguza majeraha ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na kupona kikamilifu. Bw Musyoka anapaswa kutumia uzoefu wake vilivyo kama mjumbe wa Afrika nzima kushinikiza kubuniwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa kulikoahirishwa Mei.

Kumekuwa na minong’ono kwamba, hakuna juhudi zozote zinazofanywa ili kuwapatanisha Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake, Dkt Riek Machar.

Hao ndio wadau wakuu wa sasa wanaopaswa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ifikapo Novemba mwaka huu. Dkt Machar anaishi uhamishoni nchini Sudan katika mpango unaoaminika kuwa kifungo cha nyumbani ili asivuruge mambo.

[email protected] 

You can share this post!

ODONGO: Maafisa wa FKF, klabu wakome kutumia vijana vibaya

GWIJI WA WIKI: Elizabeth Wangari

adminleo