Makala

NDIVYO SIVYO: Mkanganyiko utokanao na kiwanja, kiwanda na uwanda

June 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ENOCK NYARIKI

KIWANDA na kiwanja ni maneno ambayo hujitokeza aghalabu katika mawasiliano. Hata hivyo, si watu wengi wanaoweza kutenga tofauti baina ya maneno hayo mawili.

Uwanda ni neno jingine la kitaaluma ambalo mara nyingi hutumiwa kwa maana ya eneo fulani la kufanyia utafiti.

Maneno haya matatu yanapojitokeza katika mawasiliano, huibua utata.

Tutaanza mjadala huu kwa kutaja kwamba njia nyingine ya kuliendeleza neno kiwanja ni uwanja.

Jozi nyingine ambayo huwa na tofauti ndogo ya kimuundo kama hii ni ubawa na bawa. Ifahamike kuwa, hali hii huziweka jozi zenyewe katika ngeli mbili tofauti.

Kwa mfano, neno kiwanja ambalo wingi wake ni viwanja liko katika ngeli ya KI-VI ilhali uwanja ambalo wingi wake ni nyanja huingia katika ngeli ya U-ZI.

Jambo jingine ambalo ni muhimu kulifahamu kabla ya kuingia kwenye kitovu cha mjadala ni kuwa si wakati wote ambapo neno uwanja linaweza kutumiwa kwa maana ya kiwanja.

Mathalani, haihalisi kusema ‘kiwanja cha semantiki’ kwa maana ya eneo la fani au taaluma. Badala yake, neno ambalo linapaswa kutumiwa kwa maana hiyo ni uwanja. Kwa hivyo tutasema uwanja wa semantiki, uwanja wa fonetiki, uwanja wa fasihi na kadhalika.

Kuna neno jingine ambalo linakurubiana sana na uwanda na uwanja. Neno hilo ni mawanda. Kamusi Elezi Ya Kiswahili inaeleza kuwa mawanda ni eneo pana la kutalii na liwezekanalo kufikiwa.

Maelezo zaidi ya neno hilo kwa mujibu wa kamusi hiyo ni uwanja mpana wa taaluma fulani.

Neno kiwanja ambalo pia linaweza kuendelezwa kama uwanja lina maana ya ardhi ya kufanyia shughuli fulani kama vile ujenzi au michezo.

Uga

Ardhi yenye nyasi iliyotengwa kwa ajili ya michezo pia huitwa uga.

Hata hivyo, neno uga haliwezi kutumiwa kwa maana ya ardhi iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi.

Neno kiwanda nalo lina maana zaidi ya moja ila maana iliyotamalaki sana katika matumizi (na ambayo inatushughulisha katika makala haya) ni mahali pa kutengenezea bidhaa au vitu.

Sitautamatisha mjadala huu kabla ya kutaja kwamba uwanja, kiwanja, uga na uwanda ni maneno ambayo hayana usawe kamili.

Alhasili, kiwanja au uwanja ni ardhi iliyotengwa kwa shughuli maalumu kwa mfano michezo au ujenzi ilhali kiwanda ni mahali pa kutengenezea bidhaa.

Kamusi ya Karne ya 21 inatoa fasili ya pili ya kiwanda kuwa ni jengo kubwa lenye mitambo au mashine ambazo mafundi au wafanyakazi huzitumia kutengeneza bidhaa.