MWANAMUME KAMILI: Wajibikeni kukomesha hizi tabia za kipuzi za binti zenu!
NA CHARLES OBENE
Kuna haja kuu kutambua mahali pa wazee wa hekima katika maisha ya vijana wa leo. Vijana wa leo wanahitaji mwongozo angalau kujuzwa mbivu na mbichi ya dunia hii chakaramu. Hawajui wala hawana muda kujua kwamba dunia hii ni mti mkavu dhiki kuuparamia.
Vijanajike kwa vijanadume wanahitaji nasaha ya watu wazima ili kuwapa mawazo chanya kuwapevusha na kuwatahadharisha dhidi ya kufanya mambo kama watu walioondokewa na akili.
Vijana wanahitaji elimu ya mkekani hata kabla kusukumwa kwa lazima kwenda huko maktabani. Kweli, hawa vijana wa leo sharti kusukumwa kwenda shule.
Hawajui wala hawana haja kujua umuhimu wa mtu kuelimika. Waende shule kufanya nini ilhali wanazo rununu zenye kamera? Shule ina manufaa gani kuliko picha kwenye mitandao? Ndio maana wanahitaji kusukumwa kwa lazima kwenda shule!
Wanahitaji vilevile kusukumwa kwa lazima kwenda maabadani. Nalazimika kusadiki kwamba vijana wa leo wanaishi katika dunia yao pekee.
Ndio maana sharti kuwaleta kwa lazima karibu na Muumba. Imani ya mtu ni ngao pia inayoweza kumfaa kujikinga na mishale ya tamaa na uroho. Na vijana wa leo ndio kwanza wamejua maana ya tamaa!
Alitoka wapi yule mwanafunzi aliyefumaniwa danguroni na sare za shule? Alikuwa na haja gani iliyopiku haja ya masomo akaona heri kudurusu ya dunia danguroni kuliko ya maktabani?
Wazazi wa binti huyu walilala wapi wakati mwanao akilala nje hata baada ya kujua kwamba wanafunzi walikwisha toka shule kwenda mapumzikoni?
Nawasihi kina baba kuamka walikolala na kulazia damu ya magogo. Amkeni kina baba! Mwana amekwisha toka kokani. Sasa ndio malezi yameanza! Vijanajike wa leo wamekwisha erevuka hata kabla ya nyonga kurefuka. Hakuna haja kujifanya vipofu tusioona ulimbukeni wa watoto hawa.
Wameanza kujua kwamba pembe za ndovu zina thamani! Tahadharini kabla hawajaambukizwa zinaa na kuhimilika wangali watoto. Chukueni hatua za dharura kabla mwana kubeba mwana na kuwa mzigo kwa familia na jamii.
Kina baba ndio kwanza waliofeli katika majukumu ya malezi. Vipi? Wameachia kina mama kusumbuka na kuteseka japo wanajua kwamba vijanajike wa leo werevu kuliko mama zao. Isitoshe, kina baba wenyewe wako kuko huko kutafuta na kutafuna vyao. Muda wa malezi wataupata wapi?
Tatizo kubwa ni kwamba wazazi wamewaacha vijanajike kutoga ndewe na kuremba nyuso kama kwamba wamekwisha kuwa wanawake walioradhi kuolewa.
Uso wa mwanafunzi wa shule ya upili utamfaa nini masomoni? Kwa mashungi ya nywele vijanajike wa leo wanadhani ndio kwanza wamekwisha kuwa magwiji tayari kutafuna dunia. Ukweli ni kwamba hawajui hata kufua kitambaa cha mkononi.
Ndio wao hao wanaovaa vitambaa mwilini kama njia ya kuiteka dunia. Wanaacha vifua wazi kama tumbili kwa kusudi dunia kufaidi malapulapu yao. Wanatalii miji na vijiji kuwatembelea marafiki na wafadhili badala ya kutulia chini masomoni.
Wanahudhuria kila aina ya sherehe vilabuni na nyumbani kwa majirani ilhali hawajui hata kupika sisemi kuandika meza. Mbona tuje lia ngoa wajapo kuhimilika wangali shuleni? Hatuna budi kukomesha huu mzaha wanaofanya vijanajike wa leo.
Ndio maana nawahimiza kina baba kuamka walikolazia damu. Wajibikeni kuzikomesha hizi tabia za kipuzi wanazofanya binti zenu. Kinaya ni kwamba wazazi wanalilia mustakabali wa watoto badala ya kumakinika kimalezi. Tusije sahau msingi wa tabia za mtoto ni mzazi.
Mtoto aliyefunzwa heshima na baba na mamake hawezi kamwe kujaribu ujahili na ujinga kama ule – mwana wa kike kulala danguroni na sare za shule! Siku zote hukumbuka kichapo cha mbwa kitakachomfika kwa kukaidi nyenzo nzuri.
Kina baba hawana budi kuelewa kwamba mtoto wa kike sharti kulelewa kama mtoto wa kike! Anahitaji mwongozo mwema, nasaha na mahitaji kukidhiwa angalau kumwepusha vishawishi vya dunia.
La sivyo, vijanajike hawa watazoea maisha ya ubwete – mwanamtu kutaka vya bure, tena maisha ya dezo! Ole nyinyi mnaowapa vijanajike uhuru kulala wanakotaka! Chungu kuvunjika dhiki kwa mfinyanzi. Huo ndio wajibu, tena ndio mawazo ya mwanamume kamili.