MWANAMUME KAMILI: Mume kamili ni shujaa kwa msimamo usiotetereka!
Na DKT CHARLES OBENE
USHUJAA wa mwanamume ndiyo hamasa tunayohitaji katika jamii.
Ni wajibu wa kila mwanadamu kwanza kukubali ukweli wa hali yake duni; halafu kujiamulia bila shuruti kuwa mtu mbele ya watu.
Mtu ni utu. Utu wake hudhihiri katika ungwana na ukweli wa semi zake. Ukweli ni ngao! Kinga zake hasa kwa maisha ya mwanadamu hazimithiliki. Kwanza kabisa, inasikitisha kwamba tumezoea kama taifa na jamii kupewa ahadi zisizo kitu ila hewa na mvuke tu wa wanasiasa. Tumekwisha kuwa taifa na jamii inayothamini uongo kuliko ukweli.
Ajabu ni kwamba tukidanganywa waziwazi tunacheka, tunachekacheka nao, tunachekeshana kama kwamba tumeona lulu! Je, ni vigezo vya utu tulivyoshusha daraja ama ni matatizo mengi yametufanya watu tuliokosa utu? Hapo pa uongo ndipo tulipokalia kama taifa na jamii. Hatuna aibu hata kwenye mawasiliano kusema, “nisubiri naja! Niko hapo hapo karibu nawe!”
Yaani tumekwisha kuwa kama mazingaombwe; tunajipeleka kinafsi kwanza, kabla hata mwili wenyewe kufikishwa tunaposubiriwa! Bila shaka umekwisha sikiliza hadaa hizo za “niko hapo hapo!” haiwezekani mtu mwema “aliye hapa” vilevile kuwepo “hapo hapo!” Huo ni mzaha usio nafasi katika maisha ya watu wangwana!
Tulivyo “wananchi wema”, hasa akina sisi tunaotapata kimaisha, tena tunaopapasa maisha katika mabanda yaliyojengwa migongoni mwa mitaa ya watu tajika; tupate wapi nguvu kupinga wenye nchi wanaotulisha, wanaotuvisha na wenda wakatuvusha ng’ambo ya pili yenye matumaini? Hatuwezi thubutu kunena mbele ya wangwana wanaotupa hewa na mionzi vilevile ya kuivuta ndani mapafuni. Jamani tujalize nguvu ewe Rabana, tusijekata tamaa kabla kuyaona mengi mema kutoka kwa wenye nchi hawa waliotushika tukashikamana! Wametulisha uongo tukanata kama gundi. Hatubanduki lije jua ije mvua. Sasa uongo huo unazidi penya hadi kwenye vyumba na vitanda vyetu!
Kweli, hatuna hata akili tabaradi kuhoji ukweli wa ahadi chungu za wanasiasa.
Wametushawishi, wametushinikiza, wametuhimiza, sasa uongo wao umehanikiza na kutufanya “wananchi wema” kwa utiifu, amani na upendo kwa nchi na wenye nchi! Ndio maana wametuzoea, nasi tukawazoea na uongo kushamiri na kuwa sehemu ya maisha yetu. Hatuna budi kubadili hali hii iliyojaa unyonge na unyong’onyevu. Mwanamke na mwanamume kamili sharti kuhoji mambo na kutathmni ukweli kabla kusadiki na kufia papo hapo! Huo ndio ushujaa wa mwanamume kamili.
Ni muhali kumpata mwanamume kamili kati ya mahambe wa leo waliozoea kuwahadaa watu kwa hongo na uongo. Wiki jana nilishuhudia kisa cha ajabu. Gumegume mmoja aliyeishi na mke akamzalisha mara saba, alikiri kwamba “hakumpenda tangu wakutane miaka kumi iliyopita!” Hapo pa “mapenzi” tupaweke kando kwanza! Nitawaachia nyie wenye meno kutafuna mabuyu hayo. Mimi mwana wa kukopolewa kwenye jamvi sina mazoea wala weledi wa mambo ya mapenzi.
Mbona dume lile halikusema ukweli mapema? Mbona akampa mwenzake kichefuchefu mara saba pasipo mapenzi? Angalau mara moja tungesema ilikuwa kionja mchuzi.
Mara ya pili tungesema ilikuwa unyonge wa mkono kuzoea kuchovya gizani. Ama ajali isiyo kinga. Lakini mara saba ilhali hapakuwa na chembe wala tone la mapenzi ni mzaha! Hao ndio wanaume tunaowatumainia kutufanya watu mbele ya watu. Watawezaje kutupa matumaini ikiwa ukweli ni adimu kama barafu ya kukaanga?
Mwanamume mngwana hana budi kufunguka moyo. Hutangaza waziwazi hali ilivyo na ikibidi hujizoazoa kama ndama akipendezwa moyoni. Sichelei kunenguka na shuka kiunoni kama ishara ya moyo kutulia na mkono kutua kifuani panapopendeza! Huo ndio ukweli wa mwanamume shujaa. Ukweli ni ngao! Hamna budi kuyatoa yote moyoni angalau tusijeishi na kusubiri upepo ilhali hakuna kitu!
Nawapa changamoto wanaume wanaozalisha wanawake kisha wakaibuka na hekaya za kitoto kwamba “hapakuwa na mapenzi!” Sasa hao watoto waliozaliwa “bila mapenzi” watalishwa na nani kama baba wamekwisha tokomea nyikani? Tafuteni nafasi katika siasa maana mmekwisha tosha mboga! Afadhali tudanganywe kwenye majukwaa la siasa wala sio kwenye vitanda na jamvi tunapotafutia liwazo, tena tunapozalia vizazi vya kesho. Hapo pa kuzalishana tusithubutu kuleta mzaha na utoto wa baadhi ya wanaume wa leo.
Hii dunia haina nafasi ya watu wasiojua wanachotaka kimaisha! Msema kweli ndiye mlaji mwema! Kama lazima kula vya watu bure bilashi, huna budi kumweleza mwenza kwamba haja yako sio kuoa. Tangaza msimamo waziwazi kwamba unataka “jukwaa la mazoezi” ukisubiri kutia njuga kwenye “uwanja wa maisha!” Ole nyinyi mnaojua waliko wema wa kesho! Iwapo yuko mtu aliyeradhi kukujaalia mema kufanyia mazoezi, fanya shibe yako! Hata heri haina pingamizi kwa ridhaa ya wawili wenye akili timamu
Anajua vyema mamangu kwamba nakshi zake ndizo maisha yangu. Sina haja kujishaua na thureya za mbingu wala kusaza maboga ya shamba. Moyo kuridhika ni chaguo la mtu. Uangavu na ucheshi wake ni jaala tena ithibati ya wema wake.
Amekwisha kunionyesha wema, akanizidishia subira na matumaini; ya mbali kuyaleta karibu. Hivyo ndivyo anavyofanya mke mwema. Ole nyinyi wenye haja ya kuwafanyia wenzenu mazoezi bila kuwahakiki wala kuwahakikishia safari ya pamoja!
Nahema juu kwa juu maana nimekwisha tangaza msimamo. Bila shaka anasubiri “vijipaka na vijibwa” vitakavyomlambalamba usoni kama anavyopenda nitania. Mwanamume kamili ni shujaa kwa ukakamavu na msimamo usiotetereka wala hofu kwa kitu ama mtu yeyote.
Tunahitaji hamasa na mshawasha wa ushujaa hasa katika nyoyo za wanaume wa leo. Ushujaa wa mwanamume unaweza kudhihirika katika vita na jitihada zake kukomesha ulimbukeni wa wanaume. Tumechoka na hongo na uongo wa baadhi ya wanaume wa leo.