Makala

Mwanamume shupavu anayehamasisha umma kuhusu maswala ya hedhi

September 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na DIANA MUTHEU

KULINGANA na ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka wa 2018, wasichana 500 milioni ulimwenguni kote hawakuweza kupata vifaa vya kuwasaidia kuzingatia usafi wakati wa hedhi, na walilazimika kutumia matambara, majani, karatasi za chooni na hata blanketi.

Ripoti ya Wizara ya Afya nchini ya 2019 inasema kuwa swala la afya ya hedhi limebakia kuwa changamoto kwa wanawake na wasichana wa kipato cha chini.

“Ripoti za uchambuzi wa hali zinaonyesha kuwa wasichana wanakabiliwa na changamoto kila mwezi, na asilimia 58 ya wasichana vijijini na asilimia 53 ya wasichana katika maeneo ya mijini hawawezi kumudu usafi wakati wa hedhi,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.

Katika kaunti ya Mombasa, changamoto bado ni hizo hizo. Hata hivyo, mwanaume mmoja katika kaunti hiyo ameanza kampeni za kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kuipa swala la afya ya hedhi kipaumbele, kinyume na hali ya kawaida ambapo wanawake ndio huwa mstari wa mbele kupigia debe swaa hilo manake linawahusu.

James Atito, 28, anayejitambulisha kama “The Period Man” alisema kuwa swala la hedhi ni la jamii nzima, na wanaume wanafaa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wasichana na hata kina mama wanapata sodo za kutosha.

Hata amewahi kusafiriUbelgiji kuhutubia umati wa wanaume kuhusu maswala ya hedhi na wanachohitajika kufanya.

Bw Atito ni meneja wa maswala ya fedha katika shirika la kibinafsi la Stretchers Youth lakini pia ni mwanzilishi wa kampeni moja ya kuwahamasisha wanaume na jamii nzima kuhusu umuhimu wa kudumisha usafi wakati wa hedhi.

“Nilijitosa katika uwanja wa kuhamasisha jamii kuhusu kuwapa wasichana na kina mama visodo kwa kuwa kuna mashirika kadhaa yanayotoa msaada huo. Lakini tumeanza kuwanunulia sodo, karatasi za chooni na bidhaa zingine muhimu zinazohitajika, tukiwa katika mikutano na wasichana hao baada ya kugundua kuwa kuna wale ambao hawana uwezo wa kuzinunua,” akasema Bw Atito.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, kijana huyo alisema kuwa alijikabidhi jina la utani la “The Period Man” baada ya kutembelea kaunti ya Turkana kuhamasisha wasichana na wanawake kuhusu matumizi ya sodo spesheli zenye umbo la vikombe vinavyotumika wakati wa hedhi (menstrual cup).

“Baada ya kuzungumza na kundi hilo, msichana mmoja alinifuata na kuniuliza kama huwa napata hedhi! Mwanzo, nilicheka, lakini wiki kadhaa baadaye, niliamua kujiita jina hilo kwa kuwa hiyo ndiyo ajenda kuu katika hamasa zangu. Ningependa wanaume wawe mstari wa mbele kuyazungumzia mambo haya na pia kutafuta suluhu za kudumu,” akasema Bw Atito.

‘The Period Man’ akiwapa wasichana visodo. PICHA/ DIANA MUTHEU

Kijana huyu anasema kuwa ilikuwa ni ndoto yake kusomea udaktari lakini kabla ya kujiunga na chuo cha kutoa mafunzo hayo, alifadhiliwa kufanya kozi ya uhandisi katika Chuo cha Ufundi cha Mombasa (TUM).

“Katika mwaka wangu wa tatu chuoni, mfadhili wangu alipata changamoto kunilipia karo. Nilijaribu kufanya kazi kama vile kuchoma kachiri na mihogo, lakini sikuweza kupata fedha za kutosha kukamilisha masomo yangu, na mwaka wa 2014, niliacha masomo hayo na kujihusisha kikamilifu na shughuli katika shirika la Stretchers Youth,” akasema.

Mnamo Januari 2 mwaka huu, Bw Atito alianza kampeni yenye mada “Menforperiods365” katika mtandao wake wa Facebook, akilenga kuelimisha jamii haswa wanaume kuhusu afya wakati wa hedhi.

Katika kampeni hiyo ameweza kupata wafuasi zaidi ya 9,000 katika mtandao huo. Kila siku huwa anaandika ujumbe kuhusu maswala ya hedhi, zikiambatana na picha au video na pia amekuwa akiwauliza wafuasi wake watoe maoni yao kuhusu mada husika.

“Kupata maarifa kuhusu mada hii, nilianza kusoma vitabu, nikazungumza na wataalamu, nikatafuta maarifa zaidi mtandaoni na ripoti za mashirika kama vile Amref, Shirika la Afya Duniani (WHO), Wizara ya Afya,” alisema huku akiongeza kuwa kuna wakati huwa anahisi uvivu kuweka jumbe hizo, lakini wanaomfuatilia humtia moyo aendelee zaidi.

Kufikia Septemba 8, amefikisha siku 251 akiweka jumbe hizo. Lengo lake ni kuhamasisha watu kwa siku 365. PICHA/ DIANA MUTHEU

Pia, ameweza kuwafikia zaidi ya wasichana 500 katika kaunti ya Mombasa na kutoa msaada wa sodo, karatasi za chooni, chupi na sabuni.

Zaidi, ameweza kuwaelekeza wanawake wanne waliokuwa na magonjwa yanayohusiana na uzazi kwa wataalamu kutoka mashirika tofauti.

“Ni huzuni kusikia kina dada zetu wakijihusisha na shughuli kama vile ukahaba ili kupata fedha za kununua sodo. Pia, katika kaunti nyingi, baadhi ya wasichana wamepata mimba za mapema wakiwa katika shughuli za kutafuta bidhaa hizo muhimu kwa maisha ya wanawake,” akasema Bw Atito.

Baadhi ya changamoto ambazo amezitaja ni swala la unyanyapaa unaozingira swala nzima la hedhi na pia mazungumzo kulihusu kuwa mwiko katika jamii.

“Pia, kupata fedha za kununua sodo ni changamoto, imenilazimu nitenge fedha kutoka kwa biashara yangu ya bodaboda. Zaidi, baadhi ya watu katika jamii wamekuwa wakinidhihaki kuwa natafuta sifa na huruma kutoka kwa umma,” akasema.

Mwandani wake, Bw Evans Ouma alisema kuwa wanaume wengi hutengwa katika maswala kuhusu hedhi.

Alisema wanaume wakihusishwa, wataweza kuwaelewa wanawake zaidi na hivyo kuchukua jukumu la kuwalinda.

“Tutajaribu kuwajumuisha wanaume wengi katika kampeni na mikutano yetu. Wanaume wanafaa kuwa mstari wa mbele kuzungumzia swala hili ili kina dada zetu, kina mama na hata shangazi zetu waweze kusaidika,” akasema Bw Ouma huku akiongeza kuwa swala la hedhi linahusu jamii nzima, na wanaume wanafaa kuhusishwa ili kuziba pengo la usawa lililo baina ya jinsia mbili.

Angela Cecilia, 13 alishukuru kupata msaada wa sodo kupitia kampeni hiyo. PICHA/ DIANA MUTHEU

 

“Mamangu alipoteza kazi wakati janga la corona lilipotukumba, na hivyo tulipata changamoto kupata fedha za kununua chakula na hata sodo,” akasema Cecilia.

Mwenzake Beatrice Adhiambo alisema ameweza kujieleza anapopata shida wakati wa hedhi baada ya kuhudhuria mikutano kadhaa iliyofanywa na Bw Atito.

“Hata kama ni mwanaume, ameweza kutueleza mengi kuhusu hedhi ambayo hatukuwa tunayajua,” akasema Adhiambo.

Bw Atito alisema kuwa ameweza kushirikiana na mashirika kama vile Stretchers Youth, Afripads na mashirika mengine ya kijamii kuhamasisha umma na kutoa misaada ya bidhaa muhimu zinazotumika wakati wa hedhi.

Alisema kuwa baada ya kukamilisha kampeni hiyo ya siku 365 atakuwa ameweka msingi thabiti wa kufanya hamasa zingine.

“Mazungumzo kuhusu hedhi yasiwe mwiko kwani ni swala muhimu sana katika maisha ya mwanadamu yeyote kwa kuwa dada zetu wanapata hedhi, pia mama zetu walikosa hedhi na badala yake wakapata mimba ndipo wakatuzaa,” akasisitiza huku akisema changamoto wanazopitia baadhi ya wasichana na kina mama zinampa motisha wa kuendelea na programu hiyo.