Makala

MWANAMUME KAMILI: Lau kama si kiboko, hawa hawangeitwa wanaume!

September 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na DKT CHARLES OBENE

KUNA haja ya jamii kuhamasishwa juu ya athari ya kuwepo wanaume-jina!

Yaani wanaume kwa kuwa maumbile yao ni ya kiume. Lau kama si kiboko walichozaliwa nacho, hawangejumuishwa kabisa kwenye kundi la wanaume.

Nasema hivi kwa sababu baadhi ya babu, baba na kaka zetu wanazidi kufanya vijimambo visivyokuza hadhi na heshima ya mwanamume kamili.

Zingatia kile kisa cha mwanafunzi wa kike kujitia kitanzi katika Kaunti ya Bomet. Inadaiwa kwamba mwalimu wa kike alimvunjia heshima mno kijanajike kwa kumzomea na kumfedhehi hadharani.

Kama kawaida ya vijanajike wanaovunja ungo; hasa akina sisi watoto tuliozaliwa hoi, tunaoishi hoi na wazazi wetu wenyewe walalahoi – si nadra kukanganyika na kushindwa kumudu usafi.

Nakumbuka sana enzi za utotoni nikioshwa gwarideni msimu wa kipupwe tena mbele ya hadhira ya wanafunzi walionihurumia mwisho wa huruma.

Ningalikuwa na maji safi, sabuni na mafuta yenye marashi, ningaliwajibika mwenyewe kuepuka aibu na adhabu kuoshwa mbele ya umma.

Zito zaidi katika kisa hiki cha mwanafunzi kufa kwa hasira ni kwamba walimu wa kiume hawakuingilia kati na kumkanya mwenzao wa kike aliyetema matusi na kebehi.

Badala ya kuwa wanaume tena watu wazima wenye akili timamu, waligeuka vijitoto vya chekechea waliomcheka mwanafunzi tena mwanao aliyeshindwa kumudu hali ya hedhi.

Hebu tafakari kwa kina hali ya walimu wa kiume kumcheka kijanajike kwa kuwa kalemewa na maumbile! Namtakia mwendazake msamaha kwake Rabana, roho yake isijepata dunishwa mbele ya malaika.

Alikuwa mtoto mdogo aliyetumainia watu wazima kumwelekeza kimaisha na kumpa nasaha badala ya kumcheka na kumtania hadharani.

Hakufeli kimaisha ila hakuona mwanga kuishi na watu wazima ambao walimpokonya uzima.

Ningalikuwa katika hali yake, uamuzi ungalikuwa huo huo! Hakuna mja anayeweza kustahimili kuvunjiwa heshima hasa na mtu anayemtumainia kimaisha.

Kila panapotokea kisa cha mauaji ya kikatili hapakosi mhusika mwanamume.

Yaani kazi ya wanaume wa leo ni kushirikiana ama kushirikishwa kutekeleza unyama dhidi ya wanawake ama wanaume wenzao.

Ama wanapokea malipo na kutekeleza unyama dhidi ya wenzao. Ndio maana nashindwa elewa akili za babu, baba na kaka zetu wa leo. Vichele vya pesa vinatosha mwanamume kumtokomeza mwenzake bure bilashi? Hela na mali alizopokea Yuda Iskarioti zilimfaa nini? Hatima ya wasaliti ni hiyo hiyo!

Chanzo cha visa vya kikatili ni tabia ya wanaume kufanya mambo bila tafakari wala akili! Kweli, hana muda kupangia wazo na kulitekeleza kimpango.

Ndio maana wanakwenda vilabuni Ijumaa na kurudi Jumamosi asubuhi wamekwisha oa ama wekwa rumenya bila kujua hata jina la mke! Tatizo kubwa ni kwamba hizi ndoa za kuajabia zimekuwa si tukizi tena.

Ndio kwanza hali ya kawaida waja wa leo kukutana vilabuni na kuamka asubuhi wakiwa mke na mume. Hizo ndizo akili za wanaume wa leo. Vipi tutaepuka kufumana mishale?

Hata wanaofunga ndoa na sherehe za harusi wako mumo humo kwenye makundi ya watu wanaofanya mambo bila akili wala tafakari.

Ajabu ya ndoa za leo ni kwamba ugomvi, nguo kuchaniana na watu kufedheheshana mitandaoni unazuka hata kabla kivumbi cha harusi kutulia. Makofi kwa makonde yanaporomoshwa watu wakiwa kwenye pilkapilka za fungate na viungo kukataa kuungama.

Mwishowe waliopendezana wakapendana wanabaki kuwa mahasidi vita kupigana na usaha kutumbuliana! Hicho ndicho kinaya cha ndoa za leo.

Sijui na sina haja kujua nani wa kulaumiwa. Nijuavyo ni kwamba wapo wanaume ambao wenyewe hawajielewi tena hawataki kujua maana ya mwanamume kutumia akili kama mume.

Gumegume hawa wanazo akili ila hawataki kuzitumia kufanya maamuzi ya watu wazima. Wapo vilevile vimwana wasiojali utu – mtoto wa mtu kujitunza na mali yake kutilia poda na nakshi kabla kumkabidhi mume mmoja ufunguo wa mzinga – asali kugema kwa raha yao daima dawamu!

Tatizo kubwa zaidi ni kwamba vimwana wa leo ndio kwanza mahambe waliokosa hekima na mwanga wa mke mwema. Wakipelekwa shule hawataki kusoma. Wanataka kwenda vilabuni kula na kunywa. Hawataki kujijenga kiakili. Wanataka kututumia dodoki vifuani na kutononesha vya haja na hamjamu.

Ndio hao wanaokwenda kwa mume wakaolewa kwa kuvutiwa na kitanda cha sufu au runinga sebuleni!

Haistahimiliki kwamba mke wa karne hii anazuzukia televisheni na mazulia kwenye sebule ya nyumba ya mwanamume! Mwanamume asiyetimiza vigezo alivyoweka mke asione hata shanga kiunoni!

Mimi sijaolewa na mtu asiyetimiza vigezo vya mwanamume wa karne hii! Lakini sitaki kuolewa wala kuoa. Sijatosha mboga wala kitoweo! Napambanua hali yangu.

 

[email protected]