Makala

Mwigizaji Victor Nyaata alitamani sana kuwa mchezaji wa basketiboli

November 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

VICTOR Nyaata alizaliwa katika Kaunti ya Kisii na alitamani sana kuwa mchezaji wa mpira wa basketiboli.

Kando na mapenzi yake kwa mchezo huo, alikuwa mcheshi sana na marafiki zake walimpenda sana kwa hilo.

“Nilijitahidi sana hasa nilipojiunga na shule ya upili nikidhamiria kujiunga na timu ya shule lakini kocha aliniambia kuwa nilikuwa mfupi sana na hivyo singeweza kucheza. Hii ilinivunja moyo sana,” anasema Nyaata.

Mwalimu aliyekuwa akifunza drama na uigizaji alimjia akitaka ajiunge na klabu hiyo ili kujaza pengo katika mojawapo ya michezo ya kuigiza iliyokuwa ikiendelea.

“Tulipoenda katika mashindano na shule mbalimbali katika eneo hilo, shule yetu iliibuka nambari moja, jambo ambalo lilinitia moyo zaidi,” anasema Nyaata.

Baada ya mashindano hayo, Nyaata alianza kutia bidii katika uigizaji ambao alitaka kufanya baada ya masomo.

Alipojiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta mwaka 2010 kusomea taaluma ya Teknolojia ya Habari (IT), aliacha baada ya mwaka wa pili alipopata kazi ya uigizaji wa vitabu vya fasihi vinavyotahiniwa katika shule mbalimbali.

Mwaka 2016 alianzisha uigizaji wa video fupi (vines) kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook katika ukurasa ujulikanao kama ‘Mkisii ni Mkisii’.

Kufikia sasa, amejiunga na kushiriki uigizaji katika vipindi vya baadhi ya televisheni nchini ikiwemo Trap House cha NTV na Sunday School Academy kinachopeperushwa na KU TV.

Ameweza pia kuwa mhusika katika zaidi ya michezo 20 ya kuigiza.