MWANAMUME KAMILI: Ole wenu mnaotegemea nguvu za mikwanja kuteka vimwana!
Na DKT CHARLES OBENE
NAWAHONGERA tena nawapongeza vimwana wa leo waliokwisha erevuka na kutambua kwamba mapenzi sio pesa!
Mapenzi ni sawa na nyama ya porini. Kwanza, kula ni haramu. Mlaji na yeyote mwenye haja kula nyama ya porini sharti kutaka ridhaa na ruhusa ya mamlaka husika.
Nimezungumzia mara kwa mara umuhimu wa mwanamume kamili kujitambulisha rasmi nyumbani kwa wakwe zake.
Mama na baba zetu wanaokula pembeni tena kwenye kiza cha maki sio wanaume hasa. Wanamithilishwa na majangili wanowinda na kula haramu.
Sielewi wala sitaki kuelewa vipi mwanamume anavyoweza kutwaa ruhusa kuzaa na kuzalisha mwanamtu ilhali hajui anakotoka wala hajulikani nyumbani kwa mke.
Hebu tukivalie kiatu kuumeni. Mzazi yupi atakayefurahia mwanawe kutekwa nyara, kugaragazwa na kuzalishwa mfano wa panya na gumegume lisilojulikana hata kutuzi la kwapani?
Haidhuru upana wa pua, lakini mwanamume sharti kupeleka uso wake kwa wakwe zake.
Kula haramu ni kula dezo! Sivyo anavyofanya mwanamume kamili.
Pili, nyama ya porini hailiki mbichi! Sharti mwindaji kujua vipi kuandaa mchuzi ama kuichoma barabara. Hata matunda ya mwituni yanalika mbivu! Maboga ya shambani sharti kuchemshwa. Njugu hukaangwa. Hata wanaokula nzige wanajua tosha hekima na ustaarabu unaohitajika. Nyie mnaofakamia wenzenu vinywani kabla kupika ni wanaume sampuli gani?
Mwanamke anahitaji kwanza nafasi bora shuleni apate elimu ya maktabani kabla kunogeshwa ile ya unyagoni. Anahitaji elimu ya maabarani kabla kutia guu barabarani na mikoba begani. Anahitaji hekima ya biashara, uchumi, diplomasia na hata uhandisi kabla ya kujitosa katika biashara ya “chumwa chuma!”
Mwanamume kamili anajua tosha umuhimu wa kumpa mke nafasi kutwaa taaluma kimaisha. Mke wa leo sio runinga kutazamwa sebuleni. Tuacheni ujahili wa kutatiza masomo ya vimwana wa leo kwa mapenzi hadaa na vichele vya pesa. Mtu ni utu wala sio pesa!
Tatu, mwindaji hana budi kujituma kabla kuchuna ngozi na kula nyama ya porini. Ulaji nyama ya porini huhitaji sana maarifa, ujuzi na bidii maana wanyama wa porini wanajua maana ya “kwenda kasi!” na maana ya “kukwepa mitego!” Ole nyinyi wenye nyenzo za kobe katika dunia hii iendayo kasi kama umeme! Poleni sana nyie mnaotegemea nguvu za mikwanja kama vishawishi vinavyoteka vimwana wa leo. Kama kuku wamekwisha erevuka kukwepa mitego na nafaka, sembuse vimwana wenye akili na nafsi?
Nasema hivi kwa kuwa wanaume wa leo wanaendeleza ile dhana kwamba pesa zinatosha kuwapa “nyama ya porini!” Ndiyo maana nawapa hekima ya bure. Wanawake wa leo wanathamini sana utu kuliko pesa. Nikisema wanawake, nina maana ya watoto wa watu waliolelewa kimaadili, wanaojua nini maana ya mke mwema! Watoto wanaojua nini hadhi ya mke. Wako vilevile vicheche wanaosema heri nzi kufia kidondani kuliko kufia majutoni. Hilo ni chaguo lao. Kila mtu hutafuta sana asichokuwa nacho. Sijui wewe huna nini!
Kweli, mwanamke mwema havutiwi na kipochi ama kima cha sarafu kwenye akaunti ya mwanamume. Mwanamke mwema anaweza kuacha pesa za walalahai mwishowe akaondoka kwenda kutafuta ridhaa ya roho yake kwenye kijumba cha mlalahoi.
Utu ndio uzi pekee unaounganisha matabaka ya watu. Wanaume wenye utu wanajua kwamba mke sharti kulipiwa posa kabla kuzalishwa. Mke mwema ana gharama kuliko kitita cha dhahabu. Ole nyinyi mnaotafuta vya dezo vilabuni mkavipeleka vitandani; vya siri mkaviona kabla kuvitolea jasho! Na kama vya siri umekwisha kuviona, huna budi kuvunja kuta za benki mwanamtu kumfidia! Hivyo ndivyo afanyavyo mwanamume kamili. Akili razini ni johari za mwanamke na mwanamume kamili!