• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
MWANAMUME KAMILI: Kama kuzalisha ni raha, basi malezi yawe vilevile!

MWANAMUME KAMILI: Kama kuzalisha ni raha, basi malezi yawe vilevile!

Na DKT CHARLES OBENE

KINAYA cha maisha ni kwamba wanaume wa leo hawataki kuoa watoto wa watu waliohimilika ujanani maana “hawataki kulea watoto wa watu!”

Iwapo kila mkulima atawajibikia ukulima na uvunaji vilevile, basi hakuna shaka kwamba hasara na uharibifu wa mazao wenda ukadhibitika.

Tatizo langu ni kwamba gumegume wa leo wanazidi kuleta hasara kwenye jamii na familia za watu.

Vipi? Wanataka kula raha na kuwazalisha vijanajike ila hawataki kuwajibikia malezi ya “mazao ya ulaji raha!”

Hata vyombo vya dola vimechoka tena vimeacha kuangazia masuala ya himila za nyikani na vilabuni. Hakuna tena ukakamavu wa wanahabari kuangazia dhiki wanazopitia vijanajike.

Unyamavu huu huenda ukazalisha hasara zaidi.

Bila shaka wenda watu wamechoka kusikia lalama na lawama kutoka kila pembe juu ya dhiki zinazowakumba vijanajike.

Tuchoke tusichoke hili suala linazidi kuwa tata na linahitaji mikakati ya jamii na serikali angalau kutuepushia janga la kuwepo vizazi visivyokwisha machozi shavuni.

Ukweli ni kwamba, vijanajike wanakabiliwa na changamoto si haba! Si nyumbani si vyuoni, wanayumbishwa na kughilibiwa na papa na nyangumi ambao raha yao ni kuvizia na kula vya kuliwa bila haja ya kumwauni mtoto wa mtu. Inahuzunisha mno kuona idadi kubwa ya vijanajike ambao wamekwisha himilika japo wangali wadogo wa mwili na akili. Ni watoto, tena walezi wa watoto wasiojua wala kufahamu baba yao.

Zito zaidi ni kwamba, hawa watoto wanaolea watoto hawana kazi wala bazi. Watafanya kazi gani masikini hawa katika taifa ambalo linataka kuwaajiri wenye shahada na stashahada pekee? Wavipate wapi hivi vyeti vinavyotafutwa na waajiri ikiwa sare na vitabu vingali shuleni tangu mwanamtu kukwepa bwenini na kuingia mitaani mwingi wa haya ama shauku na hanjamu ya maisha?

Sina haya kuelekeza lawama kwa papa na nyangumi, yaani wanaume wa leo wenye tabia za kuzuzukia uzazi ilhali hawatoshi mboga. Mwanamume kamili ni sawia na mkulima anayewajibikia shamba na zao lote. Tatizo langu ni kwamba hawa papa na nyangumi wako mbioni kuwahadaa na kuwapotosha vijanajike kabla kuwatumbukiza kwenye lindi la majuto na dhiki ya malezi.

Hata baada ya kuzalisha wana wa watu, wanaume wa leo wangali mikekani na vijiweni wakitafuna meno badala ya kuwepo viwandani ama sokoni kuchuuza angalau matunda na mboga. Hawa ndio sampuli ya gumegume wanaotukosea akina sisi tunaojituma kiume ukulini.

Jamii vilevile inachangia utepetevu na uzembe wa wanaume wa leo. Ningalitaka kuona ndimi za moto zikielekezwa kwa wanaume wanaolala ilhali wamekwisha kuwa watu wa watu. Lakini bado hatujafikia kiwango cha kuwapa wanaume wazembe shuruti.

Linalohuzunisha zaidi ni kwamba, mwana wa kike kushika mimba angali nyumbani kwao huchukuliwa kama kosa la kijanajike. Ndio maana wanalaaniwa na mamamtu kulaumiwa kama kwamba walikuwa mtu na ngozi katika mahaba ya nyikani.

Pongezi hata kwa yasiyofaa

Lakini mwana wa kiume anapompachika mimba masikini mtoto wa mtu, anasifiwa na kupongezwa kama kwamba hajakosea wala kuvunja miko ya maadili. Na iwapo ataadhibiwa na yeyote, basi adhabu yake itakuwa tu kushauriwa kuwa makini wakati ujao. Hapo ndipo jamii na jamaa wanaponikosea na kunivunja moyo.

Mwana wa kike kushika mimba huashiria mwanzo wa maisha ya dhiki. Hata malofa na gumegume wa leo hawana haja kuoa waliohimilika wangali watoto maana “hawataki kulea watoto wa watu!”

Kinaya ni kwamba watu ni wao hao wasiotaka kuwajibikia malezi ya watoto wao.

Na hata wanapoolewa hawa watoto wanaozalishwa wangali watoto dhiki zao zingalipo. Hivi maajuzi nilikuwa kwenye kikao cha wazee wenye ghadhabu. Tangu mwanao kuolewa hawajamwona mumewe ama wazazi wake. Ajabu ni kwamba binti yule amekwisha kopoa mara saba tangu kufika nyumbani kwa mumewe!

Ndio wanaume hao! Haja yao kukugeuza shamba kuatika mbegu, malezi juu yako! Sivyo afanyavyo mwanamume kamili. Kama kuzalisha ni raha na malezi vilevile. Huo ndio wajibu wa mwanamume kamili.

 

[email protected]

You can share this post!

SHERIA: Huwezi kumzuia kuoa au kuolewa akitimiza umri

TAHARIRI: Serikali inasinzia klabu zikitatizika

adminleo