MWANAMUME KAMILI: Katika usasa, hakuna nafasi ya upofu wa akili, nafsi na ari
Na DKT CHARLES OBENE
KINYUME na wanavyodhani wanaume kwa wanawake wazembe wa leo, mwanadamu awe mkubwa ama mdogo ana nafasi yake katika ulimwengu huu wenye nafasi tele!
Kuna jambo moja linalovunja moyo maishani mwa wanaume kwa wanawake wa leo.
Nazungumzia ubishani na mizozo inayoletwa na kuwepo watoto nyumbani!
Mtoto mtukutu na mtundu hutengwa na kuitwa “wa baba” ama “wa mama!” Vijanadume wasiopata kitu shuleni hulengwa mno na mama kwa kuwa “na akili za baba!”
Vijanajike wenye akili butu darasani nao hujikuta wakizomewa na kuitwa “mazuzu kama akina mama zao!”
Kinaya ni kwamba kila mzazi anataka kujihusisha moja kwa moja na watoto machachari, makini na werevu darasani. Hapo ndipo utasikia, “ana akili zangu huyo!”
Ukweli wa mambo ni kwamba huu ubishi na mizozo juu ya watoto husababishwa na uzito wa mzigo wa malezi. Hakuna mzazi aliye radhi kujinyima kwa ajili ya mtoto asiyeonyesha ishara ya matunda mema.
Isitoshe, baadhi ya wazazi wa leo huingia chumbani nyonga zao kuzitwanga bila kujali vipi watalea matunda ya mahaba baina yao.
Kweli, malezi ndio mwiba unaozichoma nyayo za wapendanao hadi kuwafanya mahasidi kufarakana hadharani na kutengeana watoto.
Sijui nini au nani anayestahili kulea watoto wasiopata kitu shuleni ila najua kwamba mapenzi baina ya mwanadamu yako kuwajibikia kila mtoto pasipo kuwabagua.
Akina yakhe wanaobagua watoto ni sampuli ya wazazi wasiofaa hadhi wala kuhitaji watoto!
Hii ina maana kwamba wanawake kwa wanaume wa leo sharti kujizatiti kila uchao kuweka mikakati inayolenga kuimarisha na kudumisha hali nzuri na maisha mema baina yao.
Sharti kukuza chudi na bidii – kazi kuzifanya na wenzao kuwafanyia kazi angalau kujiweka pema kiuchumi ili kumudu gharama zote za malezi ya familia na jamaa.
Tatizo kubwa linaloghubika na kuzinga maisha ya wanadamu ni kuwepo akina yakhe wasiofanya jambo la msingi ila kusaka mapenzi katika mabaa na madanguroni.
Inahuzunisha kuona kwamba uwindaji wanawake umekuwa kama kazi kwa baadhi ya wanaume wa leo.
Ni watu wazima wenye misuli na usulisuli ila hawataki kutumia akili kufanya la tija.
Najua nyie wajuvi wa kupekuapekua mambo mmekwishaanza kutafuta sababu kama ilivyo kawaida kwa mahambe na wazembe.
Mtasingizia kwamba hamna kisomo cha kuwafaa kupata kazi za tija.
Hata ikiwa hamkusoma, basi hata wepesi wa kufahamu kibinadamu hamna? Kila mwanadamu ana nafasi yake katika ulimwengu huu.
Wanaume wa leo balaa.
Wanapoamka asubuhi, kazi wanazofanya ni kusimama stanini kuamkiana na vimwana na kujifanya kuwauzia kanchiri, chupi, poda, wanja, marashi na peremende.
Sielewi vipi mke anavyoweza kusahau kuvalia vyake vya ndani kisha akashawishika asubuhi na mapema kununua kanchiri na chupi kwenye stani badala ya kwenda kazini. Jamani wanaume!
Kazi ni kazi eti. Ndivyo wanavyojitetea wazembe wa leo. Mbona sijawaona mmeketi juu ya mbuzi nazi kukuna, kuichuja na tuwi kunogesha mboga?
Mume mwenye ari akijua vyema thamani yake hawezi kamwe kuzifanya kazi ambazo hata posho kujinunulia muhali. Ubwete huu si kazi.
Lengo lao hasa ni kufuata wanawake na kutafuta uchumba na usuhuba unaodhamiria kuchururiza mahaba – kama hayo ndiyo mahaba!
Hawa wasiochangia ukuaji wa uchumi, wasiotaka na wasiojua maana na umuhimu wa mume kufanya kazi ya tija ndio zumbukuku waliokatiza tamaa ya wanawake kuposwa.
Kucha kutwa hawaondoki chumbani wakatafuta angalau punje la nafaka. Wajapo watoto watakula nini?
Hawa waliolaza damu ndiyo wengi wanaoendeleza dhana kwamba mapenzi ni kizibo kisichomwezesha mwanamume kunena.
Ugumu wa maisha
Na wengi ndiyo kwanza tumenyamaza tusijue lipi kufanya lipi kutamka. Ugumu wa dunia umetufanya bubu maana hata watoto tumeshindwa kuwalea seuze mapenzi?
Kazi ya mwanamume kamili sio kila mke kumfakamia kinywani. Hilo liwaingie masikioni na kutua moyoni.
Heri mke kuzifanya kazi hizo za kijungumeko kama lazima kuzifanya!
Zindukeni nyie mnaochuuza jozi moja la viatu – tena vyenyewe kuukuu visivyoweza kuvutia hata mnunuzi wa mavulia.
Mwanamume kamili huamka majogoo mwingi wa ari kuchuma kwa ajili ya familia na jamaa. Isitoshe, huchuma juani akaekeza katika amali inayodumu ili kuwapa watoto uthabiti wa siku za usoni. Katika usasa, hakuna nafasi ya mwanamume kipofu wa akili, nafsi na ari.
Dunia ya leo inahitaji mwanamume anayeweza kubadili maisha ya familia na kuwapa watoto utamu wa maisha ya kisasa. Wajibikieni maishani kabla kuanza harakati zenu kuzaa na kuzalishana.
Msipofanya kazi za tija nao watoto mtawabagua kwa misingi ya akili na werevu darasani.
Baruapepe ya mwandishi: [email protected]