Makala

MWANASIASA NGANGARI: Uhasama wa Jomo, Jaramogi ulifanya Okero awike kisiasa

November 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 5

Na KEYB

MAISHA ya kisiasa ya Isaac Edwin Omolo Okero aliyekuwa waziri na mbunge wa Gem wilayani Siaya, kati ya 1969 na 1979, yalikuwa ya kupigiwa mfano.

Alihudumu katika wizara mbalimbali wakati wa utawala wa Mzee Jomo Kenyatta kati ya 1969 na 1978.

Okero aliteuliwa kama Waziri wa Kawi na Mawasiliano kati ya 1978 na 1979 wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Daniel arap Moi.

Aliaminika kuwa miongoni mwa wanasiasa wenye busara ambaye alifanya maamuzi yasiyokuwa na dosari katika ulingo wa kisiasa.

Sifa hizo zilimfanya kunawiri katika uga wa kisiasa.

Okero alijiunga na siasa akiwa na umri wa miaka 40.

Kabla ya Okero, wanasiasa wengine waliowahi kuwa wabunge wa Gem ni Wasonga Sijeyo ambaye alikuwa mfuasi sugu wa Oginga Odinga, na C.M.G. Argwings-Kodhek.

Sijeyo alikuwa mbunge kwa miezi michache kabla ya kukamatwa na kuzuiliwa kwa kuwa mwanachama wa wa KPU.

Okero, aliyejulikana kwa jina la majazi “The Barrister”, alizaliwa mnamo Julai 28, 1929, kijijini Ulumbi, Gem, karibu na mji wa Yala.

Sawa na watoto wengine, aliwasaidia wazazi wake kulima shambani, kutafuta kuni na kuchunga mifugo.

Okero alisomea katika shule ya Msingi ya Ulumbi na Uranga.

Aliishi karibu na nyumbani kwa Chifu Odera Akang’o, aliyechapa viboko watoto waliokwepa kwenda shuleni.

“Wakati huo, elimu ilikuwa muhimu sana, bila elimu hukuwa mtu,” anasimulia.

Baada ya kukamilisha elimu ya msingi, alijiunga na shule ya Upili ya Ambira ambayo mkuu wake alikuwa Mark Wellington Ombaka, baba ya aliyekuwa mbunge wa Gem baadaye, Oki Ooko Ombaka.

Mark Wellington Ombaka alikuwa mtu wa kwanza kutoka Gem kujiunga na Chuo cha Makerere na Mwafrika wa kwanza kuwa mkuu wa Shule ya Upili ya Ambira.

Shuleni Ambira, Okero alisoma pamoja na Bethwel Ogot, ambaye sasa ni Profesa wa Historia na aliyekuwa Chansela wa Chuo Kikuu cha Maseno.

Kati ya 1946 na 1947, Okero na Ogot walijiunga na Shule ya Maseno ambapo walisomea elimu ya sekondari ya chini kwa miaka mwili.

Shuleni Maseno, wanafunzi wenzake darasani walikuwa watu ambao baadaye walikuwa wanasiasa watajika kama vile Ayodo, Odero Jowi, Burudi Nabwera, Edward Khashahala na Thomas Odhiambo (mwanasayansi ambaye baadaye alianzisha Taasisi ya Utafiti ya ICIPE).

Utukutu wa Okero, hata hivyo, ulisababisha mkuu wa shule ya Maseno kumhamishia Shule ya Upili ya Alliance, Kikuyu mnamo 1948 kuendelea na masomo ya Elimu ya Sekondari ya Juu.

Shuleni Alliance (1948-1949), wanafunzi wenzake walikuwa Geoffrey Kareithi (ambaye baadaye alikuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma), James Mugo Waiyaki na Cyrus Muthiga.

Mnamo 1949, Okero alifanya vyema mtihani na kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere mnamo 1950 ambapo alikuwa mtu wa tatu kutoka kijijini Ulumbi kujiunga na taasisi hiyo ya nchini Uganda.

Wengine kutoka kijijini Ulumbi waliokuwa wamewahi kusomea katika taasisi hiyo ni Mzee Ombaka na Owiti Mudhune.

Alisomea chuoni Makerere wakati mmoja na Rais Mstaafu Mwai Kibaki na aliyekuwa Karani wa Jiji la Nairobi James Gitonga, aliyejiunga na taasisi hiyo mnamo 1951.

Agosti 1952, Okero aliongoza wanafunzi kufanya maandamano na alitimuliwa kutoka chuoni Makerere. Josephat Karanja — ambaye baadaye alikuwa Makamu wa Rais wa Kenya — pia alitimuliwa kutoka Makerere.

Mnamo 1953 alipata ufadhili wa masomo kutoka kwa serikali ya India, kupitia balozi wake humu nchini, Apa B. Pant, ambapo alienda kusomea sheria katika Chuo Kikuu cha Bombay. Alihitimu mnamo 1956.

Akiwa nchini India, alishirikiana na Polycarp Akoko na kurekodi nyimbo nne za kupongeza wanasiasa waliopigania ukombozi, akiwemo Walter Odede.

Wakati huo, vita vya Mau Mau vilikuwa vimechacha na serikali ya wakoloni ilipiga marufuku nyimbo hizo nne.

Mwaka mmoja baadaye, aliajiriwa kuwa katibu mshirikishi wa Chama cha Wanafunzi cha Kimataifa mjini Leiden, Uswisi ambapo alifanya kazi hadi 1959.

Okero, akiwa nchini Uswisi alifanikiwa kusafiri katika mataifa mbalimbali ya Ulaya na Asia hivyo alifahamu hali halisi ya maisha katika mataifa yaliyostawi kiuchumi na nchi maskini.

Mnamo Februari 1959, alielekea London na kujiunga na chuo cha uwakili cha Middle Temple. Chuoni hapo alikutana na Jaji A. B. Shah, ambaye baadaye alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa. Okero alihitimu na aliidhinishwa na serikali ya wakoloni kuwa wakili. Alijiriwa kuwa wakili wa serikali ya Kenya katika afisi ya Mkuu wa Sheria.

Siku chache kabla ya Kenya kupata uhuru wake mnamo 1963, Charles Njonjo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Sheria huku Tom Mboya akiwa waziri wa Haki.

Okero alikuwa akimezea mate wadhifa wa Naibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, lakini nafasi hiyo ilipewa Clive Brooks. Alituma maombi na kuteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Forodha ambayo makao makuu yake yalikuwa Mombasa.

Mnamo 1969, alijiuzulu kutoka wadhifa huo na kufungua kampuni yake ya kutoa huduma za sheria mjini Kisumu.

Lakini mambo yalibadilika ghafla siku chache baadaye kufuatia misukosuko iliyokumba jamii ya Wajaluo.

Waziri Kodhek alifariki mnamo Februari mwaka huo na Tom Mboya akaaga dunia miezi mitano baadaye. Chama cha Odinga cha KPU pia kilipigwa marufuku nchini.

Baada ya kifo cha Kodhek, Mwafrika wa kwanza kuwa wakili nchini Kenya, wakazi wa Gem walisisitiza kuwa walitaka wakili mwingine kuwa mbunge wao.

Okero anasema: “Nilishinikizwa kuwania hatimaye nikaamua kujitosa katika siasa.”

Alitafuta tiketi ya chama cha Kanu, lakini akanyimwa. Chama cha Kanu kilimkabidhi tiketi Wycliffe Rading Omolo. Lakini wakazi wa Gem walionekana kutoridhishwa na mwaniaji huyo wa Kanu.

Rais Kenyatta aliagiza mawaziri kumsaidia Rading kuendesha kampeni.

Juhudi za serikali ziliambulia patupu kwani wakazi wa Gem walimchagua Sijeyo aliyewania kiti hicho kupitia chama cha KPU.

Uhasama wa kisiasa baina ya Mzee Kenyatta na Odinga ulimpatia nafasi wakili huyo kijana nafasi ya kukita mizizi katika siasa.

Kenyatta alianza operesheni ya kuwafurusha wandani wa Odinga kutoka serikalini. Baadaye chama cha KPU kilipigwa marufuku na viongozi wake kuzuiliwa mnamo 1969 kufuatia maandamano makali mjini Kisumu.

Chaguzi ndogo ziliandaliwa katika maeneobunge ambapo wabunge wake walikuwa wamezuiliwa.

Wakati huo chama cha Kanu ndicho kilikuwa cha pekee. Waliotaka wadhifa wa kisiasa walitakiwa kuwania kupitia chama cha Kanu.

Okero aliwania ubunge wa Gem na akawa mbunge wake wa tatu. Aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya. Wengine walionufaika kutokana na uhasama baina ya Kenyatta na Odinga ni: Odongo Omamo (Bondo), Matthew Ogutu (Ugenya), Peter Okudo (Alego-Usonga), Grace Onyango (Kisumu), Denis Akumu (Nyakach), David Okiki Amayo (Karachuonyo) na Lawrence Oguda (Migori).

Mnamo 1973, Okero alihamishiwa wizara ya Afya, Kawi na Mawasiliano.

Alichaguliwa tena mnamo 1974 ana akateuliwa tena kuwa Waziri wa Kawi na Mawasiliano.

Hali ya kisiasa katika eneo la Nyanza ilibadilika baada ya kuachiliwa huru kwa baadhi ya waliokuwa wakizuiliwa; Odinga na Luke Obok.

Katika uchaguzi wa 1974, Okero ndiye alinusurika huku wenzake kama vile aliyekuwa waziri Omamo wakibwagwa.

Omamo alibwagwa na Ougo Ochieng aliyekuwa akiungwa mkono na Odinga.

Mnamo 1977, Okero alihamishiwa katika wizara ya Habari.

Mnamo 1978, Kenyatta alifariki na Moi akaapishwa kuwa rais.

Moi alifanyia mabadiliko Baraza la Mwaziri na kumrejesha Okero katika Wizara ya Kawi na Mawasiliano ambapo alihudumu hadi mwishoni mwa muhula wake wa pili.

Kulingana na waziri huyo wa zamani, Mzee Kenyatta hakupenda umbea. Anasema ilikuwa vigumu kumfikia Mzee Kenyatta katika siku za mwisho za uhai wake.

Katika uchaguzi wa 1979, Okero alibwagwa na Aggrey Otieno Ambala huku kukiwa na madai ya kuibiwa kwa kura.

“Kuwa kwangu waziri na mbunge kwa muongo mmoja kumenifunza kwamba ukiwa kiongozi mwenye msimamo unakuwa na maadui wengi,” anasema.

Baada ya kukaa nje ya siasa kwa miaka 10, Okero aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati iliyochunguza kiini cha Shirika la Ndege nchini kupata hasara.

Mapendekezo ya kamati hiyo ilisababisha Rais Moi kusambaratisha bodi ya Kenya Airways iliyokuwa ikiongozwa na B.M. Gecaga na kubuni bodi mpya chini ya usimamizi wa Philip Ndegwa.

Okero ni mume wa Jane Margaret Anyango aliyefariki Septemba mwaka jana, na ana watoto sita; wa kiume wanne na wawili wa kike.

 

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke