Mwanachama mwenza wa Raila katika ukumbi wa mazoezi afunguka
HUKU taifa likiendelea kumuomboleza Waziri Mkuu wa zamani, hayati Raila Amolo Odinga, wengi wamekuwa wakisimulia namna alivyogusa maisha yao, iwe kisiasa, urafiki au kifamilia.
Lakini kwa Francis Mwangi, Mkurugenzi wa Lake Naivasha Institute, Raila hakuwa tu kiongozi wa kisiasa — bali rafiki wa karibu na mwanachama mwenza katika ukumbi wa mazoezi katika Maisha Gym, Serena.
Kwa zaidi ya miaka 10, Mwangi na Raila walikuwa wakikutana jioni mara tatu au nne kwa wiki kufanya mazoezi.
“Tulifanya mazoezi naye kwa muda mrefu sana. Kabati lake la kuhifadhi mavazi lilikuwa karibu na langu,” anasema Mwangi kwa sauti ya huzuni.
Kila walipokutana, Raila alikuwa mchangamfu na mcheshi.
“Tulikuwa tukizungumza kidogo kabla ya kuanza mazoezi. Alikuwa mtu wa furaha,” anaeleza.
Mwangi anasema Raila alikuwa mnyenyekevu kwa kila mtu, hasa wafanyakazi wa ukumbi wa mazoezi.
“Alikuwa akisalimia kila mtu. Hakuwahi kuzungumzia siasa akiwa ukumbini. Gym ilikuwa mahali pa faraja kwake,” anasema.
Mbali na mazoezi, Raila alikuwa mshauri wa afya na lishe kwa wenzake. “Alituambia tuwe tukila vyakula vya asili na kuzingatia muda wa kula kabla ya kulala,” anasema Mwangi.
Kama shabiki sugu wa Arsenal, Raila hakukosa kuchambua mechi za ligi kuu ya Uingereza.
“Alijua kila kilichokuwa kinaendelea katika ulimwengu wa kandanda. Tulikuwa tukicheka sana tukibishana kuhusu matokeo ya mechi,” anakumbuka kwa tabasamu hafifu.
Licha ya umri wake, Raila alikuwa na nguvu na ari ya kushangaza. “Alikuwa akifanya mazoezi ya kuinua vyuma vizito, kukimbia kwenye ‘treadmill’, na kufanya ‘stretching’ bila kusaidiwa. Wengi tulijifunza mengi kwa kumuona akifanya hivyo kwa saa mbili mfululizo,” anasema Mwangi.
Anasema kupitia Raila, alijifunza kuwa msimamo na kujituma ni silaha muhimu maishani.
“Kama alikuwa amekasirishwa na mambo ya kisiasa nchini, ulikuwa unaona kabisa moyoni mwake amesononeka, lakini hakuwahi kukata tamaa,” anasema.
Mwangi anakumbuka mara ya mwisho kumuona Raila ilikuwa Oktoba 2, 2025, kabla ya safari yake ya kwenda India kutibiwa.
“Aliniambia atarudi tukaendelee na mazoezi. Nilimtakia safari njema bila kujua ilikuwa mara yangu ya mwisho kumuona,” anasema kwa huzuni.
Kwa Mwangi, Raila atabaki kuwa mfano wa kuigwa — kiongozi, rafiki, na baba.
“Tulimuita Baba sio kwa siasa tu, bali kwa namna alivyotujali na kututia moyo. Ukumbi wa mazoezi hautakuwa sawa tena bila yeye,” anasema kwa sauti nzito.