MWANASIASA NGANGARI: Waziri aliyezindua huduma ya simu za mkono nchini
Na KENYA YEARBOOK BOARD
CHRIS Mogere Obure alikuwa mmoja wa mawaziri waliohudumu kwa muda mrefu tangu 1984 alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa waziri msaidizi wa Wizara ya Leba chini ya Robert Ouko aliyekuwa waziri wake katika wizara hiyo.
Maisha yake ya kisiasa yalianza 1969 alipogombea kiti cha ubunge cha Bomachoge Bassi lakini akashindwa.
Alishindwa tena 1979 lakini akashinda kwenye uchaguzi mkuu wa 1983 na mwaka uliofuata aliteuliwa waziri msaidizi.
Kwenye uchaguzi wa mlolongo uliotumiwa katika uchaguzi mkuu wa 1988, alishinda kiti cha ubunge cha eneo la Bobasi eneo la Bomachoge Bassi lilipogawanywa mara mbili.
Alihamishiwa wizara ya mashauri ya nchi za kigeni na ushirikiano wa kimataifa ambapo alihudumu chini ya Ouko kabla ya waziri huyo kuuawa 1990.
Mwaka wa 1992, Obure hakugombea baada ya chama tawala cha KANU kuagiza uteuzi wa eneobunge la Bobasi urudiwe. Nafasi yake ilichukuliwa na Stephen Manoti.
Hata hivyo, alirudi tena bungeni 1997 na akateuliwa waziri msaidizi katika wizara ya uchukuzi na mawasiliano.
“Changamoto kuu wakati huo ilikuwa ni kuzindua huduma za simu za mkono Kenya. Waziri William ole Ntimama aliniteua kusimamia jopokazi lililoshirikisha wataalamu kutoka shirika la Kenya Posts and Telecommunications Corporation, Ofisi ya Rais na wizara. Tulizuru nchi tofauti za ng’ambo kutafuta wawezekezaji wanaofaa na hatimaye tulipata mshirika ambaye ni kampuni ya Vodafone,” alisema.
“Shida ilikuwa, tulikuwa tukifikiria idadi ndogo sana. Tulikuwa tukitafuta simu 600 ambazo zilikuwa mara mbili ya watu waliokuwa na simu za kawaida. Wawekezaji walikataa katakata wakitaka tuongeze idadi hadi simu milioni moja. Kwa wakati huu kuna zaidi ya simu 30 milioni zilizosajiliwa Kenya. Hatukufikiria mahitaji yangeongezeka haraka kwa sababu ilikuwa ghali mno kwa mtu kununua simu yake binafsi (simu ya mkono). Mambo yamebadilika,” alisema.
Mwaka wa 1990, aliteuliwa waziri wa viwanda na baada ya muda mfupi alihamishiwa wizara ya vyama cha ushirika katika wadhifa kama huo.
Kufuatia mageuzi katika wizara ambapo zilipunguzwa hadi 15, aliteuliwa waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo alisema alifanya mabadiliko yaliyoinua baadhi ya sekta katika wizara hiyo.
Katika mabadiliko ya baraza la mawaziri ambayo Moi alifanya mwaka wa 2001, Obure alihamishiwa wizara ya mashauri ya nchi za kigeni na ushirikiano wa kimataifa ambapo alihudumu kwa chini ya mwaka mmoja kabla ya kuhamishiwa wizara ya fedha.
“Mwaka wa 2002, tulikuwa na mageuzi mengi. Ulikuwa mwaka mgumu sana. Kulikuwa na mabadiliko mengi katika ulingo wa kisiasa na yalitupatia shida nyingi. Uchumi ulikuwa umedorora vibaya kwa sababu ya hali ya siasa na kwa hivyo mapato kutoka kwa kodi yalikuwa ya chini. Wafadhili hawakuwa wakitupatia mikopo; sijui tulivyoweza kuishi. Lakini kama waziri wa Fedha nilikuwa na jukumu la kuhakikisha uchumi haukuporomoka,” alisema Obure.
Kwenye uchaguzi wa mwaka huo chama cha KANU ambacho kilikuwa kimemteua Uhuru Kenyatta kuwa mgombeaji wake wa urais, kilishindwa na muungano wa upinzani, National Rainbow Alliance, ambao ulikuwa ukiongozwa na Raila Odinga.
Baadhi ya wanachama wa muungano huo walikuwa wanasiasa waliohama chama tawala cha Kanu.
Obure alizaliwa Septemba 1943. Alianza masomo yake katika shule ya msingi ya Kereri iliyoko Bobasi.
“Nilikuwa nikitembea kwa miguu umbali wa kilomita 12 kwenda na kutoka Shule ya Msingi ya Kereri kila siku kwa miaka minane. Ulikuwa wakati mgumu sana. Njia zilikuwa mbaya na wakati mwingi kulikuwa na mvua. Kile ambacho mazingira hayo kilikufanyia, ilikuwa ni kukufanya uongeze juhudi zako. Yalikufanya utie bidii ili ufanikiwe,” alisema.
Baada ya kukamilisha masomo ya shule ya msingi, Obure alijiunga na shule ya Sekondari ya Kamagambo SDA, South Nyanza kwa masomo zaidi na baadaye aliajiriwa kama mwalimu asiyehitimu katika shule ya msingi ya Riosiri, South Mugirango eneo linalofahamika kwa wakati huu kama kaunti ndogo ya Gucha.
Wakati huo, serikali ilikuwa imeanzisha masomo ya juu katika kidato cha tano na cha sita , kwa hivyo, Obure aliacha kazi yake ya kufunza na kujiunga na shule ya Kisii High School kwa masomo hayo yaliyofahamika kama A level.
“Nilipata vifaa bora zaidi na walimu waliokuwa wamehitimu na waliokuwa wamejitolea na kwa hivyo nilikamilisha masomo ya kidato cha tano na sita kwa muda wa mwaka mmoja badala ya miaka miwili. Nilifanya hivi kwa kufanya mtihani wa London GCSE (A Level),” alisema. Alijiunga na chuo kikuu cha Nairobi mwaka huo, 1965, kusomea digrii katika masuala ya biashara.
Akiwa chuoni alianza kuchangamkia siasa na akachaguliwa makamu rais na waziri wa masuala ya chuo katika chama cha wanafunzi. Horace Ongili Owiti, aliyekuwa mbunge wa Gem ndiye alikuwa rais wa chama hicho.
“Wakati huo, vita baridi vilikuwa vimeshika kasi na wanafunzi wakawa baadhi ya makundi yaliyolengwa. Tulialikwa kuzuru USSR (Jamhuri ya Muungano wa Kisosholisti wa Urusi” na nchi nyingine za mashariki mwa bara Ulaya. Tulikutana na viongozi wengi wa wanafunzi. Ulikuwa wakati mzuri sana,” Obure alifichua.
Akiwa chuo kikuu, Obure alisomea kozi moja ya kitaalamu iliyofunzwa na Chartered Institute of Secretaries and Administrators kutoka Uingereza, ambayo baadaye ilichangia pakubwa kumjenga kitaaluma.
“Wakati huo, idadi ya wanafunzi ilikuwa ndogo sana na tulikuwa tuking’ang’aniwa na asasi tofauti ikiwemo serikali. Kulikuwa na nafasi nyingi za kazi nilizoitiwa lakini niliamua kufanya kazi na kampuni ya East African Bata Shoe Company.
Kampuni hiyo iliniandaa kwa miaka minne katika mpango iliyotaka niende Uingereza, lakini tayari nilikuwa nimefanya kozi. Walikuwa wakifunza Wakenya kuchukua nafasi za wataalamu waliokuwa wakiondoka. Kwa hivyo, muda wangu wa miaka wa kusubiri ulipunguzwa hadi miaka miwili. Niliteuliwa karani wa kampuni hiyo mwaka wa 1970,” alieleza mwanasiasa huyo.
Obure anasema kwamba alifanya kazi katika kampuni hiyo ya viatu hadi June 1984 alipokubali kazi kama hiyo katika kampuni ya Kenya Breweries Limited (KBL). Baada ya kuhudumu kwa miaka miwili aliteuliwa kuwa karani East African Breweries Ltd (Group Company Secretary) lakini akadumisha kazi yake katika Kenya Breweries. Mwaka wa 1982, aliteuliwa mkurugenzi wa KBL.
Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board, kenyayearbook.co.ke