MUTUA: Uozo wa ajabu kugeuza corona kitega uchumi
Na DOUGLAS MUTUA
Lisemwalo lipo na ikiwa halipo limo njiani. Nimeandika hapa mara kadhaa kwamba, japo sikubaliani na watu wanaotilia shaka athari za ugonjwa wa corona nchini Kenya, wasipuuzwe.
Nasema wasipuuzwe kwa kuwa nchi haiwezi kutunukiwa wingi wa wendawazimu kiasi hicho, hawashuku mambo kimazoea tu, haikosi wanajua jambo moja au jingine.
Ni vigumu kumsadikisha mtu kutafakari kuhusu uvumi wowote unaoenea mtaani, hasa wakati wa ugonjwa wa kushtukiza kama corona, lakini sasa itabidi tutafakari tena.
Imeibuka kwamba, huenda kuna ukweli fulani katika uvumi kwamba Serikali ya Kenya inafanya biashara na janga la corona.Itakuwa vigumu kuwasadikisha watu kwamba ugonjwa huo umeenea nchini kwa kiasi kikubwa kwa sababu sasa ule wasiwasi kuwa hii ni biashara tu umethibitishwa kwa kiwango fulani.
Kutokana na ulafi wa mafisadi wanaojua vichochoro vya kupita na kuvuna vinono serikalini, sasa ule uvumi kwamba Kenya inatia chumvi habari za corona ili kukamua pesa za wafadhili utakita mizizi.
Habari fichuzi zilizochapishwa hivi majuzi kwamba, huku Wakenya wakihofia kuangamizwa na ugonjwa huo, wapo watu waliovuna fedha kutokana na hali hiyo ni za kuvunja moyo.
Mara tu ilipobainika kuwa janga la corona lingetua Kenya wakati wowote, na kwamba kiasi kikubwa cha fedha kinatengwa ili kukabiliana nao, wajanja walianzisha kampuni ghafla kujiandalia msimu wa mavuno ya fedha.
Walizimezea mate jumla ya Sh223 bilioni zilizoingia kwenye hazina ya serikali kutoka pembe zote za dunia katika muda wa miezi miwili kwa ajili ya makabiliano hayo.Baadhi yao walikodi ndege binafsi hadi Uchina kununua vifaa ambavyo vingehitajika katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo na kusubiri kuuzia serikali kwa masharti yao.
Katika maandalizi hayo ya wajanja, kanuni za ununuzi ambazo kisheria ni sharti zizingatiwe zilikiukwa kama mchezo, watu wakawa mabilionea ghafla. Shirika linalosimamia ununuzi wa bidhaa za afya (Kemsa) lilipuuza kanuni hizo na kuwapa watu wasiostahili kandarasi zilizowazolea mamilioni.
Hiyo ni hali ya kutamausha sana ikikumbukwa kwamba, Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) mnamo Aprili aliipa Serikali hundi ya Sh2 bilioni, pesa alizotwaa kutoka kwa mafisadi, ili kupambana na corona.
Kwamba, wapo wakora walioona hali ya sasa kama njia ya kujitajirisha wakati ambapo baadhi yetu tunaomba upepo wa maradhi upite mbali nasi ni jambo linaloibua maswali mengi.
Swali kuu; ni kitu gani kinachomsababisha binadamu kukoleza uovu kiasi hicho hivi kwamba hajali maisha ya binadamu wenzake?
Hivi watu wanaofaidika na uwepo wa corona nchini Kenya wangetaka ugonjwa huo uishe kabisa ilhali umekuwa kitega-uchumi chao?Nimewahi kuuliza swali hili kuwahusu watu waliotajirika kutokana na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.
Ni wangapi wanaoweza kuwa radhi kuyapoteza magari yao makubwa na marupurupu manono, wajipate bila kazi, kwa sababu dawa imepatikana?
Wapo waovu wanaoishi miongoni mwetu ambao wanatazama matatizo yetu kama fursa ya kujitajirisha. Wako radhi kujiundia pesa tu hata kama tutakufa kwa halaiki. Huo ni uovu, si ujuzi wa kufanya biashara.
Linalokata maini kuhusu kashfa hiyo ni kwamba, wadau wakuu ni watu wenye ushawishi serikalini na hasa chama cha Jubilee, hivyo hawataadhibiwa.
Kumbuka, utawala wa Jubilee umebakisha miaka miwili tu uondoke mamlakani; wakuu hawataacha kufunganya virago eti waanze kuwafuatafuata washirika wao kwenye mambo haya.
Hali ni mbaya zaidi kuliko inavyoonekana kwa kuwa ufisadi huo unafanyika hata kwenye serikali za kaunti, hivyo hatukugatua fedha na mamlaka pekee bali pia uozo.