Mwanaume achimba pango na kuishi na familia yake chini ya ardhi Busia
KATIKA kijiji cha Boro Nango, Wadi ya Marachi Magharibi, Eneobunge la Butula Kaunti ya Busia, familia moja imejenga nyumba chini ya ardhi.
Bw Kevin Onyango, 30, alijenga nyumba hiyo ya kipekee chini ya ardhi miaka sita iliyopita.
Sasa ni kivutio kwa watu wengi huku wanakijiji wakibaki vinywa wazi.
Baba huyo wa watoto watatu anasema, hatua ya kujenga nyumba hiyo, ni baada ya kutatizika kupata makao alipohamia mashinani kutoka mjini.
“Nilikuwa ninafanya kazi mjini, niliporudi ili kuanza maisha yangu nyumbani, nilikosa sehemu ya kulala nikiwa na mke wangu na watoto. Kulingana na mila za hapa kwetu, iwapo umeoa, huruhusiwi kulala katika chumba cha jikoni na hiyo ndio sehemu pekee ilikuwa imebaki. Nilielekezwa kwenda kulala kwa nyanyangu, ni mbali kidogo kutoka hapa, kisha mzozo ukazuka,” alieleza Bw Onyango.
Bw Onyango alifahamu kuwa pendekezo lililotolewa na ndunguze lilikuwa la kumzuia kujenga kwenye boma lao kutokana na shamba lao kuendelea kuwa kidogo kwa familia.
Bw Onyango ambaye ni mwanamuziki, mtindo wa Ohangla, aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa wazo hili limetimia kupitia ndoto.
Alisisitiza ndoto hiyo ilimpa taswira ya jinsi nyumba yake ingekuwa chini ya ardhi.
“Niliamka usiku huo, nikachukua kitabu na kalamu kuchora picha ile niliona kwenye ndoto. Nyumba yangu ni ya udongo lakini nilitumia miti kadhaa ili kuipa msingi thabiti,” alieleza Bw Onyango.
“Mwanzo nilianza kuchimba na kutoa mchanga ili kutengeneza nafasi mwafaka ya nyumba yangu.”
Hutegemea nguvu ya jua kupata mwangaza nyumbani humo.
Changamoto
Kabla ya kujenga, alifahamisha mama yake mzazi ambaye alipinga wazo hilo.
Kadri muda ulivyosonga ndivyo alipata himizo kujenga nyumba hiyo.
“Nilipomwambia mama ninataka kujenga, alikataa kabisa. Nilisikitika kwa kuwa nilijua sehemu ya juu itatumika kuendeleza kilimo,” aliongeza Bw Onyango.
Pia, Bw Onyango hukabiliwa na changamoto wakati wa mvua kubwa ambayo husababisha kuta za nyumba yake kuwa na unyevuunyevu.
“Kwenye ukuta huu utaona unyevu unyevu ambao unachangia kuharibu baadhi ya vitu vyangu. Lakini ninafurahi kuishi sehemu hii ambayo ina utulivu mwingi.”
Bw Onyango amejitahidi kufuga kuku katika chumba hicho kuwa njia ya kujitegea uchumi.