NDIVYO SIVYO: Kweli mazoea yana taabu, sahihi ni maakuli si 'maankuli' au 'mamkuli'
Na ENOCK NYARIKI
MOJA kati ya maneno mawili yatumiwayo na watu kurejelea chakula ni mlo.
Kuna jingine ambalo aghalabu hukosewa katika matamshi na maendelezo.
Baadhi ya watu hulitamka kama ‘maankuli’ na wengine ‘maamkuli’.
Baadaye katika mjadala huu, tutaonesha maendelezo sahihi ya neno lenyewe na pia kuelezea maana yake hasa. Hata hivyo, matamshi mengine yaliyoshamiri katika mawasiliano ya watu kwa miaka na mikaka na yasiyo sahihi ni pamoja na ‘kambumbu’, ‘kambambe’, ‘kidumbwedumbwe’ na ‘kadada’.
Baadhi ya makosa ya matamshi husababishwa na athari ya lugha za kwanza za watu isipokuwa hilo la ‘maankuli’ na ‘maamkuli’.
Sababu ni kuwa, hata watu ambao hawana shida ya matamshi hujikuta wakilitamka na hata kuliendeleza neno hilo hivyo.
Kabla ya kuingia katika kitovu cha mjadala, ningependa kutaja kwamba Kiswahili sanifu hakina mwambatano wa sauti ‘nk’.
Kwa hivyo, njia mojawapo inayotuthibitishia kuwa neno ‘maankuli’ si sahihi ni kwa kurejelea kanuni hiyo.
Ijapokuwa miambatano mingine yote tuliyoitaja kwa mfano, ‘mb’ na ‘nd’ ipo katika lugha ya Kiswahili.
Kuzichopeka sauti hizo kwa maneno ambayo kiasili hayakuwa nazo husababisha kosa la tahajia.
Mathalani, maendelezo ya neno lenye maana sawa na soka, kandanda au mpira wa miguu ni kabumbu bali si kambumbu jinsi ambavyo hutamkwa na baadhi ya wasemaji.
Kuongezwa kwa sauti ‘m’ kabla ya sauti ‘b’ ya mwanzomwanzo mwa neno husababisha kosa la tahajia. Vivyo hivyo, kudondoshwa kwa sauti ‘n’ katika neno kandanda husababisha kosa kama hilo.
Neno kabambe ni kivumishi ambacho hutumiwa kurejelea kitu chochote kilicho na sifa imara au thabiti au chenye nguvu nyingi. Neno hilo halipaswi kuongezewa sauti ‘m’ kabla ya ‘b’ ya mwanzoni mwa neno. Kwa hivyo kuliendeleza kama *kambambe ni kosa la kisarufi.
Neno kindumbwendumbwe nalo lina maana zaidi ya tatu ila hutumiwa sana katika sajili ya michezo kurejelea mashindano yenye ushindani mkali kati ya timu mbili za mchezo wa kandanda au baina ya wanamasumbwi. Kudondoshwa kwa sauti ‘n’ hali inayolifanya neno hilo kuendelezwa kama *‘kidumbwedumbwe’ ni kosa la tahajia.
Neno maakuli lina maana ya aina yoyote ya chakula kinacholiwa na mwanadamu. Neno hilo halipaswi kuongezewa sauti ‘n’ au ‘m’ kabla ya ‘k’ kwa sababu hali hiyo husababisha kosa la matamshi na tahajia. Alhasili, maadamu utamu wa lugha ya Kiswahili upo katika matamshi, umakinifu mkubwa unahitajiwa wakati wa kuyatamka maneno.