MWANAMUME KAMILI: Jamani wazazi pimeni semi kabla kutamka!
Na DKT CHARLES OBENE
WIKI jana nilikumbana na migogoro kadha vyuoni iliyonihuzunisha mno.
Vyuo vikuu hali kadhalika taasisi za elimu ya juu zinazolenga kupambanua akili za vijana zimekumbwa na migomo ama migogoro isiyoeleweka.
Kwanza kabisa, wanafunzi waliokwenda kunoa akili zao kitaaluma ndio wanaochochea migogoro na vita hivi kwa kutatiza sheria na usimamizi wa vyuo. Isitoshe, baadhi ya wazazi vilevile wanaunga mkono ubozi wa watoto wao. Kulikoni?
Katika Chuo Kikuu kimoja kwenye kitovu cha Magharibi mwa Kenya, wanafunzi waligoma wakitaka “vyakula bora” badala ya “vya kawaida” walivyokwisha kuzoea siku nenda siku rudi.
Wasomi hawa ambao kwanza wanapokea mkopo wa masomo angalau kuwawezesha kumudu hali vyuoni wanataka vyuo vibadili mapishi na kuwa hoteli za kifahari. Afadhali wakwende kwao nyumbani panapopikwa vyakula bora!
Pamoja na “vyakula vya hadhi” wasomi hawa wanataka “marufuku kuingia mabweni ya kike ama ya kiume kuondolewa!”
Yaani wanataka maisha huru huria kuingia na kutoka kwenye mabweni hayo kwa wakati na kwa haja zao. Hebu niwajuze wasomi hawa kwamba hata nyikani kuna sheria zinazodhibiti hali na maisha ya hayawani.
Sembuse vyuoni? Kinaya ni kwamba hakuna hata mmoja aliyegoma kwa kuwa maktaba yanafungwa na kufunguliwa kama ofisi za serikali. Hayo mnayotaka mabwenini mtayapata tena makuu!
Pamoja na vijana waliokengeuka, baadhi ya wazazi walitia vidole vinywani wakitaka wasimamizi wa vyuo kuwapa wasomi ridhaa yao. Sijui kama hawa ni wazazi ama ni sampuli ya watu wazima waliozizima akili.
Jamani wazazi wa leo, pimeni semi zenu kabla kutamka mbele ya watu wazima.
Mwanamume na mwanamke kamili hujizatiti kufanya maamuzi magumu kwa manufaa ya vijana. Kufanya hivyo ndio kuwalea vyema!
Hebu tukumbukeni alivyofanya Rais wa Muungano wa Tanzania kupiga marufuku masomo ya vijana sambamba na ufuska. Hivyo ndivyo inatubidi kufanya katika taifa hili.
Vijana sharti kuchagua moja kati ya masomo ama anasa. Jamii yenye watu wazima haina budi kutunga sheria kuelekeza mambo kwa heshima na hadhi!
Mtoto ni mtoto na vijana wa leo wangali watoto wanaotegemea ufadhili wa walipa kodi na wahisani wala hawawezi kuchagua wanavyotaka kuishi kwenye mabweni vyuoni. Kama wamekwisha komaa nyonga, hawana budi kukodi nyumba zao nje ya vyuo wakapambana na hali zao kama wanavyofanya watu wazima.
Nasisitiza kwamba mtoto ni mtoto wala hawezi kujifanya mtu mzima kwa kuwa anatekenyeka maeneo nyeti. Isitoshe, jukumu la vijana wa leo ni kujizatiti kwa udi na uvumba kufanikisha maisha kupitia masomo.
Ole nyinyi mnaotaka kuzuru mabweni ya kike na ya kiume huru huria. Mtakuja vuna zao tosha la ulimbukeni huo.
Tatizo langu ni kwamba baadhi ya wazazi wanaounga mkono tabia za mahambe hawa hawajui maana na umuhimu wa vijana kufika na kufuzu vyuoni.
Labda ndio maana wanadhani vyuo vya elimu ni sawa na madanguro wanamoishi wao wenyewe. Hao ndio wazazi wenye akili duni wanaorudisha nyuma gurudumu la maendeleo nchini.
Lazima watu wazima wajumuike kuhakikisha vizazi vijavyo vinalindwa barabara kutokana na tabia za wachache weledi na wajuvi wanaotaka kuhatarisha maisha ya watoto masikini waliokwenda vyuoni kusoma.
Ulinzi huu unahitaji sheria kali ili kuzuia utundu na umero wa ujanani kuuharibu mustakabali wa vijana. Ndio maana nawakashifu wazazi wanaounga mkono matakwa ya vijana vyuoni.
Tazama jinsi taifa hili linavyolilia watu wadilifu wenye akili na ung’amuzi! Nani mwenye kutuokoa kutoka dhiki siku za usoni ikiwa vijana ndio kwanza wanaotaka kupapurana mabwenini badala ya kusoma kwa bidii na kufuzu vyuoni? Nini hatima ya mtoto kuzaa mtoto? Apandaye upepo atakuja vuna kimbunga!
Watoto wa leo ni kama mto unaofuata mkondo! Hatuna budi kuwapa mwelekeo kama watu wazima.
Miongoni mwetu, kuna wanawake kwa wanaume wanaojizatiti kila uchao kujijenga na kuimarisha mustakabali wao.
Kwa chudi na bidii, wanafanya kila jitihada kujiweka pema kiuchumi na kijamii. Juhudi za wangwana hao sharti kuungwa mkono. Hakuna haja kuishi kama vipofu wa akili, nafsi na ari ilhali tunazo akili timamu.
Tuogope nini ikiwa sisi watu wazima ndio kwanza tunaofadhili mahambe wanaotaka kuzalishana kwenye mabweni ya vyuoni?
Hekima ya mtoto mwema humwongoza kujua kwamba bidii masomoni ndio ufunguo wa maisha mema.
Vijana wanaotaka kuzuru mabweni ya wenzao hawana haja kusoma wala hakuna sababu kufuja pesa za umma kuwalipia karo ya bure. Hata kwao kuna vyumba vinavyoweza geuzwa mabweni ya anasa. Hiyo ndio kauli ya mwanamume kamili!