Mwenyekiti wa Magavana: Hakuna kingine kizuri zaidi ya SHA sababu NHIF haipo tena
BARAZA la magavana (CoG) limepigia debe bima mpya ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) likisema manufaa yake yana uzito kuliko changamoto ambazo zimeripotiwa katika vituo vya afya tangu ianze kutekelezwa Oktoba 1, 2024.
Akizungumza katika Kaunti ya Turkana walipohudhuria tamasha za utamaduni wa Waturkana maarufu tobong’ lore, Mwenyekiti wa CoG Ahmed Abdullahi, ambaye pia ni Gavana wa Wajir, amesema changamoto zinazoshuhudiwa ni za kawaida katika mchakato wa utekelezaji wa mradi wowote mpya.
“Sisi Wakenya huwa na msukumo wa kupinga kila kitu kutoka kwa serikali hata kama ni kizuri,” alisema Gavana Abdullahi mnamo Ijumaa Oktoba 25 akiwa Lodwar.
“Ninataka kuwaambia Wakenya kuwa hakuna kitu kingine kizuri zaidi ya SHA kwa sababu NHIF haipo tena.”
Akikariri msimamo wa CoG, Gavana wa Tharaka Nithi anayehudumu katika wadhifa wa Mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika baraza hilo Muthomi Njuki, amesisitiza haja ya umma kukumbatia bima ya SHA kikamilifu.
“Ninaomba wananchi waunge ajenda ya serikali kama hii ya afya. Tunataka wakenya wajiandikishe ili wanufaike na mpango huu,” alisifu bima hiyo Gavana Njuki.
Makato
Wakenya sasa wanakatwa asilimia 2.75 ya mapato yao kwa SHA yenye malengo ya kufanikisha huduma sawa za afya kwa wote.
SHA imechukua nafasi ya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) kwa lengo la kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kupitia nyongeza ya makato ya kila mwezi.
Wagonjwa waliokuwa wakitegemea Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF) wanaendelea kutatizika huku mpango mpya wa Afya ya Huduma ya Jamii (SHIF) ukifeli hata serikali iliposisitiza kila Mkenya anafaa kujisajili.
Hata hivyo, baadhi ya hospitali zimekataa kuhudumia wagonjwa waliohitaji huduma muhimu wanaotegemea bima ya taifa ya afya.