Makala

NASAHA: Ramadhani ni fursa ya kuzitakasa nafsi zetu na kuacha maasi

May 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA KHAMIS MOHAMED

KWA majaaliwa ya Mwenyezi Mungu, tumeingia siku ya 16. Palipo na uzima ni wiki mbili tu zimesalia mwezi huu mtukufu kuondoka.

Ndugu Waislamu, tulio na nyoyo zilizojaa dhambi, njooni tupae mbinguni kwa pamoja kwa kutumia mabawa ya toba ili tupate kunufaika na rehema, msamaha na maghfira ya Mwenyezi Mungu katika mwezi huu mtukufu wa ramadhani.

Ni fursa nyingine adhimu ya kutenda mema na kuacha mabaya tuliokuwa tukiyatenda katika kipindi kingine chote cha miezi mingine.

Tuko katika mwezi ambao Mtume Muhammad (SAW) alisema hivi kuuhusu: ‘Unakuja katika nyoyo kwa baraka na maghfira na kwa siku kadhaa kutua katika nyoyo za waumini wenye hamu ya kutubia na kuomba maghfira na kuacha maasi.

Katika kufunga kwake Muislamu hupata mafunzo ya kutenda mema na kuacha mabaya ndio maana tunashuhudia kwa kiasi kikubwa maasi kupungua katika mwezi huu.

Waislamu,ambao walikuwa walevi, wazinzi, wapigaji kabari, wezi wa kimabavu alhamdulillahi wamesitisha matendo hayo kwa sababu ya kufunga mwezi mtukufu.

Hakika hapa ndipo ambapo jamii ya Waislamu tunatakiwa kujitathmini na kutafakari. Je, baada ya mwezi hii ya kufunga ikiisha tutarudi katika maasi yaliokolea katika nafsi zetu, ama tutachukua njia ya uchaji Mungu?

Tuchukue fursa hii kubadilisha tabia zetu kikamilifu. Tutubie tauba ya kikweli.

Tumeelezwa kwamba mwenye kutubia anatakiwa atomize mashariti matatu ambayo ni kuacha maasi kabisa,kujuta kufanya maasi,kuazimia kuwa hatorudia tena maasi hayo.

Lakini inavyoonekana wengi wetu ni kama tunamchezashere Mwenyezi Mungu aliyetukuka kwa kuacha madhambi na maasi mwezi wa Ramadhan peke yake, tukidhani kwamba Mwenyezi Mungu ni wa Ramadhan pekee.

Hivi sasa Misikiti zimechangamka, lakini tukifikia mwisho mwisho ya mwezi wa ramadhani tunaghura msikiti. Waislamu tujitathmini.

Ramadhani ni chuo cha mafunzo ya ucha Mungu.

Ndugu zangu katika Imaan naiusia nafsi yangu na zenu kuzitakasa nafsi zetu ziwe katika daraja ya nafsi zilizotulia, kwa asili nafsi zimeumbwa kwa asili kuwa na Matamanio, hivyo tumuombe Allah atupe Tawfiq tuweze kuzidhibiti nafsi zetu kuzielekeza kwenye Imani thabiti ya Kiislamu na tuzilee mpaka zivutike kwenye hali ya kutenda mambo mema yatakayotukurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hivyo iwe ni sababu ya kupata radhi na Maghfira ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kisha tudumu katika Uongofu wa utakaso wa nafsi zetu mpaka turejee kwa Mola wetu hali ya kuwa ameturidhia.