MWANAMUME KAMILI: Kucheza na dume la leo ni kuhatarisha shoka fuvuni!
Na CHARLES OBENE
DAMU ya usalata ingali ardhini, vidimbwi vidogo vidogo vya huzuni vimetulia na kushikamana na ardhi kama ithibati ya kupinga mauaji ya kikatili yaliyotokea maeneo ya Eldoret na Nyeri.
Mjini Eldoret, tunahuzunika mno jinsi mwanamume alivyodaiwa kuhitimisha safari ya maisha ya kichuna mmoja kwa kutumia shoka!
Ole nyinyi watoto wa watu mnaotafuta wanaume waliolelewa vichakani wakichanja kuni ama kufyeka misitu!
Huenda wanaume sampuli hiyo wasione tofauti kati ya mwanadamu na miti iliyokauka.
Kweli, kuna uwezekano mkubwa wanaume hawa kutotambua kwamba shoka halina nafasi katika maisha ya binadamu sisemi kutumika kama kifaa cha adhabu.
Katika eneo la Nyeri, mwana wa masikini aliasi shule ya upili akaona heri kutia mkono mzingani kuhisi uchungu wa usena wa nyuki. La ajabu ni kwamba mwanamume mtu mzima alikubali kuhitimisha masomo ya mwanadada yule ili wakaoane.
Hebu tafakari kwa kina.
Mwanamume alimhimiza mwanamke kuacha shule ili wafurahie ujana na ujanja wao pamoja!
Matokeo ya ulimbukeni ule ni mauaji yaliyotekelezwa kikatili mno.
Mama wa watoto wawili alivamiwa usiku akafumwa kifuani na mumewe.
Ampungia dunia na utamu wake mkono wa buriani katika umri wa miaka ishirini na tatu! Lau angalijua kwamba mapenzi ya ujanani yangalimzolea kifo, labda angalisalia shuleni – maktabani akisomea taaluma ya kumfaa maishani!
Lakini kijanajike yupi mwenye macho kuona uchungu wa vifo kama hivi?
Tunajifunza nini katika visa hivi viwili? Wanaume wa leo wanasifika kwa kauli mbiu ya jicho kwa jicho! Hawajabadilika wala hawatabadilika milele! Mwanamtu kuacha ya shuleni na kushikamana na mume asiyependa masomo ni kujichimbia kaburi!
Mwisho wa tamaa ni mauti. Ole nyinyi vijanajike mliozamisha akili kwenye simu na mitandaoni kucheka na kucheza na madume wa leo! Hamjaona uchungu wa shoka fuvuni!
Ole nyini mnaotafuta pesa za ususi – angalau kununulia singa za Kichina.
Ole nyinyi mnaotoroka maktabani mkakimbilia vilabuni kunywa na kula vya bure!
Sielewi wala sitaelewa jinsi mwanamke anavyoweza kuhitimisha masomo kwa kuwa amekwisha kumpata mwanamume aliyeradhi kumpeleka chumbani wakazae na kulea watoto!
Jamani vimwana wa leo, lini mtapata funzo mkasitisha ulimbukeni wenu?
Jicho kwa jicho hupofusha mji. Hivyo ndivyo walivyosema wangwana wanaojua hekima ya kuishi na waja wastahiki.
Je, wako wapi wangwana katika dunia hii inayotawaliwa na madume pwaguzi?
Matapeli hawa ndio kwanza tishio kwa muamana na mshikamano wa jamii.
Mlaji wa mali ya mwanamume hana chake.
Tukubali yaishe!
Nawatahadharisha nyie wanawake wa leo mlioingiwa na pepo wa pesa! Hata katika mitandao ya kijamii mko mbioni kutafuta madume wenye pesa.
Yaani hamna haja tena kuwachumbia walalahoi wenzenu wanaobahatisha maisha ati.
Lakini ulafi huu ndio kwanza utawakutanisha na dhoruba ya shoka! Mwanamume wa leo ndiye pwaguzi hasa. Nyie pwagu vichuna wa leo hamtoshi mboga.
Mwanamtu chezea maisha, lakini tarajia kivumbi na dhiki maishani.
Wewe kidokozi utaliwa na kuachika kinywa juu mfano wa jibwa aliyepata kichapo kukanyaga asikoalikwa! Ole nyinyi mnaopigiwa upatu kwa viuno vyenu!