Makala

Mwaka mmoja wa baraka na laana ya SHA

Na ANGELA OKETCH August 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 4

Mwaka mmoja baada ya kuzinduliwa kwa Mamlaka ya Bima ya Afya ya Jamii (SHA), mageuzi makubwa ya huduma ya afya yaliyopangwa na serikali yako kwenye njia panda kati ya kufanikiwa kwa kishindo au aibu ya kufeli.

Katika mojawapo ya hospitali kuu za rufaa nchini, simulizi mbili tofauti zinaendelea kwa wakati mmoja – zikionyesha uhalisia wa changamano za mfumo ambao kwa baadhi umeleta faraja ya maisha, huku wengine wakiachwa kwenye hali mbaya zaidi.

Bi Margaret Wanjiku anamshika mwanawe mchanga kwa upole, machozi ya furaha yakitiririka usoni mwake. Kupitia SHA, alifanyiwa upasuaji wa dharura wa kumpata mtoto, ambao awali angelipa Sh300,000 – lakini sasa gharama hiyo ililipwa kikamilifu.

“Niliamini nitampoteza mtoto wangu na kuingia kwenye madeni. SHA ilituokoa. Nilikuwa nimesikia kuwa mfumo huo unafaa walioko serikalini pekee, lakini haikuwa hivyo,” anasema.

Vivyo hivyo, Bw Brian Kipchoge anaendelea na tiba ya saratani ya damu (leukemia). Akiwa chini NHIF, familia yake ilikuwa imefikia kikomo cha matibabu. Lakini kupitia SHA, gharama yote inagharamiwa.

Bw Samson Waweru, aliyehusika kwenye ajali wiki iliyopita, pia anasema bili yake ya hospitali pamoja na miguu bandia aliyopewa, zililipwa na SHA.

Hata hivyo, si mbali na hapo, Bw James Mutua anashika karatasi ya dawa ambazo hawezi kununua. Fundi huyo wa magari kutoka Kibera, hajapata huduma yoyote kutoka kwa SHA tangu mabadiliko yalipoanza – baada ya kushindwa kukamilisha mchakato wa tathmini ya uwezo wa kuchangia. Mfumo huo hauwezi kugharamia matibabu yake. “NHIF ilikuwa rahisi. Sasa narudi tena kulipa kila kitu kwa pesa taslimu,” anasema kwa uchungu.

SHA ilipozinduliwa kuchukua nafasi ya NHIF, serikali iliahidi huduma ya afya kwa wote itakayolinda Wakenya dhidi ya gharama za juu za matibabu. Lakini takriban miezi 18 baadaye, takwimu zinaonyesha mfumo unaoendelea kuporomoka.

Kati ya Wakenya milioni 25 waliosajiliwa kwenye mfumo huo, ni milioni 4.5 pekee waliofanikiwa kukamilisha mchakato wa tathmini ya mchango – na si wote wanaolipa kwa wakati. Cha kushtua zaidi, ni chini ya milioni moja wanaolipa viwango walivyowekewa – hali inayotia wasiwasi kwa mfumo wa bima ya afya.

Katika mwezi wa Julai pekee, SHA ilikusanya Sh6.7 bilioni, ambapo Sh5.9 bilioni zilitoka kwa wafanyakazi wa sekta rasmi 70,793 waliokatwa asilimia 2.75 ya mishahara yao. Kwa upande mwingine, wanachama 187,727 wa sekta isiyo rasmi kati ya milioni 16.7 waliostahili, walichangia Sh780 milioni pekee – hali inayoonyesha mapungufu makubwa ya mfumo huo.

SHA imepoteza karibu nusu ya wanachama kutoka sekta isiyo rasmi waliokuwa wakilipa NHIF – kutoka 1.8 milioni mwaka 2022 hadi chini ya 900,000. “NHIF ilihitaji Sh500 kwa mwezi. SHA inataka Sh6,000 kwa makadirio ambayo sielewi. Nitatoa wapi pesa hizo wakati sina kazi ya kila siku?” anauliza Bw Peter Otieno, mfanyakazi wa ujenzi kutoka Kisumu.

Lakini Katibu wa Huduma za Afya, Dkt Ouma Oluga, anapinga kulinganishwa kwa SHA na NHIF. “Kulinganisha SHA na NHIF ni hadithi ya mafanikio. Tunahitaji uhamasishaji zaidi,” anasema. Mfumo wa tathmini ya uwezo wa kulipa uliokusudiwa kusaidia kuchangia kulingana na kipato, umekuwa kikwazo kikubwa.

Wataalam wanasema SHA haifanyi kazi kwa kutumia fomula rasmi iliyowekwa na serikali. “Katika nchi yenye ukosefu mkubwa wa ajira na watu wanaoingia na kutoka kwenye umaskini kila mara, mfumo huu haukufaa,” alisema Dkt Brian Lishenga, Mwenyekiti wa Muungano wa Hospitali za Kibinafsi.

Anasema serikali imesitisha kimya kimya matumizi ya fomula hiyo kutokana na ugumu wake, hivyo kuchangia chuki miongoni mwa wananchi wanaohisi hawakutendewa haki.

Lakini Dkt Oluga anasisitiza kuwa mfumo huo bado unatumika. “Wakenya wanaopokea huduma kupitia SHA wote wamepitia mfumo huo. Changamoto ni uhamasishaji wa jamii kuelewa umuhimu wake,” anasema.

SHA inavutana na hospitali za binafsi hasa kutokana na msimamo wake wa kutotambua madeni ya NHIF. “Hatuambiwi ni lini tutalipwa. Lakini tunatakiwa kuendelea kuwahudumia wagonjwa chini ya SHA. Hii ni hali isiyowezekana,” anasema Dkt Anastasia Nyong, ambaye anaendesha hospitali ya kibinafsi mjini Nakuru.

Matokeo ya hali hii ni kuwa hospitali nyingi za kibinafsi zimepunguza idadi ya wagonjwa wanaodhiliwa na SHA.

Dkt Vitalis Ogolla, daktari wa meno na mtoa huduma wa zamani chini ya NHIF, anakosoa matumizi ya Sh104 bilioni kwa mfumo mpya wa wa SHA. “Fedha hizo zingeweza kujenga hospitali za rufaa sita. Huu ulikuwa mradi wa kunufaisha wachache,” anasema.

Dkt Lishenga anakubaliana naye, na kuongeza kuwa SHA ilikataa pendekezo la kipindi cha mpito cha miaka miwili.

Sababu nyingine inayozua wasiwasi ni utoaji wa huduma za afya za msingi bila ya kuchangia. “Huduma za msingi bila malipo zimepunguza motisha ya watu kuchangia. Kama unaweza kupata asilimia 90 ya huduma zako kwa kujisajili tu, kwa nini ulipie?” anahoji Dkt Lishenga.

Lakini Dkt Oluga anatetea SHA, akisema mapato ya sasa ni mara mbili ya yale ya NHIF. “Tayari tumeshalipa Sh50 bilioni kwa miezi nane, ikilinganishwa na NHIF ambayo ililipa kiasi hicho kwa mwaka mzima,” anasema.

Hospitali za kibinafsi zinalaumu Baraza la Madaktari na Madaktari wa Meno (KMPDC) kwa kuzipokonya leseni, kupunguza idadi ya vitanda na kuziwekea masharti mapya.

“Hatuwezi tena kusaidia akina mama kujifungua kwa sababu tunaambiwa hatuna daktari wa kugadisha wa kudumu. Hospitali ya serikali iko kilomita 80, na barabara huwa hazipitiki mvua ikinyesha,” anasema Dkt Victor Ng’ani wa Taita Taveta.

Lakini Dkt Oluga anasema:“Tunazingatia ubora wa huduma. Hatutaruhusu visa kama vya ‘Mugo Wa Wairimu’ kurudi. Mgonjwa ndiye atakuwa mfalme.” Licha ya matatizo, SHA ina mafanikio ya kidijitali. Mfumo wa mkataba wa kielektroniki umeondoa rushwa. Hospitali mashinani zinaweza kujiunga ndani ya siku chache.

Mfumo wa HIE – Health Information Exchange – unaunganisha data zote za afya kitaifa. Tayari umeonyesha mafanikio katika kugundua ulaghai na kuongeza kasi ya ulipaji wa madeni yakidaiwa.

“Tunaweka msingi wa teknolojia utakaohudumia Kenya kwa miongo kadhaa ijayo,” anasema Dkt Mercy Mwangangi, Mkurugenzi Mkuu wa SHA. SHA pia imechochea mjadala mkubwa zaidi kuhusu afya kuwahi kushuhudiwa nchini. Wakenya sasa wanajadili kwa makini viwango vya michango, huduma zinazopatikana, na ubora wa huduma. Mikutano ya hadhara kwenye kaunti huvutia mamia ya watu – na mitandao ya kijamii imejaa maoni kuhusu SHA.

“Tunajua mabadiliko haya ni magumu, lakini tunaunda mfumo wa afya utakaokua kulingana na mahitaji ya Wakenya. Muda utakapofika, kila mmoja atathamini juhudi hizi,” asema Dkt Mwangangi.

TAFSIRI: BENSON MATHEKA