Makala

Mwanamume ashuhudia ‘akizikwa’ kabla ya kujitokeza akiwa mzima

Na DAVID MUCHUI October 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAKAZI wa kijiji cha Nkamathi, Mutuati Kaunti ya Meru, Jumanne walishangaa kumuona mwanaume aliyedhaniwa kuwa amefariki na kuzikwa akijitokeza akiwa mzima na buheri wa afya.

Abdalla Mwenda, 20, ‘alizikwa’ Ijumaa wiki jana baada ya familia hiyo kutambua mwili uliopatikana katika nyumba aliyokuwa akiishi katika soko la Mutuati.

Bw Mwenda alishangaa kwa nini familia yake na wanakijiji walidhani amekufa bila kujaribu kumtafuta.

Baadhi ya wakazi walisema walikuwa wameshuku mwili huo na wakaiomba familia kufanya uchunguzi zaidi kabla ya mazishi.

Chifu wa Nkamathi Bernard Muroki alisema mwanamume huyo hakuwa amefika nyumbani kwa takriban miezi mitatu mwili huo ulipopatikana katika nyumba aliyokuwa akiishi.

“DCI imekuwa ikichunguza suala hilo. Inaonekana uchunguzi zaidi unapaswa kufanywa ili kutambua mwili ambao ulizikwa,” Bw Muroki alisema.

Ilichukuliwa kuwa marehemu alikuwa Mwenda kwa vile mwili ulipatikana katika nyumba aliyokuwa akiishi.

“Nilihitimisha kuwa Bw Mwenda alikuwa akiishi na mwanamke katika nyumba ambayo mwili huo ulipatikana katika soko la Mutuati. Mwili ulipopatikana, mwanamke huyo hakuonekana. Jambo hilo lilitatizwa na ukweli kwamba wazazi wake wanaishi Mombasa,” Bw Ithalii alisema.

Kaburi lililo na msalaba wenye jina Abdalla Mwenda ambaye alidhaniwa aliaga dunia. Picha|Hisani

Hata hivyo, kulingana na Mwenda, alitengana na mwanamke huyo na kuhamia Nthambiro, umbali wa kilomita 20 hivi.

“Kwa kuwa kazi yangu ni kuchuma miraa, mimi hutoka kutoka sehemu moja hadi nyingine. Nimeshtuka kupata familia yangu ilinizika,” alisema Bw Mwenda aliyekuwa ameshtuka.

Jambo la kushangaza ni kwamba mfanyakazi mmoja ambaye amekuwa akifanya kazi na Bw Mwenda, alisema walipita nyumbani kwa Mwenda siku ya Ijumaa mazishi ikiendelea.

“Tuliondoka Nthambiro, Igembe ya Kati siku ya Ijumaa na tulikuwa tuvune Miraa eneo la Ntonyiri. Tulipita nyumbani kwa Bw Mwenda na alishangaa kwa nini kulikuwa na watu wengi nyumbani kwao lakini tukaendelea na safari.”

“Siku ya Jumapili, mtu alitueleza kwamba Bw Mwenda alikuwa amezikwa. Bw Mwenda alishtuka sana hata akashindwa kufanya kazi. Akaenda kulala,” akasimulia mmoja wa watu wanaofanyakazi na Bw Mwenda.