Makala

Naam, tunatumia program ya kujua mtu alipo ila hatufichui siri kwa polisi, Safaricom yajitetea

Na CHARLES WASONGA November 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KAMPUNI ya mawasiliano ya Safaricom hatimaye imekiri hutumia programu ya kampuni ya Neutral Technologies ilinayodaiwa kutumiwa na kampuni za mawasiliano kutoa data za kibinafsi kusaidia polisi kuendeleza utekaji nyara.

Hata hivyo, kampuni hiyo imefafanua kuwa hutumia programu hiyo kufanikisha usakaji wa walaghai wa kifedha pekee.

“Kampuni ya Neutral Technologies inayo sifa kimataifa na huendesha shughuli zake katika zaidi ya nchini 30 kusaidia kampuni za mawasiliano kugundua na kuzuia ulaghai wa kifedha. Hii ndio maana mnamo 2012 Safaricom ilikodi Neutral Technologies kutekeleza mfumo wa kudhibiti ulaghai wa kifedha katika laini zetu zote,” Safaricom ikasema Alhamisi kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

“Hata hivyo, programu hii haitumiki kufanikisha utoaji wa data au maelezo ya wateja wetu kwa watu wengine, wakiwemo maafisa wa usalama,” ikaongeza.

Safaricom ilitoa ufafanuzi huo kufuatia ripoti maalum iliyochapishwa katika gazeti la Daily Nation, toleo la Oktoba 29, 2024 ambapo ililaumiwa kwa kutoa data za wateja wake kwa polisi kufanikisha utekaji nyara.

“Tunaheshimu usiri wa wateja wetu na tunazingatia kikamilifu sheria za nchi hii za kulinda data. Kwa hivyo, huwa hatupeani data zozote za mteja wetu yeyote ila inapohitajika kupitia agizo la mahakama,” kampuni hiyo ikasisitiza.

Ripoti hiyo maalum iliyochapishwa kufuatia uchunguzi ulioendeshwa na wanahabari kwa mwezi mmoja, inaanika jinsi polisi wamekuwa wakipata data za mawasiliano ya simu za wateja wa kampuni za mawasiliano na kuzitumia kuwateka nyara watu wanaosawiriwa kuwa wakosoaji wa serikali.

Hatimaye baadhi ya wanaotekwa nyara hupatikana wameuawa na miili yao kutupwa kwenye misitu au kando mwa mito.

Wakati huu familia ya wakili John Eric Wesonga almaarufu Lavani Milam, inataka mpendwa wao aachiliwe baada ya kutekwa nyara na watu wasiojulikana katika eneo la Ruaka, kaunti ya Kiambu.

Kulingana na familia hiyo, Wesonga ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali, alichukuliwa mnamo Jumanne Oktoba 29 saa tisa na dakika 30 alasiri na simu yake ikazimwa.

Naye mwanablogu mbishani Scophine Aoko Otieno maarufu kama Maverick Aoko, alitoweka wiki hii na hajapatikana.

Rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) Faith Odhiambo na wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu wameendeleza shinikizo za kutaka Aoko aachiliwe.

Nao mabalozi wa mataifa kadhaa ya Ulaya Alhamisi wametaka serikali kukomesha visa vya watu kutekwa nyara kiholela na maafisa wa usalama.

Kwenye taarifa mabalozi hao wa Ujerumani, Finland, Ireland, Uingereza, Uswidi na Uholanzi, wameitaka serikali kuheshima Katiba yake inayolinda haki ya kimsingi ya raia.

Kulingana na ripoti ya Daily Nation, Safaricom ilikodi huduma za Neutral Technologies ili kuunda programu itakayotumika na maafisa wa polisi kufikia rekodi za simu zinazopigwa na wateja wa kampuni hiyo.

Data hizo maarufu kama CDRs husheheni maelezo kadhaa kuhusu mteja fulani, ikiwemo mahala alipo na watu aliowasiliana nao.

Ni maelezo hayo ambayo, kulingana na ripoti hiyo, huwasaidia maafisa wa usalama kufanikisha utekaji nyara wa watu, kwa urahisi zaidi.