MWANASIASA NGANGARI: Mlezi wa wanasiasa tajika Pwani
Na KENYA YEAR BOOK
TANGAZO la saa saba mchana la kitengo cha habari cha Rais kilichojulikana kama Presidential Press Unit la kufutwa kwa Robert Stanley Matano kama Waziri wa Habari na Mawasiliano mwaka wa 1985, lilimgonga katibu huyo mkuu wa chama cha Kanu kama dhoruba.
Matano, ambaye alikuwa njiani kutoka nyumbani kwake Mazeras, Pwani akitumia garimoshi, alishuka Nairobi na kupiga simu katika ofisi yake akitaka gari la kuhamisha bidhaa zake za kibinafsi kutoka nyumba ya serikali aliyokuwa akiishi.
Alikuwa amehudumu kwenye serikali za Kenyatta na Moi katika nyadhifa tofauti za uwaziri; Utamaduni, Huduma za Jamii na Makao, Vyama vya Ushirika na Maendeleo na Habari na Mawasiliano.
Alipofutwa kazi, alitulia hadi alipopoteza kiti chake cha ubunge 1988 kisha akastaafu na kuanza kilimo nyumbani kwake mashambani.
Matano alizaliwa Mazeras, Kaloleni mnamo 1925 na alisomea shule ya Mazeras Intermediate na kisha akajiunga na shule ya chama cha Wamishenari, Church Missionary Society, eneo la Kaloleni.
Alifanya vyema na akaitwa kujiunga na shule ya sekondari ya Kaaga, Meru na baadaye shule ya Alliance mwaka wa 1936.
Alikuwa mwanafunzi mwenye bidii na mtiifu. Na mwaka wa 1946, alijiunga na chuo cha Makerere aliposomea diploma ya masuala ya elimu na kufuzu 1948.
Mwaka wa 1949, alianza kazi ya kufunza katika shule ya Sekondari ya Ribe Boys Junior na baadaye Alliance. Alipandishwa cheo kuwa afisa wa elimu wa wilaya (DEO) Mombasa na Kwale.
Katika siasa, Matano alikuwa upande uliokuwa ukitaka mfumo wa utawala wa majimbo uliopingwa na chama cha Kanu kilichotaka serikali ya umoja wa kitaifa.
Matano alijiunga na siasa miaka ya 1960 baada ya kushawishiwa na Ronald Ngala.
Alikuwa katika ujumbe uliosafiri Lancaster 1960, 1961 na 1962. Kanu ilishinda uchaguzi wa 1963 na kuunda serikali baada ya uhuru na Kadu kikawa upinzani.
Lakini mwaka wa 1964, chama hicho kilivunjwa na wanachama wake, akiwemo Matano, aliyekuwa amechaguliwa mbunge wa Kinango, walijiunga na chama tawala.
Akiwa mbunge na waziri, mapenzi ya Matano kudumisha maadili yalifanya wanachama wengine wa chama kumchukulia kama limbukeni katika siasa. Lakini nyota yake ya kisiasa ilianza kung’aa alipokuwa Kanu, Mboya akiwa Katibu Mkuu.
Baada ya Mboya kuuawa 1969, Rais Kenyatta alimteua Matano kaimu katibu mkuu wa Kanu.
Lakini chama hakikuwa kimechangamka kilivyokuwa awali. Baada ya kongamano la Limuru mwaka wa 1966 ambao Odinga aliondoka kuunda chama cha KPU, Kanu hakikuandaa uchaguzi wa matawi madogo, matawi au uchaguzi wa kitaifa hadi 1979.
Kama sehemu ya mikakati yao ya kisiasa, Kenyatta na washauri wake walihisi kwamba uchaguzi wa chama ungegawanya nchi na kupanua mpasuko kati ya kambi tofauti katika chama tawala.
Chama hicho kilikuwa baridi hivi kwamba katibu mtendaji John Keen alimwandikia barua Kenyatta kulalamika kwamba wajumbe wa Kanu hawakuwa wamekutana tangu 1962, mwaka mmoja kabla ya uhuru.
Maafisa wakuu wa chama hawakuwa wamekutana tangu 1964. Chama kilikuwa na deni la pauni za Uingereza 20,000. Simu katika makao makuu zilikuwa zimekatwa kwa kutolipa bili. Wafanyakazi hawakuwa wamelipwa mishahara kwa miezi saba.
Kwa ufupi, Keen alionyesha kuwa kwa sababu chama hakikuwa kimekutana au kufanya uchaguzi, hakikuwa na nguvu.Kenyatta hakumsamehe Keen kwa hili.
Mbunge wa Butere Martin Shikuku alieleza bunge vivyo hivyo mwaka wa 1975. “Kanu kimekufa,” alisema. Lakini wakati mbunge mmoja alipomtaka kufafanua madai hayo, Spika wakati huo Jean-Marie Seroney, ambaye alikuwa mkosoaji wa serikali, alisema hakukuwa na sababu ya kufafanua “lililokuwa wazi”.
Muda mfupi baadaye, Shikuku na Seroney walikamatwa katika majengo ya bunge na kutupwa kizuizini.
Hii ilikuwa hali ya chama tawala ambacho Matano alihudumia akiwa kaimu katibu mkuu kati ya 1966 na 1979 alipothibitishwa kushikilia wadhifa huo mwaka mmoja baada ya kifo cha Kenyatta.
Akiwa mmoja wa maafisa wakuu wa chama cha Kanu, Matano alikuwa na wakati mngumu hasa wakati wa uchaguzi wa ubunge ambapo wawaniaji walilalamika kuwa walizuiwa au kukosa kuruhusiwa kugombea katika maeneobunge au wadi kwa sababu moja au nyingine.
Kisa kinachokumbukwa zaidi ni makabiliano na mwekahazina wa kitaifa wa Kanu, Justus ole Tipis, kuhusu kuidhinishwa kwa waliokuwa wanachama wa KPU, akiwemo Odinga, kugombea viti vya kisiasa 1979.
Matano na Tipis walipigana katika Ukumbi wa Kenyatta International Conference Centre, ambapo makao makuu ya Kanu yalikuwa.
Tipis, mwanasiasa mwenye hasira, alimgonga Matano kichwani kwa rungu.
Baada ya kupoteza kiti chake cha ubunge, Matano alisema angestaafu siasa akieleza kuwa mtu akiwa mwanasiasa hubakia kuwa mwanasiasa na akaamua kuchagua kuwa mshauri akihitajika.
Matano alikuwa mlezi wa wanasiasa wengi kutoka pwani wakiwemo Shariff Nassir na Noah Katana Ngala, mwana wa mwanzilishi wa chama cha Kadu Ronald Ngala.
Matano pia alikuwa mmoja wa waanzilishi wa chama cha Shirikisho Party of Kenya, ambacho wakati mmoja kiliongozwa na aliyekuwa mbunge wa Matuga na waziri Chirau Ali Mwakwere.
Ingawa Matano alistaafu siasa, alihudhuria mikutano ya wajumbe wa chama Mombasa na kuwahakikishia wanachama angepatikana kwa ushauri wa kisiasa wakati wowote wakimhitaji.
Matano aliwakilisha Kinango kwa miaka 27- kutoka 1961 hadi 1988 — wakati mwanasiasa aliyegombea kwa mara ya kwanza, Ali Bidu, alipomshinda kwenye uchaguzi wa kura ya mlolongo ambao Moi alikuwa ameanzisha. Uchaguzi huo ulikosolewa kote nchini na kimataifa kama usiofaa.
Matano anasifiwa kwa kutekeleza wajibu muhimu kupigania siasa za vyama vingi. Akiwa aliyeongoza Kanu kilipokuwa chama cha kipekee, alibaini vyema kilipotumiwa kuangamiza maisha ya kisiasa ya viongozi wengi.
Kwake, kuwa na vyama vingi hakungerejeshea watu haki zao za kujieleza na kujumuika lakini pia kungewapa nafasi ya kujiunga na mirengo ya siasa wanayotaka na kuleta kuvumiliana kisiasa.
Matano hakujijengea sifa kama kiongozi wa eneo lake au kiongozi wa kitaifa.
Hakuna mradi ambao anaweza kuhusishwa nao.
Hata hivyo, kitu kimoja ambacho anakumbukwa nacho ni kubuni chama cha Shirikisho Party. Lakini chama hicho bado hakina umaarufu kitaifa au hata eneo la pwani.
Wanasiasa kama Shariff Nassir, Darius Mbela na Karisa Maitha, ambao walijiunga na siasa miongo mingi baada yake waliacha kumbukumbu eneo la pwani na kitaifa.
Viongozi wa eneo hilo na wanasiasa hawakumbuki ikiwa Matano alikuwa na ajenda za kijamii, kiuchumi au kisiasa za eneo la pwani.
Maoni ya wengi ni kuwa, ingawa alishikilia nyadhifa kuu serikalini, hakutumia nguvu zake kushawishi eneo lake la Kinango kupata maendeleo ya kijamii au kiuchumi au hata kujipatia utajiri wake binafsi.
Kinango, ambalo ni eneo kame na lililo na viwango vya juu vya umasikini halina miradi ya maana ya maendeleo ambayo inaweza kuhusishwa na Matano.
Aliyekuwa waziri Suleiman Shakombo anamtaja Matano kama mwanasiasa mpole aliyechukia ufisadi na maovu mengine. “Matano alikuwa mwanamume msafi,” alisema Shakombo, ambaye alikuwa waziri kati ya 2005 na 2007.
Mtumishi wa umma ambaye alifanya kazi na Matano jijini Nairobi anasema kwamba hakutumia ushawishi wake kupatia watoto na jamaa zake kazi serikalini.
Alipokufa akiwa masikini hoe hae, waliomuomboleza walilaumu serikali kwa kumtelekeza.
Aliyekuwa waziri Katana Ngala alimtaja kama mtu aliyeshirikiana vyema na watu, aliyeepuka mizozo.
Aliyekuwa mbunge wa Bahari, Joe Khamisi alimtaja kama kiongozi mtulivu aliyetaka kufanya kazi bila kujitangaza.
Katibu mkuu wa chama cha Shirikisho, Yussuf Abubakar alisema waziri huyo wa zamani aliwahimiza wabunge wa eneo la Pwani kuunga chama hicho.
Lakini wakosoaji wa Matano wanamlaumu kwa kushindwa kupigania wasio na mashamba na kuwalinda dhidi ya kubaguliwa wakati wa kugawa kwa rasilimali za eneo hilo.
Kuna madai kwamba Matano hakusema lolote kuhusu kuporomoka kwa viwanda eneo la Pwani kama kiwanda cha sukari cha Ramisi na kiwanda cha Korosho ambavyo vilikuwa tegemeo la maelfu ya wakazi wa Kwale na Kilifi.
Lakini Khamisi anatofautiana na wakosoaji hao akisema baada ya kufutwa kazi, Matano alikubali hali yake na kutulia katika shamba lake eneo la Kinango.
Hakuweza kumudu gharama ya kusafirisha bidhaa zake za nyumbani hadi Mazeras alipolazimishwa kuhama nyumba ya serikali jijini Nairobi.
Matano aliacha wajane wawili Ruth na Susan, watoto 16 na wajukuu 20.
Katika siku zake za mwisho alikuwa akiishi katika kijiji cha nyumbani mashambani cha Ndugu ni Mkono, Mazeras na alikufa 2008 akitibiwa katika hospitali ya Mombasa alikopelekwa baada ya kuugua. Alikuwa na umri wa miaka 83.