Mwamko mpya kwa wafugaji wa mbuzi Kirinyaga wakipata huduma za AI
WAFUGAJI wa mbuzi katika Kaunti ya Kirinyaga wanatarajiwa kunufaika kufuatia kuanzishwa kwa Kituo cha kuendesha mbinu ya kisasa ya utungaji mimba (AI).
Kilifunguliwa rasmi na Rais William Ruto wakati wa ziara yake katika kaunti hiyo Jumatano iliyopita.
Kituo hicho, kilichoko katika Taasisi ya Mafunzo kuhusu Afya ya Mifugo na Masuala ya Kiviwanda (AHITI) eneo la Ndomba ndicho cha kwanza cha aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kinatarajiwa kuleta mwamko mpya katika sekta ndogo ya ufugaji, haswa kitengo cha ufugaji mbuzi.
Wakati wa shughuli ya kufunguliwa kwa kituo hicho, Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru alisema huduma za AI itakayotolewa katika kituo hicho zitachangia katika kuimarisha maisha wafugaji wa eneo hilo na uchumi wa Kenya kwa ujumla.
“Ni fahari yetu kuwa na Kituo cha AI cha kuhudumia Mbuzi hapa Ndomba. Hii ni rasilimali bora sio tu kwa kaunti yetu bali kwa nchi yetu. Kituo hicho kitachangia kuimarishwa ka uzalishaji wa bidhaa za mbuzi na chakula kwa ujumla katika kaunti ya Kirinyaga,” Bi Waiguru akaeleza.