Mzozo waibuka kuhusu uhalisi wa saini katika wosia wa Kibaki
FAMILIA ya aliyekuwa rais, Mwai Kibaki, inavutana na mwanamume anayedai kuwa mwanawe, katika mzozo mpya wa kisheria kuhusu wosia wake.
Mwanamume huyo, Jacob Ocholla Mwai, amewasilisha kesi katika Mahakama Kuu ya Nairobi akidai saini kwenye wosia ulioandikwa Desemba 23, 2016 sio ya Kibaki na ni ghushi.
Pia, ameibua madai kuhusu lugha ya Kibaki kwenye wosia akiagiza watekelezaji jinsi ya kusimamia mali yake kupitia kampuni.
Bw Ocholla anasema maneno ya Kibaki, yanaonyesha kuwa kulikuwa na wanufaika wengine mbali na watoto wanne waliotajwa kwenye wosia na kwamba wanaweza kuwa yeye na Bi JNL, mwanamke anayedai kuwa bintiye Kibaki.
‘Wosia wa mwisho wa Mwai Kibaki wa Desemba 23, 2016 ni batili kwa sababu saini yake katika ukurasa wa uthibitisho ni ya kughushi,’ asema wakili wa Bw Mwai Omoke Morara katika stakabadhi za kesi mahakamani.

Bw Ochola pamoja na Bi JNL waliwashtaki watoto wanne wa Kibaki—Judy Kibaki, David Kagai, Jimmy Kibaki na Anthony Githinji—mwaka wa 2022 wakipinga ugavi wa mali yake na kutaka washirikishwe kama warithi. Wanne hao ndio watekelezaji wa wosia.
Awali, Bw Ocholla na Bi JNL walitaka mahakama iamuru kufukuliwa kwa mwili wa Kibaki kwa uchunguzi wa DNA ili kusuluhisha mzozo kuhusu uhusiano wa kibiolojia na marehemu Rais, lakini familia ilipinga ikitaja ukiukaji wa faragha yao.
‘Mawakili wa Bw Ocholla na Bibi JNL wamefanikiwa kupata hati ambazo zina saini zisizo na shaka za Mheshimiwa Mwai Kibaki, CGH (Marehemu). Zinajumuisha saini yake katika Mazungumzo ya Maridhiano ya Kitaifa Kenya na Makubaliano ya Utekelezaji wa Pendekezo la Tume ya Uchunguzi wa Ghasia za Baada ya Uchaguzi ya Desemba 16 2008,” asema wakili huyo.
Pia, walipata saini za Kibaki kwenye taarifa yake kama shahidi katika klesi ya iliyokuwa katika Mahakama Kuu ya Nyeri mnamo Septemba 2013.
Mnamo Desemba 11, 2024 Bw Ocholla na Bi JNL walishirikiana na mkaguzi wa uchunguzi wa stakabadhi, Bw Martin E. Papa, kuchunguza na kuchanganua saini zilizotajwa ikilinganishwa na ile iliyo kwenye wosia.
Ripoti ya mtaalamu huyo ilifichua tofauti zinazoibua shaka kuhusu uhalisi wa wosia huo.