Mwanachuo aliyeteswa na polisi alijiunga na Chuo cha Multimedia juzi tu
TREVOR Mathenge, akiazimia kupata shahada chuoni Multimedia kipindi kifupi baada ya kusajiliwa, alikumbwa na masaibu ya ghafla mnamo Jumanne.
Mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza katika kitivo cha masomo ya uanahabari aliongeza urefu wa orodha ya wananchi wanaodhulumiwa kila leo na maafisa wa polisi wasiojali.
Polisi hao, waliokuwa wanadhibiti maandamano ya wanachuo, walimwacha akiwa hoi taabani.
Kwa sasa Bw Mathenge amelazwa katika hospitali ya Orthopaedic Medical Services mjini Rongai.
Wanafunzi waliandamana kutaka hali ya maisha yao katika Chuo Kikuu cha Multimedia iimarishwe.
Wanafunzi walioshuhudia kisa hicho wanasema kulikuwa na makabiliano kati ya wanafunzi na maafisa wa polisi ambapo polisi walirusha mabomu ya machozi katika mabweni.
Akitafuta eneo salama, Mathenge alianguka kwenye shimo na kuvunjika mguu.
Licha ya masaibu haya, maafisa hao walimtoa shimoni na kuanza kumshambulia.
Kuna kanda ya video ambayo inasambaa mitandaoni kuonyesha polisi wakilipua bomu la kutoza machozi karibu na mwanafunzi huyo ambaye alikuwa hajiwezi.
Mathenge, ambaye alijiunga na chuo hicho Agosti 26, sasa anauguza majeraha na kusumbuliwa na kiwewe cha yaliyomkuta.
Mnamo Jumatano alifanyiwa upasuaji ili kushikanisha mguu uliokuwa umevunjika.
Hatukuita polisi
Kaimu Makamu Chansela wa chuo hicho Rosebella Orangi Maranga alipinga kuwa usimamizi wa chuo uliita maafisa wa polisi kudhibiti maandamano.
Wanafunzi walitaka usimamizi wa chuo kuhakikisha wana maji ya kutosha na kuimarisha hali ya usafi.
“Kwa kawaida haturuhusu polisi kuingia chuoni lakini jana (Jumanne) walikuta lango liko wazi. Hatukuwaita,” alisema.
Haijabainika bado kama wanafunzi wote walionyanyaswa na polisi walivunja sheria ama walikabiliwa kwa misingi ya Sheria ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi ya 2011.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Multimedia (MUKSA) Ronald Cheruiyot alisema kilichomkuta Bw Mureithi, ambaye alikaa wiki tatu pekee katika chuo hicho, hakikufaa kabisa.
Bw Cheruiyot alisema waliohusika wanapaswa kuwajibika kwa sababu maandamano yao yalikuwa ya amani.
Uongozi wa wanafunzi ulisema ulitaarifu huduma ya polisi kuhusu maandamano yao.
“Mguu wake wa kulia ulivunjwa, na katika onyesho la kutisha la kutojali maisha ya binadamu, maafisa hao walimwacha katika hali ya hatari, akiwa amezingirwa na vitoa machozi ambavyo vililipuka,” Bw Cheruiyot alisema akiongeza kuwa wameahirisha maandamano.
Polisi wakashifiwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Africa Hussein Khalid amelaani tukio hilo akisema kuwa ni jambo la kusikitisha kwa polisi kuwa na ukatili kiasi hicho.
Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (Ipoa) imeanza uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Mnamo Jumanne, maafisa wa Ipoa walizuru chuo baada ya kanda ya video kuonyesha dhuluma iliyotekelezwa na polisi kusambaa mitandaoni.
Uongozi wa chuo hicho baadaye ulitoa taarifa ukisema uhaba wa maji katika taasisi hiyo ulitokana na kuharibika kwa bomba kuu la maji lililoathiri mtiririko wa mara kwa mara wa maji katika chuo hicho.