• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 9:50 AM
MWANASIASA NGANGARI: Nabwera: Uanadiplomasia ulimzuia kutofautisha kazi ya Kanu na ya Serikali

MWANASIASA NGANGARI: Nabwera: Uanadiplomasia ulimzuia kutofautisha kazi ya Kanu na ya Serikali

Na KENYA YEARBOOK BOARD

YAMKINI Burudi Nabwera alikuwa mmoja wa wanasiasa nchini waliopata kisomo cha kiwango cha juu katika vyuo vya Uingereza katika enzi ya ukoloni.

Na kwa sababu hii alifahamu barabara mfumo wa kiuchumi wa kibepari katika mataifa ya Kimagharibi na Usoshiolisti uliokumbatiwa na mataifa ya Mashariki.

Hii ndio maana baada ya Kenya kupata uhuru, Rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta alimteua Bw Burudi kuwa balozi wa Kenya nchini Amerika.

Na chini ya utawala wa Rais wa pili Daniel Moi, alihudumu katika nyadhifa mbalimbali serikalini na hatimaye akateuliwa kuwa Waziri katika Afisi ya Rais. Vilevile, aliwahi kuhudumu kama Katibu Mkuu chini ya utawala wa chama kimoja cha kisiasa.

Kimsingi, kwa kumteua katika Nabwera katika nyadhifa hizo mbili, nyakati tofauti katika utawala wake, Moi alikuwa akipania kutumia tajriba yake pana katika mawanda ya siasa, uongozi na diplomasia.

Nabwera alizaliwa mnamo 1924 na akasomea katika Shule ya Upili ya Kitaifa ya Maseno, Chuo Kikuu cha Makerere Uganda kabla ya kusomea shahada ya uzamili katika Chuo cha London School of Economics.

Ni katika shule ya upili ya Maseno ambapo alikutana aliyekuwa Makamu wa Rais Jaramogi Oginga Odinga. Wanasiasa wengine waliokuwa wanafunzi katika shule hiyo ya hadhi, na ambao Nabwera alisoma nao, ni; Masinde Muliro, Wycliffe Wasia Awori ambaye baadaye alikuwa mjumbe wa Kenya katika bunge la Legco nchini Uingereza akitetea uhuru wa Kenya.

Na Nabwera alipojiunga na chuo kikuu cha Makerere, alikutana na wasomi mashuhuri kama vile Bethwel Allan Ogot, Thomas Odhiambo, Josephat Karanja (aliyehudumu kama makamu wa rais kwa kipindi kifupi katika utawala wa Moi. Baadaye Rais Mstaafu Mwai Kibaki pia alijiunga na chuo hicho kwa masomo ya juu.

Kwa mujibu wa kitabu ambacho Nabwera aliandika chini ya kichwa, “How it Happened” utangamano wake na watu kama hawa ulimfaidi zaidi katika maisha yake ya siku za usoni, kama mtumishi wa umma na hatimaye kama mwanasiasa.

Alimsaidia sana Rais Moi kwa kushirikiana vizuri na aliyekuwa Waziri Moses Mudamba Mudavadi kuwadhibiti kisiasa wabunge wabishani nyakati hizo, kutoka magharibi mwa Kenya, Martin Shikuku (Butere), Lawrence Sifuna (Bungoma Kusini) na waziri Elijah Mwangale ambaye yeye (Moi) hakumwamini.

Katika chama cha Kanu, kwa ushirikiano wa David Okiki Amayo kama mwenyekiti na Nabwera kama Katibu Mkuu wa tatu, waliweza kutisha kuwatimua wanasiasa waasi ndani ya Kanu. Sera na maongozi ya Kanu yaliendeshwa kwa njia ya kidikteta.

Lakini licha ya umaarufu wa Nabwera ndani ya Kanu, kwa kuwatisha wakosoaji wake kila mara, mnamo 1986 alichochea hasira ndani ya Kanu kwa kutoa matamshi ambayo yalikuwa mwiko kutolewa mwaka huo.

Alitangaza kupitia runinga ya Sauti ya Kenya (sasa KBC) kwamba chama hicho tawala kingewasamehe kundi la wanasiasa ambao walikuwa washirika wa aliyekuwa Mkuu wa Sheria Charles Njonjo, na ambao walikuwa wamefurushwa kutoka chama hicho.

Nyakati hizo ilikuwa ni mwiko kwa afisa yeyote wa Kanu, hata kutafakari kuwasamehe wanasiasa ambao walikuwa wamefurushwa chamani kutoka na ushirikiano nao na Njonjo.

Moi alikuwa amemwelekezea Njonjo kidole cha lawama kwa kushirikiana na taifa moja la kigeni kujaribu kuipindua serikali.

Taarifa ya Nabwera kwamba “Watu wa Njonjo” wasamehewe, iliwakasirisha vigogo wa Kanu.

Na baada ya muda alipokonywa cheo cha Katibu Mkuu wa Kanu na kikapewa Moses Mudavadi.

Na hii ndio maana baadaye katika kitabu chake Nabwera anauliza maswali ya balagha hivi: Mbona Kanu ambayo imeongoza kwa takriban nusu karne, haiwezi kuona dalili kwamba inapoteza mamlaka?

Mbona Kanu isijikaze kurejesha sifa zake. Mbona vyama vya kisiasa visiweke nidhamu miongoni mwa wanachama jinsi alivyofanya akiwa Katibu Mkuu.

Mapema, alipohudumu kama Waziri katika Afisi ya Rais, Nabwera alikuwa na ushawishi mkubwa zaidi ya Katibu Mkuu wa Kanu. Katika wadhifa huu (wa uwaziri), Nabwera alikuwa mmoja wa mawaziri wenye ushawishi mkubwa katika utawala wa Moi.

Wafanyabiashara, wanasiasa na watu wanaosaka kazi wangefurika afisini mwake katika Jumba la Harambee kumsihi “apeleke maombi yao katika Ikulu.

Kosa la Nabwera ni kwamba hakuweza kutofautisha kati ya shughuli za serikali na zile za chama.

Ushindi wake katika uchaguzi wa ubunge wa Lugari mnamo 1988, kupitia kura ya mlolongo ulimfanya kutotofautisha kati ya masuala ya chama na yale ya serikali. Aligombea ubunge kwa mara ya kwanza mnamo 1979 katika eneobunge la lililokuwa eneobunge la Lurambi Kaskazini.

Nabwera alitumia muda wake mwingi kumtetea bosi wake, Moi, na chama cha Kanu na akasahau wapigakura wake wa Lugari.

Hii ndio maana katika uchaguzi mkuu wa 1992 aliangushwa na mwanasiasa limbukeni Apili Wawire.

Lakini itakumbukwa kwamba kabla ya Nabwera kuondoka bungeni, alihudumu kama Waziri wa Habari na Utangazaji ambapo aliendelea kuvumisha sifa za Kanu.

Akihudumu katika wizara hiyo, ilitekeleza mageuzi katika mashirika ya habari ambayo yalitumika kuvumisha sifa za Kanu kuelekea uchaguzi mkuu wa 1992, baada ya mfumo wa utawala wa vyama vingi kurejeshwa nchini.

Kwa mfano, alifuta kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Habari Nchini (KBC) James Kangwana, pamoja na wanachama wa bodi yake, kupitia tangazo kwenye gazeti rasmi la serikali. Nafasi aliwapa watu ambao waliaminika kuwa waaminifu kwa Kanu.

Kwa bidii na ukakamavu huo, Nabwera aliisuta Benki ya Dunia (WB) kuwa kuiwekea Kenya masharti magumu ya kiuchumi.

Kwa mfano, alitaja matakwa ya benki hiyo kwamba idadi ya vyuo vikuu ipunguzwe kama ambayo haingeweza kutekelezwa.

Nabwera ambaye alimuoa Bi Tabitha, mnamo 1958 atakumbukwa kama mwanadiplomasia na mwanasiasa aliyetekeleza mengi nchini chini ya serikali za Mzee Kenyatta na Moi.

 

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board, kenyayearbook.co.ke

You can share this post!

AKILIMALI: Alitambua kipaji chake katika ususi akiwa shuleni

KINAYA: Jubilee si lolote si chochote

adminleo