• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 10:55 AM
MWANASIASA NGANGARI: Waziri Otiende alivyoweka msingi wa elimu

MWANASIASA NGANGARI: Waziri Otiende alivyoweka msingi wa elimu

Na KEYB

WAKATI chama cha Kenya African Union (KAU) kilipobuniwa miaka ya 1940, Otiende alikuwa mmoja wa wasomi waliotoa ushauri ambao ulitumiwa na vyama vingine vya kisiasa baadaye.

Licha ya amri walimu wasishiriki siasa, Otiende alikubali kuwa mwenyekiti wa chama hicho eneo la Nyanza Local Native Council.

Kama angegunduliwa, angepoteza kazi yake. Hata hivyo, alihisi kwamba lilikuwa jukumu lake kutumia maarifa na tajiriba aliyokuwa amepata katika vita vya ukombozi.

“Maoni yetu yalikuwa haya: Ikiwa hatungeshiriki siasa, nani angefanya hivyo?” anasema.

Ingawa alijaribu kuficha vitendo vyake vya kisiasa akiwa shuleni, majasusi wa wakoloni walifahamu kuhusika kwake na mara kwa mara alisumbuliwa na wasimamizi wa shule.

Alijitokeza hadharani na kuzuru kote nchini akiwa na viongozi wengine wa KAU. Hata hivyo haikuwa rahisi: “Kwa sababu KAU haikuwa na pesa za kufadhili shughuli za kisiasa, tulitumia pesa zetu na kugharimia safari na mahitaji yetu tukizuru maeneo tofauti nchini kuunganisha jamii, lakini ari ya kutaka kukomboa nchi iliwafanya watu wachange,” alisema.

Shule aliyotumwa kufunza kutoka Alliance ni Jeans School, kwa sasa Kenya Institute of Administration (KIA), Kabete mwishoni mwa miaka ya 1940s.

Jean School ilianzishwa kama kituo cha kuwashauri Waafrika waliopigana Vita vya Pili vya Dunia. Mmoja wa wanafunzi wake katika shule hiyo alikuwa Moses Mudavadi, baba ya Musalia Mudavadi.

Baadaye Moses Mudavadi aliwakilisha eneobunge la Vihiga kwa miaka 30. Ikiwa Alliance ilichangia Otiende kujiunga na siasa, basi Jeans School ilimfanya kuwa mpiganiaji uhuru.

Alijifunza mengi kutoka kwa wanajeshi waliopigania Uingereza ambao walikuwa wanafunzi wake.

Mwaka wa 1950, aliteuliwa katibu mkuu wa KAU na akashirikiana kwa karibu na Gichuru, ambaye alikuwa mwenyekiti wa chama hicho na rafiki yake.

Otiende alianzisha gazeti la Sauti ya Mwafrika, lililopigania uhuru. “Tulianzisha gazeti hilo ili kufikia watu wengi na kuvuka vizingiti vya watu kutotembea maeneo tofauti vilivyowekwa na wakoloni,” alisema.

Maumau ilianzishwa eneo la Kati ya Kenya na ikawa inashirikiana na KAU. Serikali ya Wakoloni ilitangaza hali ya hatari 1952 wito wa Waafrika kutwaa silaha kupigania uhuru wao ulipozidi na ikazidisha ukatili dhidi ya Waafrika.

Mnamo Oktoba 20, amri za kikatili zilizidishwa na KAU ikapigwa marufuku. Otiende na maafisa wengine wa KAU walianza kutumia mikakati rasmi na isiyo rasmi wakihimiza serikali ya wakoloni kuwapatia Waafrika haki ya kuwa na vyama vya kisiasa na wakati huo huo wakihimiza wapiganaji wa Mau Mau kuendeleza vita.

Otiende alifahamu kuwa hangejificha kutoka kwa serikali ya wakoloni milele. Lakini hakutarajia kukamatwa kwake Oktoba 1952.

Alikuwa amesafiri mashambani kuhudhuria mazishi ya jamaa yake wakati wapiganiaji uhuru Waafrika walipokamatwa.

Aliamka asubuhi na kupata nyumba yake ikiwa imezingirwa na maafisa wa usalama. Alizuiwa nyumbani lakini hakutupwa gerezani kama viongozi wengine.

Anafichua kuwa hakuwa Mau Mau bali alikuwa akiwasaidia kwa chakula na maji walipotorokea magharibi mwa Kenya.

Ni baada ya hali ya hatari kuondolewa 1960 ambapo Otiende aliweza kutoka nje ya nyumba yake na kushiriki siasa.

“Nashukuru ndugu zetu kutoka Kati ya Kenya walitekeleza jukumu muhimu katika kupigania uhuru kwa sababu masuala ya ardhi yalikuwa tata eneo hilo. Wengi wetu tulijitolea sana lakini hatutambuliwi kama wapiganiaji uhuru,” alisema.

Serikali ya kikoloni iliporuhusu vyama vingi vya kisiasa, Otiende aliongoza Abaluyia People’s Union na alitembelea maeneo mengi Magharibi mwa Kenya na kuwa na marafiki wengi.

Alipoamua kugombea ubunge, alikuwa na nafasi nzuri kwa sababu alikuwa amekutana na watu wengi na alifahamu matatizo ya eneo hilo. Baadaye alipokuwa waziri alitumia watu aliojuana nao aliposimamia Local Native Council.

Katika baadhi ya maeneo ya baraza hilo na hasa kaskazini (Kimilili na Lugari), ardhi iliyonyakuliwa na walowezi ilikuwa suala tata na Otiende alitetea ikarudishwa. Kutokana na juhudi za Waafrika, serikali ya Wakoloni ililazimika kufanyia mageuzi siasa za uwakilishi mwishoni mwa miaka ya 1950s. Kwenye uchaguzi wa Legislative Council wa 1957 maeneo manane yalibuniwa. Otiende aliamua kugombea kiti cha eneo la Nyanza North dhidi ya Masinde Muliro na W.W.W. Awori, miongoni mwa wengine.

Muliro alishinda lakini Otiende aliendelea kuhudumia watu katika nyadhifa tofauti. Uchaguzi ulipokaribia, mageuzi zaidi yalifanywa- East African Common Services Organisation chini ya East African Legislative Council ilianzishwa 1960 na ikawa wawakilishi wake wachaguliwe.

Otiende alichaguliwa katika baraza hilo ambalo jukumu lake lilikuwa ni kusimamia huduma zilizofanana Kenya, Uganda na Tanzania. Aliteuliwa mwenyekiti wa idara ya jamii na utafiti wa kisayansi na kuhudumu kwa miaka miwili hadi 1966.

Otiende atakumbukwa kama mmoja wa walioweka msingi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki 1967 na kubuniwa kwa mashirika kama East African Railways, the East African Harbours and the East African Posts and Telecommunications. Kabla na baada ya uchaguzi, Otiende alijiunga na Kanu kwa sababu anasema alitaka kuunganisha nchi.

“Nilibaki Kanu kwa sababu nilitaka nchi iungane. Uhuru haukuwa wakati wa kuanzisha na kushughulika na vyama vya kikabila,” alieleza.

Wakati wa uhuru alikuwa mwakilishi wa East African Legislative Council kuanzia 1960, alichaguliwa kuwakilisha Vihiga kwenye uchaguzi wa Mei 1963. Jomo Kenyatta alipotangaza baraza lake la kwanza la mawaziri, alimteua Otiende waziri wa Elimu na Utamaduni kwa sababu alikuwa amesomea ualimu Makerere-na alikuwa na ujuzi baada ya kufunza Alliance na Jeans School na kujitolea kwake katika vita vya uhuru.

Kenya ilipokuwa Jamhuri 1964, Kenyatta alimteua Otiende waziri wa Afya na Makao ambapo alianzisha ujenzi wa nyumba za makazi kote nchini. Mtaa wa Otiende eneo la Lang’ata, Nairobi, ulipewa jina hilo kwa heshima yake.

Kuhusika kwake katika masuala ya kitaifa kulimfanya apoteze kiti chake cha Vihiga aliposhindwa na Peter Kibisu kwenye uchaguzi wa 1969. Otiende anaeleza kuhusu kushindwa kwake: “Kati ya uhuru na 1969, Kenya ilibadilika haraka sana.

Viongozi waliacha kuchaguliwa kwa sababu ya tajiriba na mchango wao kitaifa. Tabia ilianza ambapo watu walianza kuthamini pesa kupima uwezo wa kisiasa.”

Baada ya kushindwa, Otiende aliacha kushiriki siasa kwenye uchaguzi. Mnamo 1981 aliteuliwa mwenyekiti wa Bodi ya Maziwa wadhifa alioshikilia hadi 1984. Mnamo miaka ya 1980s wakati wa kilele cha udikteta wa Kanu, Otiende alikihama chama hicho tawala kuungana na Jaramogi Odinga, na wengine kupigania demokrasia.

Chama cha Forum for the Restoration of Democracy (Ford) kilipobuniwa 1991, alikataa ushawishi wa Kanu kurejea katika chama hicho. Alijiunga na Ford.

Chama hicho kilipovunjika kuwa Ford-Asili na Ford-Kenya, Otiende alijiunga na Ford Kenya na kuwa mwenyekiti wa tawi la Vihiga.

Wakati Raila Odinga na Wamalwa Kijana walipozozania uongozi wa Ford-Kenya, Otiende alikuwa miongoni mwa waliojaribu kuwapatanisha na juhudi hizo zilipogonga mwamba alivunjika moyo na kuhama chama hicho.

Otiende anaishi Vihiga ambapi anafanya utafiti wa dawa za kienyeji na watu wengi humtembelea kwa ushauri.

You can share this post!

ODM yaponda washirika ‘kuweka ushindani’ Kibra

Raila ametuzuia kufikia Rais – wabunge

adminleo