Makala

NASAHA: Jiandae kisaikolojia kukabiliana na halamba halumbe zijazo za masomo

September 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na HENRY MOKUA

HUKU shule zikitarajiwa kufunguliwa karibuni, pana haja ya maandalizi ya kisaikolojia miongoni mwa maandalizi mengine kwa washika dau wote.

Maandalizi mengine yote yakifanikiwa ya kisaikolojia yakasalia huja matarajio, matazamio yetu yakakosa kufikiliwa.

Likizo hii ndiyo ndefu zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa miaka ya hivi karibuni. Kwangu, ndiyo ya kwanza kuwahi kuwa ndefu zaidi. Urefu wenyewe umezua mengi mazuri na mabaya kwa wakati mmoja. Je wahitaji kufanya nini…mimi je?

Kwako mwanafunzi ambaye umetanabahishwa na habari za kufunguliwa kwa shule mapema kuliko ulivyotaraji, kumbuka hakuna kilicho aushi duniani kinachodumu ni mabadiliko!

Ninajua ni wanafunzi wa kuhesabu wamekuwa na uhusiano wa karibu na vitabu vyao tangu tangazo kwamba shule zingefunguliwa Januari kutolewa. Wengine wote walivipa breki hadi sasa.

Nimewaona wachache, hasa watahiniwa wakianza kuvikungúta vumbi tangu makisio kwamba kufunguliwa kungewadia mapema kuanza.

Ingawa awali wakijiambia: msiba wa wengi ni harusi, sasa wanaanza kuukubali ukweli kwamba kila mmoja atapata alama inayowiana na maandalizi yake. Kinachonisikitisha daima ni mimi mwenyewe au mwingine yeyote kukosa kuyafikilia malengo yake kutokana na sababu zinazoweza kuepukika…tuziite visingizio.

Kwa muda uliosalia kabla ya shule kufunguliwa, nakuomba ewe mwanafunzi ujinyime na kujituma kadri uwezavyo kuufidia muda uliokwisha kuupoteza. Hivi ni kwa sababu nisemavyo mara kwa mara, maumbile yana mazoea ya kuweka rekodi ya kutowajibika kwako kisha yakakuadhibu baadaye.

Isitoshe, Mwenyezi Mungu mwenyewe akikupa uwezo ukautelekeza una hakika ya kutwaliwa talanta na uwezo huo aliokupa akapewa mwingine.

Wacha mzaha ewe mwanafunzi! Jitathmini upya ikiwa umeusahau uwezo wako kamili. Ukisha, mtafute unayeweza kushauriana naye kuhusu ndoto zako akakuhamasisha. Aweza kuwa mzazi wako, ndugu yako, rafiki yako, mtaalamu wa masuala ya taaluma, mnasihi. Mweleze bayana unayotaka kuyafikilia maishani.

Mwombe akupe maoni yake waziwazi kuhusu anavyouona uhusiano wako na ndoto zako. Je mnachukuana ama pana pengo kubwa? Waweza kufanya nini kulipunguza pengo lenyewe hatua kwa hatua hadi ukafikia panapofaa? Sema na mwingine kisha mwingine halafu uyalinganishe maoni yao.

Hakikisha unajiambia ukweli pia. Ikiwa wahitaji kujinyima zaidi, fanya vile. Ukigundua ndoto zako haziwiani kabisa na nafsi yako, ziwazie tena, jiweke kwenye ratili upya.

Ewe mzazi mwenzangu, wacha msongo! Si wewe tu uliyebugia karo yote ya mwanao mwaka huu! Mbona ujiruhusu kuugua wakati wengine wengi wapo katika hali yako na wametulia.

Ni kweli kwamba hili si suala la kuonea fahari, lakini ikiwa ndiyo uhalisia, utafanya nini? Tulia, anza kuweka mikakati upya ikiwa kama mwanao ulidhani shule zisingefunguliwa hivi karibuni.

Waza taratibu, kwa makini kuhusu mbinu utakazozitumia kupata karo itakayohitajika katika muhula unaotarajiwa kuanza.

Kisa na sababu ya kukunasihi usijipe shinikizo ni kwamba aghalabu, unapokuwa umejitesa na kujiumiza, unagundua suluhu ya changamoto yako ilikuwa karibu nawe tu. Kwa hivyo wazia namna ya kumkimu mwanao anapojiandaa kurejea shuleni bila kujihangaisha kupita kiasi.

Mwalimu mwenzangu…changamka! Wengi wanazidi kutuonea imani wanapoiwazia hali inayotusubiri.

Baadhi yao ni wanafunzi wenyewe, wazazi. Wanashangaa ikiwa tutawahi kuidhibiti hali baada ya wanafunzi wetu kujiingiza katika kila aina ya hulka katika likizo ndefu hii inayoelekea kutamatika.

Labda umeyasikia mengi mengine hapo ulipo. Lililo hakika ni kwamba maji tuliisha kuyavulia nguo, sharti tuyakoge.

Mwalimu, wewe ni sawa na betri mpya kwenye gari jipya! Hivi utashindwa kuizindua betri ya gari lililokwama na kuliamsha kabisa?

Nina hakika ari unayo ya kuufanya mustakabali wa kila mwanafunzi wako uwe bora kuliko hata wako mwenyewe…mbinu unazo na fursa pia, katu usiutelekeze wajibu wako. Kumbuka walimu wako walijihini na kutoa kijasho kukunyoosha, hutokosea kulipa deni!