• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
NASAHA ZA RAMADHAN: Tudumishe heshima ya juu tunaposherehekea Eid ul-Fitr

NASAHA ZA RAMADHAN: Tudumishe heshima ya juu tunaposherehekea Eid ul-Fitr

Na SHEIKH MOHAMED KHALIFA

TUMEFIKA ukingoni mwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Umekuwa mwezi mzima wa kuzitafuta fadhila za Mwenyezidi Mungu (SWT).

Ndani ya Ramadhani, tumevuna mengi. Allah (SWT) amesema mwenyewe kupitia Hadithi Qudsi kwamba saum ni yake yeye na ndiye anayejua malipo ya mtu aliyefunga.

Lengo la kusema saum ni yake si kwamba ibada nyingine hazifanywi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (SWT). La! Ni kwa sababu ibada kama swala, kutoa sadaka, kusoma Qur’ani na kadhalika, malipo yake yanajulikana.

Mtume (SAW) alishawatangazia Waislamu kuwa malipo ni kumi kwa kila herufi. Lakini katika ibada ya kufunga, malipo hayakutajwa ni kiasi gani.

Ina maana Mwenyezi Mungu (SWT), hulipa kila saum ya mtu kulingana na ilivyofungwa. Kuna wale ambao saum zao ni za gredi ya kwanza, gredi ya pili, ya tatu na za chini zaidi. Kwa hivyo aliyezingatia masharti ya kufunga, hupata malipo ambayo wingi wake ni Mwenyezi Mungu (SWT) pekee anayejua.

Basi kwa kuwa tumejitahidi kuifunga saum ipasavyo, bila shaka tumevuna thawabu kwa wingi. Haya ni malipo ambayo yafaa tuyatunze kwa kuchunga jinsi ambavyo tutasherehekea sikukuu ya Idd.

Baa zimefungwa na watu wamekatazwa na serikali kutangamana. Lakini haina maana kuwa ni kila mtu atakayekosa njia ya kusherehekea. Siku ya Eid ul-Fitr ni siku muhimu sana. Mwenyezi Mungu (SWT) huwatuma malaika kwa maelfu kuwasalimia waumini kwa kukamilisha ibada muhimu.

Ni siku ambapo yatakikana kuwe na heshima ya kiwango cha juu. Mwenye kusherehekea kukmilika kwa mwezi wa Ramadhani, yampasa ajue kwamba kufunguliwa kwa shetani kutoka minyororo, si sababu ya Mwislamu kupoteza mazuri yote aliyojibidiisha kuchuma. Hebu fikiri, itakuwaje kama utapambana kwa miaka thelathini kuunda biashara, kujenga nyumba au kuwekeza kisha siku moja uamke na kukuta moto umeteketeza?

Tusiharibu juhudi zetu za mwezi mzima kwa siku moja sababu ya mambo ya kipuuzi kama kupigana, kuanza kutongoza, kukesha kula miraa au matusi.

You can share this post!

TAHARIRI: DCI isafishe ufisadi katika soka ya Kenya

Watu 5 waangamia kwenye ajali

adminleo