Makala

Ndama wa Fred Machoka aliyezaliwa Jumatano apewa jina Raila Odinga

Na SAMMY WAWERU October 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

NCHI ikiendelea kumwomboleza aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, mwanahabari tajika Fred Machoka amempa mmoja wa ng’ombe wake jina la lakabu la kiongozi huyo. 

Ndama aliyezaliwa jana, Alhamisi, Oktoba 16, 2025, Bw Machoka amempa jina Rao kama ishara ya heshima kwa mwanasiasa huyo mashuhuri.

Ndama wa Fred Machoka aliyepewa jina RA001. PICHA| SAMMY WAWERU.

Bw Odinga aliaga dunia mnamo Jumatano, Oktoba 15, siku moja kabla ya ndama wa Machoka kuzaliwa.

Alifariki India ambako alikuwa akipokea matibabu.

“Sidhani kunaye asiyejua Bw Raila Odinga ndani na nje ya Kenya. Ni shujaa wa nchi yetu, na ni huzuni kumpoteza. Kwa heshima zake kupigania uhuru wa demokrasia, ndama wa ng’ombe wangu aliyezaliwa jana (Jumatano) nimempa jina la Rao,” mwanahabari huyo wa Shirika la Royal Media akaambia Taifa Dijitali kwenye mahojiano ya kipekee nyumbani kwake Isinya, Kaunti ya Kajiado.

Bw Machoka, ana mradi wa kilimo na ufugaji unaofahamika kama Fred Ranch eneo la Isinya.

Ndama wa Fred Machoka aliyepewa jina RA001. PICHA| SAMMY WAWERU.

Akimwomboleza Bw Odinga, Bw Machoka, alimtaja Waziri Mkuu huyo wa zamani kama Baba wa Demokrasia Kenya kufuatia mchango wake mkuu.

Bw Odinga amemiminiwa sifa na viongozi wakuu nchini, akiwemo Rais William Ruto, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, viongozi nje ya nchi na Wakenya kwa jumla, wakisema utendakazi wake utasalia kwenye nyoyo za wengi.

Mwaka 1992, chini ya utawala wa Rais wa wakati huo, Daniel Arap Moi (marehemu kwa sasa), Raila Odinga pamoja na wanasiasa wengine kupitia vuguvugu walitetea kuzinduliwa kwa mfumo wa vyama vingi Kenya – hatua iliyochangia kukua kwa demokrasia Kenya.

Ng’ombe wa Fred Machoka aliyezaa ndama aliyepewa jina la Odinga, mwanahabari huyo alisema ilikuwa mara yake ya kwanza kujifungua.

Ni ndama maridadi wa kiume, wa mchanganyiko wa rangi ya kahawia na nyeupe.

Ndama RA0 001. PICHA| SAMMY WAWERU.

Kwenye sikio, ana nembo iliyoandikwa Rao 001 na tarehe aliyozaliwa – 16/10/2025.