Makala

NAOMIE OLANDO: Nilianza kuigiza kimzaha lakini sasa nategemea sanaa hii

April 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

AKIWA mdogo alitamani sana kuhitimu kuwa daktari wa magonjwa ya binadamu kama taaluma yake, lakini leo hii anaorodheshwa kati ya wanawake wanaovumisha sekta ya biashara hapa nchini. Baada ya ndoto hiyo kuambulia patupu alianza kutamani kuonekana kwenye runinga.

Hata hivyo, Naomie Ramtu Olando anajivunia kushiriki vipindi kadhaa ambavyo vimebahatika kupata mpenyo na kupeperushwa kwenye runinga.

”Kiukweli masuala ya maigizo nilianza kama mzaha mwaka 2016 ambapo tangia kipindi hicho, kando na kufanya biashara huwa napata nafasi kushiriki filamu nafasi inapotokea,” alisema na kuongeza kuwa ingawa anapania kuanzisha brandi ya kuzalisha filamu mwanzo wa ngoma analenga kujifunza masuala kadhaa kuhusu maigizo.

Ingawa hajajitolea kabisa kushiriki maigizo anasema angependa zaidi kufikia viwango vya Taraji P. Henson kati ya wasanii walioigiza katika filamu kama ‘Empire’ na ‘Cookie’ miongoni mwa zinginezo.

”Bila kumpigia debe uigizaji wake huwa wa kuvutia maanake huwa kila nafasi anayopewa anajua kuitoa vizuri kama iliandikwa kutoka kwa maisha yake,” akasema.

Msanii huyu akifahamika kama Mama Sue anajivunia kushiriki kipindi cha ‘Sue and Johnnie’ kilichopeperushwa kupitia Maisha Magic East ndani ya miaka mitatu.

Kipindi hicho kilizalishwa na kundi la Phil-it Productions. Kadhalika amebahatika kushiriki kipindi cha Selina (Multa Productions) na Twisted Roses (Kadi Productions).

Kando na hayo anasema anacho kipaji tosha katika maigizo ambapo ana imani anapata nafasi kushiriki filamu zingine miaka ijayo kwa kuzingatia uigizaji hauna umri.

Mwana dada huyo aliyezaliwa mwaka 1979, anasema huwa anatamani sana kufanya kazi na wasanii mbali mbali humu nchini pia Afrika ili kupata nafasi kukuza talanta yake.

Kwa wana maigizo wa humu nchini anapenda kushirikiana nao Angie Magio na Aisha Mwajumlah walioigiza filamu kama ‘Maza’ na ‘Pete’ (zote DSTV/GoTV) mtawalia.

Kwa wasanii mahiri wa Afrika ambao hushiriki filamu za Kinigeria (Nollywood) anasema angependa sana kufanya kazi nao: Patience Ozokwor ‘Blood Sister,’ ‘The Wedding Party 2’. Pia yupo Genevieve Nnaji ‘Games Women play,’ na ‘Lionheart’. Alisema kuwa katika uhusika wao wasanii hao huwa wanashiriki kwa kujitolea katika nafasi zozote.

”Pia natoa pendekezo kwa maprodusa wa humu nchini wawazie zaidi kuzalisha filamu zinazoangazia utamaduni wetu ili kuvutia wafuasi wa humu nchini,” alisema na kuongeza kuwa suala hilo limefanya wapenzi wa burudani kupenda sana kutazama filamu za kigeni.

Anashauri wasanii chipukizi kuwa endapo wanahisi wana talanta wasisubirie miaka iende mbali muda ndio huu watafute jinsi ya kuingia katika ulingo wa maigizo.

Anahimiza wasanii wanaoibukia kwenye gemu kuwa uigizaji siyo mteremko unahitaji nidhamu, kujitolea na kujituma bila kulegeza kamba pia kumtegemea Mungu zaidi.

Pia anawaambia kamwe wasipuuze masomo maana ndiyo msingi wa kila jambo wanalofanya. Anahimiza wanawake wenzake kuwa wanastahili kuvaa vizuri na kujiheshimu ili kujihepusha na wanaume ambao hupenda kushusha wanawake hadhi.