Makala

NDIVYO SIVYO: Mashimo shambani ‘huchimbwa makoongo’ kwa upanzi, hayakatwi

May 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ENOCK NYARIKI

WAKULIMA katika maeneo mengi ya taifa la Kenya wanaendelea kuyaandaa mashamba yao kwa upanzi.

Katika makala haya, nitaiangazia kauli ambayo wakulima hupenda kuitumia katika mazungumzo yao hasa katika msimu huu.

Katika eneo la Oloilien, Kajiado Magharibi, wakulima husema “kukata mashimo” kwa maana ya kufukua mashimo madogo ya kupandia mbegu.

Ingawa Oloilien ni makazi ya makabila mbalimbali, kauli hiyo ‘kukata mashimo’ ambayo yamkini imetokana na lugha ya Gikuyu hutumiwa na takriban watu wengi kwa maana hiyo.

Hata hivyo, wenyeji wa maeneo mengi ya Kati hulitumia neno kuchimba kwa ufaafu pale wanaporejelea kitendo hicho cha kufukua mashimo madogo ya kupandia mbegu.

Neno “kukata” katika maeneno hayo huhusishwa na mitaro.

Kwa hivyo, wenyeji husema “kukata mitaro” kwa maana ya kufanya mitaro kwenye ardhi.

Upo utata katika matumizi ya dhana lima na chimba.

Katika sehemu, kamusi imelifafanua neno “lima” kuwa ni kutayarisha shamba kwa kufyeka na kutifua ardhi kwa jembe.

Hakika hiyo huenda ikawa ni njia finyu mno ya kulieleza neno hilo. Sababu ni kuwa, dhana kilimo – nomino inayotokana na leksimu hiyo – ina maana ya sanaa ya kulima na kupanda mazao shambani.

Katika baadhi ya jamii, neno lima pia huhusishwa na ufugaji. Katika jamii hizo, kauli “kulima kuku” au “kulima nguruwe”( hiyo ikiwa tafsiri ya moja kwa moja) hukubalika kwa maana ya kufuga kuku au kufuga nguruwe.

Katika jamii ya Abagusii, neno “kulima” au “kuchimba” hueleweka kwa maana finyu ya kufukua ardhi kwa ajili ya upanzi.

Kwa hivyo, neno hilo haliwezi kutumiwa kwa maana ya kufukua mashimo ya kupanda mbegu. Tafsiri ya moja kwa moja ya kitendo hicho katika lugha hiyo ni “kupiga mashimo”(goaka ebikamago).

Ufukuaji

Alhasili, jamii ya Wakikuyu hulinasibisha neno kuchimba na ufukuaji wa shimo kubwa na lenye kina ilhali kukata ni kufukua shimo dogo au mtaro. Hata hivyo, dhana hizo zinatofautiana kimatumizi.

Kukata ni kutenganisha sehemu moja ya kitu kwa kisu au kitu chochote chenye makali kama vile upanga au shoka.

Waama, neno hilo halipaswi kutumiwa kwa maana ya kufukua ardhi kwa njia yoyote ile.

Kauli ambayo inapaswa kutumiwa kwa maana ya kufukua mashimo shambani kwa ajili ya kupanda mbegu ni kuchimba makoongo.

Kitendo cha kulima majani juujuu bila ya kuchimbua ni kugwaza. Lakini dhana kugwaza haiwezi kutumiwa kwa maana tuliyokwisha kuielezea.