Mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi alidhulumiwa kimapenzi – Wabunge
NA CHARLES WASONGA
KAMATI ya Bunge imethibitisha kuwa mwanafunzi mmoja alidhulumiwa kimapenzi katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi, Nairobi lakini ikashindwa kuthibitisha aina ya dhuluma kwa sababu kisa hicho kingali kinachunguzwa na asasi husika.
Kwenye ripoti ambayo imeidhinishwa na Kamati ya Bunge kuhusu Elimu lakini ambayo haijawasilishwa bungeni, kamati hiyo inaitaka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kukamilisha uchunguzi kuhusu kisa hicho haraka iwezekanavyo ili wahusika wafunguliwa mashtaka kwa mujibu wa sheria.
“Kamati hii inakubali kwamba suala hilo bado linachunguzwa na asasi husika kwa lengo la kuhakikisha kuwa mhusika anatambuliwa na kushtakiwa inavyopasa. Kwa hivyo, kamati hii haiwezi kutoa kauli yake ya mwisho wakati huu,” inasema ripoti hiyo.
Hata hivyo, ripoti hiyo ilijumuisha ushahidi wa wa Dkt Kanyi, mtaalamu wa masuala ya uzazi anayehudumu katika Hospitali ya Nairobi Women’s Nairobi ambaye alimchunguza mwathiriwa na kubaini kubaini kuwa akitokwa na majimaji meupe katika sehemu zake za siri.
“Sehemu ya siri ya msichana ilikuwa sawa katika uchunguzi zaidi ulionyesha kuwa ilikuwa ikitokwa na majimaji maupe. Uchunguzi wa kina wa majimaji hayo ulionyesha uwepo wa manii,” inasema ripoti hiyo.
Ripoti iliyowasilishwa kwa Kamati hiyo na Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) Thomas Mutie pia alithibitisha kuwa mwanafunzi wa kike alidhulumiwa.
“Uchunguzi wa kidijitali wa sehemu ya uke ulionyesha kulikuwa na majiji maji mweupe katika sehemu hiyo,” ikasema ripoto hiyo.
Kulingana na ripoti ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Tinderet Julius Melly, kabla ya usiku ambapo kisa hicho kinadaiwa kutendeka shule hiyo ya Wasichana ya Moi aliandaa mashindano ya michezo ya kuigiza baina ya mabweni hadi saa mbili za usiku.
“Wasimamizi wa shughuli hizo hawakuwa walimu ambao wameajiriwa na usimamizi wa shule kinyume na sehemu ya 23 (2) ya Sheria ya Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuhusu usimamizi wa michezo shuleni,” ikasema ripoti hiyo.
Sheria hiyo inawazuia watu wasiokuwa walimu dhidi ya kuwafundisha wanafunzi fani mbalimbali za michezo.
Kulingana na ripoti hiyo, wakati wa mahojiano mashahidi wote waliohojiwa hawakufichua kuwa kulikuwa na watu ambao sio walimu siku hiyo.
Wakufunzi na wasimamizi wa michezo hiyo pia hawatia saini stakabadhi zozote kuthibitisha ikiwa waliondoka shule baada ya michezo hiyo.
Wabunge hao pia wanasema katika ripoti hiyo kwamba usalama shuleni humo haukuimarishwa hali ambayo iliwaacha wanafunzi na walimu katika hatari ya kupata na madhara.
“Hakukuwa na kamera za usalama (CCTV) katika mabweni ya wanafunzi kwani kamera za zamani ziliharibiwa katika mkasa wa moto uliotokea shuleni humo mnamo Septemba mwaka jana,” kamati hiyo ikasema.
Vile vile, wanachama wa kamati hiyo waligundua kuwa kulikuwa na mlinzi mmoja pekee wa kike ambaye alisimamia mabweni manne, na kufuatilia mienendo ya wanafunzi na usalama wao usiku huo wa mkasa.
“Walinzi wengine shuleni humo usiku huo hawakubaini tukio lolote lisilo la kawaida usiku huo. Hii ndio maana kisa hicho kiliripotiwa na wanafunzi majira ya asubuhi,” ripoti hiyo inasema.
Kando na hayo ripoti hiyo ambayo huenda ikawasilishwa bungeni juma lijalo linasema kuwa milango ya bweni la Elgon ambamo tukio hilo linadaiwa kutokea ilikuwa kuukuu na katika hali mbaya.
“Milango ilifungwa kutoka ndani usiku huo ambapo kisa hicho kinadaiwa kutendeka hali ambayo huenda ilipelekea watu wasiojulikana kuingia mle,” kulingana na ripoti hiyo.
Katika mapendekezo yake kamati hiyo inaitaka Wizara ya Elimu kuhakikisha kuwa shule zote za umma zimewekwa kamera za CCTV ili kuimarisha usalama wa wanafunzi
Vile vile inapendekeza kuwa walimu wote wakuu kuhakikisha kuwa wakati wa aina yoyote ya michezo shuleni au nje ya shule, sharti wanafunzi waandamane na angalau mwalimu mmoja wa jinsia sawa ambaye amesajiliwa na TSC.
Pia kamati hiyo inapendekeza kuwa watu ambao hawasajiliw kuwa walimu, au walimu ambao waliondolewa katika orodha ya walimu kwa sababu za kinidhamu wasiruhusiwe kufunza, au kusimamisha shughuli zozote zinazowahusu wanafunzi.