Makala

Nakhumicha ataka aombewe apate kazi baada ya Ruto kumpiga Kalamu

Na CHARLES WASONGA October 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Waziri wa Afya Susan Wafula Nakhumicha amemtaka Kiongozi wa Kanisa la Kianglikana Nchini (ACK) Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit amwombee apate kazi nyingine.

Akiongea Jumamosi alipohudhuria mazishi ya mamake Gavana wa Bungoma Ken Lusaka,  Rodah Lusaka, Bi Nakhimicha alikiri kuwa amekuwa akipitia wakati mgumu tangu alipopoteza kazi yake ya uwaziri.

Hata hivyo, alisema Mungu amekuwa mwema kwake na kwamba anatarajia mema hivi karibuni.

“Askofu uniombee. Hali haijakuwa rahisi kwani baada ya kuhudumu kuitwa waziri sasa nimesalia tu Nakhumicha. Jina langu limekuwa la kipekee, ukiita tu Nakhumicha watu wanasema ni yule Mama wa Wizara ya Afya. Naomba uendelee kuniombea kwa sababu Mungu amenilinda na ninatarajia mema,” akaeleza.

Baada ya Rais William Ruto kuwafuta kazi mawaziri wake 21 mnamo Julai 11, 2024 isipokuwa Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Nakhumicha ni miongoni mwa 11 ambao hawakuteuliwa tena.

Wengine walikuwa Waziri wa zamani wa Elimu Ezekiel Machogu, Moses Kuria (Utumishi wa Umma), Eliud Owalo (ICT), Zacharia Njeru (Maji), Mithika Linturi (Kilimo), Aisha Jumwa (Jinsia) na Penina Malonza (Utalii).

Wengine walikuwa Profesa Njuguna Ndung’u (Fedha), Ababu Namwamba (Michezo), Florence Bore (Leba) na Simon Chelugui (Vyama vya Ushirika).

Walioteuliwa upya walikuwa Profesa Kithure Kindiki (Usalama), ambaye ndiye wa pekee aliyerejeshwa katika wizara yake ya awali. Wengine waliohamishiwa wizara zingine ni; Alice Wahome (kutoka Maji ya Ardhi), Kipchumba Murkomen (kutoka Uchukuzi hadi Michezo), Davis Chirchir (kutoka Kawi hadi Uchukuzi), Alfred Mutua (kutoka Utalii hadi Leba), Justin Muturi (kutoka Mkuu wa Sheria hadi Wizara ya Utumishi wa Umma),  Rebecca Miano (Ustawi wa Maeneo kame hadi Utalii), Aden Duale (kutoka Ulinzi hadi Mazingira), Soipan Tuya (Mazingira hadi Ulinzi) na Salim Mvurya (Uchimbaji Madini hadi Biashara).

Watu wageni walioteuliwa ni pamoja na Andrew Karanja (Kilimo),  Eric Muuga (Kilimo), Debra Barasa Mlongo (Afya), Julius Migos Ogamba (Elimu) na Dkt Margaret Nyambura (ICT).

Wengine ni viongozi wa zamani wa ODM ambao ni; John Mbadi (Fedha), Opiyo Wandayi (Kawi), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika), Hassan Joho (Uchimbaji Madini) na Beatrice Askul Moe (Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki)

Hatamu ya Bi Nakhumicha katika Wizara ya Afya ilizongwa na migomo kadhaa ya madaktari na wahudumu wengine wa afya.